Migodi ya Barrick inavyoimarisha afya za wananchi Mara
- Yatoa vifaa vya kupimia magonjwa kw hospitali mbili.
- Ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo kuisaida jamii.
Mara. Huenda wakazi wa Mkoa wa Mara wakapata uhakika wa afya zao, baada ya wawekezaji wa madini mkoani humo kuendelea kuboresha huduma za afya na vifaa tiba katika hospitali za umma.
Migodi ya Barrick ya Tanzania, ya North Mara na Bulyanhulu imetoa msaada wa vifaa vya kisasa vya utambuzi wa magonjwa zaidi ya manne, ukiwamo Uviko-19 kwa hospitali mbili za Mkoa wa Mara.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi ofisini kwake mjini Musoma, Meneja Mkuu wa North Mara, Apolinary Lyambiko amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wao wa kusaidia nchi, kupambana na kukabiliana na ugonjwa wa Uviko-19 pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza.
“Vifaa hivi vina uwezo wa kupima magonjwa ya kuambukiza kama virusi vya Uviko-19, kifua kikuu, nimonia, mafua makali na mengineyo,” amesema Lyambiko.
Vifaa hivyo vitaharakisha upimaji wa magonjwa hayo na kupunguza muda wa wagonjwa kukaa hospitali kusubiri matibabu.
Daktari Mkazi katika Mgodi wa North Mara, Dk Nicholas Mboya alibainisha thamani ya vifaa hivyo kuwa ni Sh115 milioni
Amesema kwa kutumia vifaa hivyo, utambuzi unaweza kufanywa kupitia aina tofauti za sampuli; kwa kuchukua vipimo kwenye pua, koo, mate au makohozi na kutoa majibu kati ya dakika 49 na 80.
“Aina hii ya upimaji ni moja ya mambo yanayothibitisha ubora wa vipimo hivi na usasa wake, vina uwezo wa kutambua majibu ya sampuli nne kwa wakati mmoja,” amesema Dk Mboya.
Mganga Mkuu wa Mko (RMO) wa Mara, Dk Juma Mfanga amesema vifaa hivyo ni vya kisasa ambapo kimoja kina uwezo wa kupima sampuli 50 kwa siku moja na hivyo mkoa umeongezewa uwezo wa kupima sampuli 100 kwa siku moja.
Soma zaidi:
Hospitali zitakazofaidika
Amesema kifaa kimoja kati ya hivyo kitatumiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, huku kingine ikielezwa kuwepo uwezekano wa kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, ambako muingiliano wa watu wakiwamo watalii ni mkubwa.
“Ikipelekwa Serengeti, itasaidia upimaji wa Uviko-19 hasa kwa watalii, ambao sampuli zao zilikuwa zikipelekwa nje ya mkoa, sasa zitapimwa hapo hapo wilayani Serengeti,” amesema Dk Mfanga.
Ugonjwa wa Uviko-19 umekuwa na tabia ya kubadilika badilika, hivyo vifaa hivyo vya kisasa vinatoa uhakika katika utekelezaji wa mipango ya kukabiliana nao na kupata mafanikio yanayotarajiwa.
Kwa upande wake RC Hapi ameishukuru na kupongeza ushirikiano ambao umekuwa ukitolewa na Barrick kwa Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo mkoani humo na nchi kwa ujumla.
Amesema Serikali ya Mkoa huo itaendelea kushirikiana na mgodi huo, ikiwa ni pamoja na kufanikisha maendeleo yake mathalan upanuzi wa uwekezaji huo ili Taifa liendelee kunufaika katika nyanja mbalimbali.
TANGAZO

Latest