Guterres: Madhara ya vita Ukraine yanavuka mipaka
- Madhara yazidi kuongezeka kwa wananchi.
- Nchi zinazotegemea bidhaa kutoka Ukraine na Urusi zaathirika na vita hiyo.
- Mazungumzo ya kidiplomasia yasisitizwa ili kumaliza vita hiyo.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema kuwa Ukraine inazidi kuteketea mbele ya macho ya dunia na madhara ya vita kwa wananchi ni makubwa.
Guterres amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani Machi 14, 2022 na kueleza kuwa hali inazidi kuwa mbaya na vita hiyo haitakuwa na mshindi bali kila mtu atakuwa ameshindwa.
“Watu wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto wanauawa. Baada ya kushambuliwa na majeshi ya Urusi, barabara, viwanja vya ndege na shule vimesalia magofu,” amesema Guterres.
Licha ya madhara ya vita hiyo ambayo imefikisha siku 21, Katibu Mkuu huyo ametahadharisha kuwa madhara ya vita hiyo yanavuka mipaka na waathirika wakuu ni nchi maskini pamoja na zile zinazotegemea bidhaa kutoka Ukraine na Urusi.
Nchi ya Ukraine peke yake inatoa zaidi ya nusu ya unga wa ngano unaosambazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WPF), hivyo vita hiyo inaweka hati hati ya uzalishaji na upatikanaji wa ngano hiyo.
“Tegemeo la chanzo cha chakula limepigwa bomu. Urusi na Ukraine zinachangia zaidi ya nusu ya mafuta ya alizeti na takribani asilimia 30 ya unga wa ngano unaotumika duniani kote,” amesema Guterres.
Guterres ameongeza kuwa nchi 45 za Afrika na nyingine zinazoendelea huagiza theluthi moja ya ngano kutoka Ukraine au Urusi, na 18 kati ya hizo zinaagiza takribani asilimia 50.
Nchi hizo ni pamoja na Burkina Faso, Misri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lebanon, Libya, Sudan na Yemen, hivyo amesihi kuchukua hatua zozote zinazowezekana kuepusha kimbunga cha njaa na kusambaratika kwa mfumo wa chakula duniani.
Soma zaidi:
-
ICC yaelekeza macho yake Ukraine, Urusi ikiendelea na mashambulizi
-
Simulizi ya mwanamke aliyejifungua katikati ya mashambulizi Ukraine
-
UNCHR, UNICEF zawalilia watoto wakimbizi kutoka Ukraine
Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa bei za chakula, mafuta na mbolea zinaongezeka kwa kasi kubwa, huku minyororo ya usambazaji wa bidhaa ikivurugwa na gharama za usafirishaji bidhaa kutoka nje zimefikia kiwango cha juu kuwahi kufikiwa.
Kutokana na hali hiyo, Guterres amesihi viongozi wa dunia kujizuia kupeleka fedha zaidi katika bajeti za silaha na badala yake zielekeze kwenye misaada rasmi ya maendeleo na hatua kwa tabianchi.
Licha ya kuwa Umoja wa Mataifa kupitia mfuko wake wa usaidizi wa dharura (CERF) kutoa Dola za Marekani milioni 40 (Sh92.5 bilioni) zaidi ili kusongesha misaada ya haraka kwa wahitaji, Guterres anasisitiza kutumia diplomasia ili kumaliza vita hiyo.
“Hatujachelewa kutumia diplomasia na mazungumzo. Tunahitaji amani kwa ajili ya wananchi wa Ukraine,” amesema Guterres.
Latest