Baraza Kuu la UN laitaka Urusi iondoke Ukraine bila masharti

March 3, 2022 1:27 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Matokeo ya kura ya azimio kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine. Picha| UN


  • Yasema uvamizi wa Urusi ni kinyume na sheria za kimataifa.
  • Wajumbe wa Baraza hilo wataka mgogoro huo umalizwe kwa amani.
  • Tanzania haijaonyesha msimamo kuhusu mzozo huo.

Dar es Salaam. Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa limeitaka Urusi iondoke nchini Ukraine na isitishe mashambulizi inayofanya nchini humo kwa sababu yanaathiri raia wasio na hatia wakiwemo watoto.

Katika kikao chake maalum cha dharura kilichofanyika jana (Machi 2, 2022) pia limepitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine linasisitiza azma yake ya kutambua mamlaka ya Ukraine, uhuru, umoja na mipaka yake ya majini na ardhini inayotambulika kimataifa.

Kwa kiasi kikubwa wajumbe wa kikao hicho kilichofanyika New York, Marekani walikuwa na maoni ya kuitaka Urusi iondoe vikosi vyake nchini Ukraine kwa mujibu wa Chata ya Umoja wa Mataifa inayopinga uvamizi wa taifa moja dhidi ya lingine. 

Marekani ilipigia chepuo upigaji wa kura ya ndiyo kwa azimio hilo ambapo mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Linda Thomas-Greenfield amesema “piga kura ya ndiyo iwapo unaamini kuwa taifa lako lina haki ya mamlaka ya mipaka yake na uhuru.”

Hata hivyo, Mwakilishi wa kudumu wa Belarus kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Valentin Rybakov amesema amedai kuwa Belarus kwa upande wake inaratibu mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi lakini cha ajabu hakuna nchi inayotilia maanani. 

“Tunapiga kura ya hapana dhidi ya azimio hili kwa sababu tunaamini azimio hili lilipaswa kuwa na kipengele kimoja tu cha kuepusha chuki na si vinginevyo,” amesema Rybakov.

Rwanda kwa upande wake imesema imeunga mkono azimio hilo kwa kutambua kuwa inaunga mkono Chata ya  Umoja wa Mataifa huku ikisema Urusi na Ukraine ndiyo zenye ufunguo wa kumaliza mgogoro unaoendelea huku.

Imesema harakati zozote za muingilio wa kigeni kwenye mzozo huo utafanya hali kuwa mbaya zaidi.

Mwakilishi wa India kwenye Umoja wa Mataifa Balozi T. S Tirumurti ametaja tukio la kuuawa kwa raia wa India hapo jana kwenye mji wa Kharkiv huku akishukuru nchi jirani na Ukraine ambazo zimefungua mipaka yao kuruhusu raia wa nchi ya tatu kuingia. 

Amesema tayari India imetuma ndege kuchukua wanafunzi wake walioko Ukraine na kusisitiza kuwa India ambayo haikupiga kura kuonyesha msimamo wowote inaamini tofauti zozote zinaweza kumalizwa kwa mazungumzo.


Soma zaidi:


Undani wa azimio la UN

Azimio hilo namba A/ES -11/L.1 limepitishwa kwenye kikao hicho cha 11 cha dharura wakati huu ambapo Urusi inaendelea kuishambulia Ukraine ambapo misingi ya azimio hilo pamoja na mambo mengine ni tangazo la Februari 24 la Rais Vladmir Putin la kuanzisha operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine.

Kikao hicho cha dharura kimeitishwa na Baraza la Usalama, ikiwa ni miaka 40 tangu kikao kama hicho kiitishwe kwa lengo la kulinda amani na usalama duniani.

Wajumbe 141 wamepiga kura ya ndiyo huku 5  wakipiga kura ya hapana na wengine 35 hawakupiga kura yoyote, ambapo kwa mujibu wa kanuni za Baraza Kuu katika kikao kama hicho, kura zinazohitajika kupitisha azimio ni theluthi mbili za wajumbe walioko kwenye kikao.

Azimio linalaani vikali uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ikiwa ni kinyume na kipengele namba 4 cha Ibara ya 2 ya Chata ya Umoja wa Mataifa.

Azimio pia linataka Urusi isitishe mara moja matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya Ukraine na ijizuie dhidi ya vitisho vyovyote kinyume cha sheria au matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya mwanachama yeyote wa Umoja wa Mataifa.

Urusi pia inatakiwa iondoe mara moja na bila masharti yoyote vikosi vyake kutoka eneo la mipaka ya Ukraine inayotambulika kimataifa.

Azimio linataka pia Urusi ibadili kauli yake kuhusu hadhi ya baadhi ya maeneo ya Donetsk na Luhansk huko Ukraine.

Kuhusu misaada ya kibinadamu, azimio linataka pande zote kwenye mzozo huo kuruhusu ufikishaji wa misaada bila vikwazo vyovyote kwa wahitaji nchini Ukraine sambamba na kulinda raia wakiwemo wafanyakazi wanaotoka misaada ya kibinadamu na watu walio hatarini kama vile wenye ulemavu, wanawake, watoto wazee, wahamiaji, na watu wa jamii ya asili.

Miongoni mwa nchi 35 ambazo hazikupiga kura kuonesha msimamo wowote ni Tanzania, Uganda, India, Bolivia, Burundi, Namibia, Msumbiji na Equatorial Guinea.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW