Mamia hatarini kufariki kwa kukosa huduma ya oksijeni Ukraine
- Ni baada ya Urusi kuivamia Ukraine wiki iliyopita.
- Mzozo huo umeathiri huduma za afya ikiwemo oksjeni kwa wagonjwa.
- Urusi na Ukraine kukaa meza moja kumaliza mzozo huo.
Dar es Salaam. Wakati mzozo wa Urusi na Ukraine ukiendelea, Shirika la Afya la Duniani (WHO) limesema kuna upungufu wa huduma ya oksijeni, jambo linalohatarisha maisha ya mamia ya watu wanaohitaji huduma hiyo nchini Ukraine.
Urusi ilivamia Ukraine wiki iliyopita kwa kile kwa kile inachodai inapigania na kulinda maslai na uhuru wa wa majimbo mawili ya Donetsk na Luhansk huku pande mbili zikiendelea na mapigano katika ardhi ya Ukraine.
Katika taarifa ya pamoja ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus na Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Dk Hans Henri Kluge iliyotolewa mjini Geneva Uswis wamesema vita vimesababisha uhaba wa huduma hiyo muhimu na kwamba sasa wanashirikiana na wadau ili kuweka utaratibu salama wa kusafirisha huduma hiyo kupitia Poland.
Viongozi hao wa WHO wamesisitiza kuwa “wakati huu wa janga la Ukraine, afya lazima ibaki kuwa kipaumbele cha kwanza cha hatua za msaada wa kibinadamu, na mifumo ya afya na vituo viendelee kulindwa, kufanya kazi, kuwa salama, huduma za matibabu kupatikana kwa wote wanaohitaji, na wafanyakazi wa afya walindwe ili waendelee kuokoa maisha.”
Wamesema vifaa vya kuokoa maisha vya ikiwemo mitungi ya oksijeni, ambavyo ni muhimu kwa wagonjwa walio na hali mahtuti, pamoja na wale walio na Uviko-19 ambao idadi yao ni 1,700 hospitalini hivi sasa vipatikane kwa wakati licha ya vita kuendelea.
Madaktarim wakimuwekea hewa ya oksijeni mgonjwa wa Uviko-19 katika hospitali ya Kramatorsk Ukraine. Picha| UNICEF/Evgeniy Maloletka.
Oksijeni pia ni muhimu kwa magonjwa mengine hatari kuanzia watoto wachanga hadi wazee yanayotokana na matatizo ya ujauzito, kujifungua, magonjwa ya muda mrefu, majeraha na kiwewe.
“Hali ya uhaba wa usambazaji wa oksijeni inakaribia kiwango cha hatari sana nchini Ukraine. Malori hayawezi kusafirisha usambazaji wa oksijeni kutoka kwenye kituo cha uzalishaji hadi hospitali kote nchini, pamoja na mji mkuu wa Kyiv.
“Hospitali nyingi zinaweza kumaliza akiba yao ya oksijeni ndani ya saa 24 zijazo. Baadhi tayari zimeisha. Hii inaweka maelfu ya maisha ya watu hatarini,” wamesema madaktari hao.
Zaidi ya hayo, wamesema watengenezaji wa jenereta za oksijeni za kimatibabu katika maeneo kadhaa pia wanakabiliwa na uhaba wa kemikali ya “zeolite”, bidhaa muhimu, hasa inayoagizwa kutoka nje ya nchi ili kutoa oksijeni salama ya matibabu.
Hali hii kwa mujibu wa WHO inazidisha hatari kwa wagonjwa, huduma muhimu za hospitali, lakini zihatarishwa na uhaba wa umeme na magari ya kubeba wagonjwa ambazo ziko katika hatari ya kukumbwa katika mzozo huo.
Katika miaka ya hivi karibuni, kwa msaada wa WHO, Ukraine ilikuwa imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo yake ya afya chini ya mpango kabambe wa mageuzi ya afya.
Soma zaidi:
-
Mjue askari aliyekataa kubeba silaha vitani na kuokoa watu 75 kwenye pambano kali
-
ICC yaelekeza macho yake Ukraine, Urusi ikiendelea na mashambulizi
-
UN yakwaa kisiki kuiwajibisha Urusi uvamizi Ukraine
Hii ni pamoja na uongezaji wa haraka wa uwezo wa tiba ya oksijeni kwa wagonjwa mahututi wakati wa janga la Uviko-19.
Kati ya vituo vya afya zaidi ya 600 kote nchini vilivyotathiminiwa na WHO wakati wa janga hilo, karibu nusu vilisaidiwa moja kwa moja kwa vifaa, ujuzi wa kiufundi na uwekezaji wa miundombinu, kuwezesha mamlaka ya afya kuokoa mamia ya maelfu ya maisha ya watu.
Maendeleo haya sasa yako katika hatari ya kusambaratishwa kutokana na mzozo wa sasa.
Licha ya changamoto zinazoletwa na hali ya sasa, WHO imesema inajitahidi kuhakikisha usambazaji wa vifaa vya matibabu vinavyohusiana na hewa ya oksijeni na vifaa vya matibabu ya majeraha.
Ili kufanikisha hili, WHO inaangalia kikamilifu suluhu za kuongeza vifaa ambavyo vinaweza kujumuisha uagizaji wa mitungi ya hewa ya oksijeni kutoka kwenye mitandao ya kikanda.