Yanga, Simba wanavyoiweka Kigoma kwenye mtego wa Corona
- Mechi yao inachezwa katika mkoa ambao upo hatarini kutokana na mwingiliano wa watu kutoka mataifa jirani.
- Wakazi wa Kigoma/Ujiji bado hawajali tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya.
- Wataalamu wa afya wanahofu inaweza kuchochea kuongezeka kwa maambukizi.
Kigoma. Tofauti na maisha yao ya kila siku, wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Julai 25 mwaka huu watakuwa na moja ya matukio makubwa kuwahi kutokea katika mji wao litakalokutanisha maelfu ya watu.
Wakazi wa mji huo wa mkoa wa Kigoma uliopo magharibi mwa Tanzania watashuhudia timu mashuhuri za soka Tanzania za Simba na Yanga zikichuana vikali katika Uwanja wa Lake Tanganyika katika fainali za kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup).
Ni mara chache sana hutokea kwa timu hizi ambazo huvuta maelfu ya mashabiki kukutana nje ya Dar es Salaam.
Simba na Yanga watakutana Lake Tanganyika, wenye uwezo wa kubeba mashabiki 20,000, wakati taifa likiendelea kukabiliana na ongezeko kubwa la maambukizi ya wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya Corona (Uviko-19).
Ni mtego vita dhidi ya Uviko-19
Timu hizo zinakutana katika mji ambao wakazi wake bado hawaonekani kujali na kufuata miongozo ya afya ili kujikinga na maradhi hayo ambayo hadi Julai 21, yalikuwa yameshagharimu maisha ya watu 29 kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima.
Idadi ya wagonjwa wanaolazwa kwa Uviko-19 Tanzania imeongezeka mara nane ndani ya mwezi mmoja kutoka watu 100 mwishoni mwa Juni hadi watu 858 Julai 22, mwaka huu.

Uchunguzi uliofanywa na Nukta Habari kwenye mitaa mbalimbali ya karibu kata 10 za manispaa hii kuanzia Buzebazeba, Mwanga Kusini, Mwanga Kaskazini, Businde, Kasimbu, Kigoma, Kasingirima, Kagera, Kipampa hadi Katubuka unaonyesha wakazi wengi wanapuuza miongozo ya afya licha ya viongozi wa Serikali kuwahamasisha kuchukua tahadhari na kuwapatia elimu mtaani.
Sehemu kubwa ya wakazi wa hapa hawavai barakoa kwenye mikusanyiko na wala hawanawi mikono na maji tiririka na sabuni wanapoingia kwenye maeneo ya kupata huduma, kinyume na maagizo ya wataalamu wa afya.
Sehemu kubwa ya maeneo ya kutoa huduma ikiwemo maduka na magenge nayo hayajaweka nje maji na sabuni tofauti na ilivyokuwa mwaka 2020 mara baada ya Serikali kutangaza ujio wa maradhi hayo yanayozidi kusambaa kwa kasi nchini.
Maisha kama hakuna Corona vile
Ni maeneo machache sana ambayo wakazi hawa wanatii kufuata miongozo hiyo zikiwemo ofisi za umma, vituo vya kutoa huduma za afya na benki.
Katika soko maarufu la vyakula la Nazareti, Fatuma Khamis mkazi wa Kibirizi amekaa pembeni ya matunda anayouza akiwa hajavaa barakoa wala kuweka ndoo ya maji ya kunawa na sabuni.
Kundi kubwa la watu linapita mbele yake huku wengine wakiongea naye karibu kabisa bila barakoa.
“Hapa wengine wanafanya hizo taratibu na wengine hatufanyi, baadhi ya watu wanaamini kuna corona na wengine hawaamini ndiyo maana hawavai barakoa na hawana mpango wa kuamini kuwa corona ipo,” anasema Fatuma na kukiri kuwa elimu inatolewa mtaa kwa mtaa na Serikali kwamba wanawe mikono, wavae barakoa na wakiumwa waende hospitali..
Mwaka jana baada ya Serikali kutangaza uwepo wa ugonjwa huo Machi 16, Fatuma anasema katika soko hilo ilikuwa ni vigumu kuingia bila barakoa au kunawa maji tiririka na sabuni.
“Kwa sasa halina mkazo kwa sababu watu tumeshasahau kuhusu Corona na tulikuwa tumeshapotezea,” anasema.
Watoa huduma za usafiri ambao watakuwa wakikutana na watu wengi zaidi wakati huu wakiwasafirisha mashabiki wa Yanga na Simba nao hawajali, jambo linalowaweka hatarini kuambukizwa au kuambukiza abiria wao Uviko-19.
Abiria wakigombania usafiri katika stendi ya Masanga mkoani Kigoma. Abiria na watoa huduma hawazingatii miongozo ya kujikinga na Uviko-19 kama kuvaa barakoa au kuachiana nafasi wanapokuwa kwenye vyombo vya moto. Picha|Gift Mijoe.
Kati ya bajaji 10 na daladala tulizopata huduma na mpiga picha wangu hakuna hata moja iliyokuwa inasisitiza barakoa au watu kupeana angalau nafasi kupunguza uwezekano wa maambukizi. Wengi walitushangaa tulipokuwa tumevaa barakoa.
Dereva Bajaji wa eneo la Bulonge katika manispaa hiyo, Maulid Paulo mwaka jana alikuwa anavaa barakoa muda wote na kuziuza kwa abiria aliyekuwa akiingia bila kuvaa lakini baada ya kutangazwa kuwa hakuna Corona anasema hafanyi tena hayo.
Hata hivyo, matangazo ya mara kwa mara ya Serikali kuhusu maambukizi ya wimbi la tatu yameanza kumuogopesha.
“Hali inayoelekea siyo shwari kwa hapa ninahitaji niwe na ‘mask’ (barakoa) na nitakuwa nauza kama biashara ili watakaoingia bila ‘masks’ (barakoa) niwauzie. Nitaweka maji na ‘sanitiser’ (vitakasa mikono),” anasema.
Katika stendi ya mabasi ya Masanga ambayo huenda ikatumika zaidi kusafirisha abiria wa mechi hiyo, Serikali imeweka huduma za maji ya kunawa kabla ya kuingia getini lakini ni mmoja tu kati ya 10 ndiyo anayejali angalau kunawa mikono na sabuni.
Licha ya kuwa hatarini kupata Uviko-19 kutokana na kusafirisha abiria wengi tofauti kwa siku, sehemu kubwa ya madereva wa bajaji katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji hawafuati miongozo ya kujikinga. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Wataalamu wa afya waonya
Wataalamu wa afya wana wasiwasi kuwa mechi hiyo ya Simba na Yanga na mikusanyiko mikubwa mingine itaongeza zaidi maambukizi ya Uviko-19 katika mkoa huo unaopakana na mataifa jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.
Dk Syriacus Buguzi, daktari na mtaalamu wa mawasiliano katika sayansi kutoka kampuni ya ResearchCOM anasema mkusanyiko huo ulipaswa kuzuiwa kabisa ili kupunguza uwezekano wa kuongeza maambukizi.
Kwa sasa, anasema, mikakati ya kuzuia mikusanyiko “iko katika matamko ya jumla jumla ya Serikali kuhusu ‘mikusanyiko isiyo ya lazima’.
“Hapo ni ngumu kutambua ni mikusanyiko ipi siyo ya lazima,” anasema Dk Buguzi na kuongeza;
“Hatari ya hii ni kwamba maelfu watakusanyika na kuambukizana virusi vya Corona na baada ya hapo watarudi majumbani na kuwaambukiza wazee, na wenye magonjwa wa muda mrefu. Hiyo itaongeza ugumu katika afua dhidi ya Uviko-19.”
‘Wana nia gani?’
Julai 22, Serikali ilipiga marufuku mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na kwamba ile ya lazima ipate vibali maalum. Siku moja baadaye miongoni mwa masuala aliyoonekana Dk Gwajima kuhoji kuwa viongozi wengine wa chini hawatekelezi ipasavyo ni mikusanyiko kwenye matamasha na michezo.
“Tunapojazana na kusongamana kwenye viwanja kuangalia burudani mbalimbali kama mpira au jambo lolote bila kuchukua tahadhari; kwani haiwezekani wakabaki wachache ikawezekana kuwamudu kutekeleza tahadhari? Na huyo anayekaribisha tu watu wengi na kuwafanya wasongamane pasipo uwezekano wa kutekeleza afua za kinga kwa ufanisi, je anakuwa anayo nia gani?” alihoji Dk Gwajima.
Tuendelee kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona @taifastars_tff @taifastars_tff @samia_suluhu_update @msemajimkuuwaserikali @gersonmsigwa
pic.twitter.com/ZDnHHbdxn8— MSDtz (@MsdTanzania) July 21, 2021
Viongozi wa Serikali katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji wameiambia Nukta Habari kuwa wamekuwa wakijitahidi kila wazalo kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo katika mitaa yote 68 lakini bado wapo baadhi ya watu wanaopuuza.
Kigoma/Ujiji waendelea kupambana
Kaimu wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Fredinand Filimbi anasema manispaa hiyo ipo kwenye eneo hatarishi kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu wa ndani na nje ya nchi kutoka Burundi na DRC.
Ili kukabiliana na vihatarishi hivyo, anasema wamekuwa wakisisitiza watu kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono na maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita moja.
Baadhi ya bomba katika Soko la Buzebazeba katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji zikiwa bado hazijaanza kutoa huduma Julai 3, 2021. Picha|Gift Mijoe/Nukta.
Katika mahojiano yaliyofanyika mapema mwezi Julai, Filimbi anasema wamekuwa wakielimisha watu mtaa kwa mtaa ili kujikinga na Uviko-19 kwa kuwa baada ya maradhi hayo kutangazwa kupungua mwaka jana watu walijiachia lakini kwa sasa janga hilo limerudi kwa kasi.
Hadi Julai 3 Filimbi alisema hali haikuwa mbaya kwa kuwa hakukuwa na matukio mengi yaliyokuwa yameripotiwa zaidi ya wageni waliobainika mpakani kuwa na Uviko-19 ambao walipatiwa huduma stahiki.
Katika kumudu mechi ya Simba na Yanga, Thobias Andengenye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma aliwaambia wanahabari Julai 23 kuwa mashabiki wote watakoingia uwanjani watatakiwa kuvaa barakoa wakati wote wa mchezo na kunawa maji tiririka na sabuni yatakayowekwa nje ya uwanja wa Lake Tanganyika.
“Askari wamejipanga vya kutosha kwamba, ndiyo watu wengi wanakuja Kigoma lakini hatutegemei siyo kila anayekuja Kigoma ataenda kushuhudia mpira. Sisi tunatoa rai wale watakaokosa nafasi ya kuingia uwanjani watauona mpira kupitia kwenye televisheni,” anasema Andengenye.
Miongoni mwa mikoa yenye wagonjwa wengi
Mechi ya Simba na Yanga inachezwa katika mkoa ambao mwanzoni mwa Julai ulikuwa ni miongoni mwa mikoa yenye wagonjwa wengi wa maradhi hayo kwa mujibu Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akiwa ziarani mkoani humo.
“Nchi hii kati ya tarehe 5 na 9 (Julai) pekee yake tulikuwa na wagonjwa 471…kati ya mikoa 10 yenye wagonjwa wengi ni pamoja na mkoa wetu wa Kigoma kwa sababu pia ya mwingiliano na watu wa nchi jirani,” alisema Dk Mpango mapema Julai 17 akibainisha kuwa katika kipindi hicho mkoa huo ulikuwa na wagonjwa 18.
Je, mamlaka zitaweza kudhibiti idadi ya wafuasi kuingia katika uwanja huo ili kudhibiti maambukizi ya Corona? Ni suala la muda.
Makala haya ni sehemu ya mfululizo wa ripoti maalum kuhusu Uviko-19 kwa hisani ya Shirika la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).
Latest