ICC yaelekeza macho yake Ukraine, Urusi ikiendelea na mashambulizi

February 25, 2022 12:08 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) yasema inafuatilia kwa karibu mzozo wa Ukraine.
  • Imesema itachunguza kama kuna ukiukwaji wa haki za binadamu. 
  • Watu zaidi wa 100 Urusi kuivamia Ukraine.

Dar es Salaam. Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Karim Khan amesema mahakama hiyo inafuatilia kwa ukaribu kinachoendelea Ukraine baada ya uvamizi wa Urusi na itachunguza kama kutakuwa na  uwezekano wa uhalifu wa kivita nchini humo.

Kauli ya ICC inakuja ikiwa imepita siku moja tangu Urusi iivamie Ukraine kwa kile inachodai inapigania na kulinda maslai na uhuru wa wa majimbo mawili ya Donetsk na Luhansk.

Khan katika taarifa yake iliyoitoa leo Februari 25, 2022 amesema Ofisi yake itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya Ukraine ikiwa ni utekelezaji wa  majukumu yake kwa huru na bila upendeleo.

“Ofisi inaendelea kujizatiti kikamilifu katika kuzuia uhalifu wa kikatili na kuhakikisha kwamba mtu yeyote aliyehusika na uhalifu huo anawajibika,” amesema Khan akiwa nchini Bangladesh.

Amesema akirejea The Hague, Uholanzi, makao makuu ya ICC anakusudia kutoa taarifa ya kina zaidi kuhusu hali ya Ukraine, tathmini ya kina na hatua zinazofuata kuhusu mzozo huo.

“Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu matukio ya hivi majuzi ndani na karibu na Ukraine na wasiwasi unaoongezeka,” amesema Khan na kuongeza kuwa, 

“Nazikumbusha pande zote zinazoendesha uhasama katika eneo la Ukraine kwamba ofisi yangu inaweza kutumia mamlaka yake na kuchunguza kitendo chochote cha mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu au uhalifu wa kivita uliofanywa ndani ya Ukraine.”

Kwa mujibu wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky,  raia 137 na wanajeshi wameuawa nchini humo katika siku ya kwanza ya uvamizi wa Urusi wakati  vikosi vya nchi hiyo yenye nguvu duniani vikisonga mbele kuelekea mji mkuu, Kyiv.


Soma zaidi:


Urusi yaingia katika mzozo wa pili na Ukraine

Kufuatia Urusi kuchukua eneo la Crimea mnamo Machi 2014 na mapigano yaliyofuata mashariki mwa Ukraine kati ya waasi wanaoiunga mkono Urusi na vikosi vya serikali ya Ukraine, Ukraine ilikubali ICC kuchunguza vitendo vya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa katika eneo lake.

Mnamo Desemba 2020, ofisi ya mwendesha mashtaka ilitangaza kuwa ina sababu ya kuamini uhalifu wa kivita na uhalifu mwingine ulitendwa wakati wa mzozo wa mashariki mwa Ukraine.

Uchunguzi wa awali ulifungwa, lakini ombi rasmi kwa majaji kufungua uchunguzi kamili bado halijawasilishwa.  Urusi si mwanachama wa ICC na ilipinga kesi hiyo ya ICC.

Hata hivyo, mahakama inaweza kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliofanyika katika eneo la Ukraine bila kujali utaifa wa wahusika wanaodaiwa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW