UN yakwaa kisiki kuiwajibisha Urusi uvamizi Ukraine
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana jana kwa dharura New York Marekani. Picha| UN.
- Urusi yatumia kura ya turufu kupinga maazimio ya Urusi.
Dar es Salaam. Jitihada za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwajibisha Urusi iliyoivamia Ukraine kwa kuzingatia kanuni na sheria za kimataifa zimegonga mwamba baada ya Urusi kuamua kwa mara nyingine kutumia tena kura yake ya turufu kupinga azimio lolote dhidi yake.
Baraza hilo limekutana kwa dharura kujadili hali inayoendelea nchini Ukraine na moja ya ajenda ilikuwa kuchukua hatua za kuiwajibisha Urusi kwa uvamizi wake.
Hata hivyo, kama ilivyotarajiwa wajumbe wote 15 wa Baraza la Usalama walialikwa na Rais wa Baraza hilo ambaye ni mwakilishi wa kudumu wa Urusi kupiga kura ya kupitisha au kupinga azimio hilo.
Matokeo ni kuwa wajumbe 11 wamepiga kura ya ndiyo kwa azimio hilo, wajumbe 3 wamejizuia kupiga kura na mjumbe mmoja ambaye ni Urusi akatumia haki yake ya kura ya turufu kupiga kura ya hapana na kulipinga azimio hilo.
Kwa kuwa Urusi ni mjumbe wa kudumu wa Baraza hilo kwa kutumia kura yake ya veto azimio hilo limeshindwa.
Kabla ya kupigwa kura Februari 25, 2022 baraza hilo liliwasilisha muswada unaoyakumbusha mataifa yote wajibu wao wa kujizuia na matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya mataifa mengine kwa kuzingatia katiba ya Umoja wa Mataifa na kuhakikisha migogoro yote ya kimataifa inatatuliwa kwa njia ya amani.
Mswada wa azimio hilo mbali ya kukumbusha wajibu muhimu wa nchi chini ya katiba ya Umoja wa Mataifa wa kudumisha amani na usalama wa kimataifa na maazimio mbalimbali ya kimatifa na Umoja wa Mataifa , “Unalaani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.”
Soma zaidi:
-
Mjue askari aliyekataa kubeba silaha vitani na kuokoa watu 75 kwenye pambano kali
-
ICC yaelekeza macho yake Ukraine, Urusi ikiendelea na mashambulizi
Azimio hilo pia ambalo lengo lake kuu ni kukomesha vita, limeelezea hofu kufuatia ripoti za mauaji ya rai na majeruhi.
“Limeamua kwamba hali ya Ukraine ni uvunjifu wa amani na usalama wa kimataifa, na kwamba shirikisho la Urusi limefanya vitendo vya uchokozi dhidi ya Ukraine, chini ya sura ya VII ya mkataba wa Umoja wa Mataifa,” inaeleza sehemu ya azimio hilo.
Azimio hilo linasizitiza haki ya uhuru, umoja, na uadilifu wa eneo la Ukraine ndani ya mipaka yake inayotambulika kimataifa.
Kwa mantiki hiyo limeitaka Urusi kuacha mara moja matumizi yake ya nguvu dhidi ya Ukraine na kujiepusha na tishio lolote lisilo halali au matumizi ya nguvu dhidi ya nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Pia limeitaka Urusi kuondoa mara moja na bila masharti vikosi vyake vya kijeshi kutoka eneo la Ukraine ndani ya mipaka yake inayotambulika kimataifa na bila masharti na kubadili uamuzi wa kuyashikilia majimbo ya Donetsk na Luhansk ambayo ni ya Ukraine.
Mwisho azimio hilo limetoa wito kwa pande zote kuruhusu na kuwezesha upatikanaji wa haraka, salama, na usiozuiliwa wa usaidizi wa kibinadamu kwa wale wanaohitaji nchini Ukraine.
Pia kulinda raia, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na watu walio katika mazingira magumu wakiwemo watoto, na kuheshimu haki zao.
Latest