ICJ: Urusi isitishe mara moja mashambulizi Ukraine
- Mahakama ya haki ya Umoja wa mataifa yaitaka Urusi kusitisha operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine.
Dar es Salaam. Mahakama ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki (ICJ) katika uamuzi wake uliotolewa Machi 16, Hague nchini Uholanzi imesema Urusi isitishe operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine.
Uamuzi wa Mahakama hiyo unafuatia ombi la Ukraine la Februari 27 la kuishutumu Urusi kutumia kisingizio cha mauaji ya kimbari kuhalalisha uvamizi wake wa kijeshi nchini humo.
Majaji 13 kati ya 15 wa mahakama hiyo wameunga mkono ombi la Ukraine kutaka Urusi isitishe operesheni zake, huku majaji wawili, Makamu wa Rais wa ICJ Kirill Gevorgian kutoka Urusi na Jaji Xue Hanging kutoka China wakipinga ombi hilo.
Hata hivyo, majaji wote walikubaliana kuwa pande zote kwenye mzozo huo zijizuie kufanya kitendo chochote kinachoweza kuchochea zaidi mzozo wa sasa au kufanya hali kuwa ngumu zaidi kupata suluhisho.
Katika ombi lake, Ukraine ilieleza kuwa baada ya madai ya uongo ya vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa maeneo ya Luhansk na Donetsk , Urusi ilitangaza na kutekeleza operesheni maalum za kijeshi ili kuzuia adhabu dhidi ya madai yake hayo.
Zinazohusiana:
-
ICC yaelekeza macho yake Ukraine, Urusi ikiendelea na mashambulizi
-
Baraza Kuu la UN laitaka Urusi iondoke Ukraine bila masharti
Akiwasilisha uamuzi wa mahakama, Rais wa ICJ Jaji Joan Donoghue amesema mazingira sahihi yalikidhi kuipatia mahakama mamlaka ya kutoa uamuzi.
Jaji huyo ameeleza kuwa haki zilizosisitizwa na Ukraine zina mashiko na hakuna mauaji ya kimbari yaliyotekelezwa.
“Bila shaka, operesheni yoyote ya kijeshi, hususan inayofanyika katika kiwango kinachotekelezwa na Urusi kwenye eneo la Ukraine, inasababisha vifo, inaleta madhara ya mwili na akili, na inaharibu mali na mazingira,” amesema jaji huyo.
Donoghue ameongeza kuwa ICJ inaona kuwa wananchi wanaoathiriwa na vita vya sasa ni wale walio hatarini zaidi.
“Uvamizi wa Urusi umesababisha vifo vya mamia ya rai na wengine wamejeruhiwa, mali zimeharibiwa ikiwemo uharibifu wa majengo na miundombinu,” amesema.
Mahakama pia imesema kuwa Urusi imekataa kushiriki kwenye mchakato wa kesi hiyo na baadaye iliwasilisha nyaraka kwa kesi hiyo kuwa ICJ inakosa mamlaka na uhalali wa kuisikiliza na hivyo kuitaka mahakama ijizuie kushiriki katika kutoa uamuzi wowote na iondoe shauri hilo mahakamani.
Uamuzi ICJ ni wa kwanza kutolewa na mahakama hiyo tangu Urusi ivamie Ukraine Februari 24, japokuwa uamuzi huo una mashiko, ripoti zinahoji iwapo Urusi itazingatia uamuzi huo, na Mahakama hiyo haina njia ya moja kwa moja ya kuutekeleza.
Latest