Matarajio ya Watanzania bajeti kuu ya Serikali 2022-23
- Bajeti hiyo inatajiwa kuwasilishwa kesho Bungeni Dodoma.
- Serikali inatarajia kutumia Sh41 trilioni mwaka ujao.
- Watanzania waseme ije na suluhu ya kupanda kwa bei ya bidhaa, ukosefu wa ajira na uboreshaji wa huduma za jamii.
Dar es Salaam. Ikiwa zimesalia saa chache kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23, Watanzania wametoa maoni mbalimbali kuhusu bajeti hiyo huku baadhi wakitarajia kuona bajeti hiyo inakuja na sera ya kupunguza bei za bidhaa ili kuwapatia wananchi ahueni ya maisha.
Bajeti hiyo inasubiriwa kwa hamu na wengi kwa sababu itaweka bayana uwepo wa unafuu au ugumu wa maisha ya wananchi wa kawaida, wafanyakazi na biashara kwa mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai mosi.
Tofauti na miaka mingine, bajeti ya mwaka ujao wa fedha itakayowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba, imekuja wakati dunia ikishuhudia kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta kutokana na vita kati ya Urusi na Ukraine.
Pia ni katika kipindi ambacho nchi nyingi ikiwemo Tanzania zinaendelea kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zilizosababishwa na ugonjwa wa Uviko-19.
Makadirio ya awali ya bajeti hiyo ya 2022/23 ya yaliyowasilishwa mapema mwaka ujao na Dk Mwigulu Nchemba bungeni yalikuwa Sh41 trilioni kutoka Sh37.9 trilioni ya mwaka 2021/22.
Kati ya fedha hizo, Sh25.5 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo ni asilimia 62 ya bajeti yote.
Je, Watanzania wanatarajia nini kutoka kwenye bajeti hiyo itakayowasilishwa na Dk Nchemba Bungeni Dodoma kesho Juni 14?
Soma zaidi:
-
Deni la Serikali Tanzania laongezeka, lavuka Sh60 trilioni
-
Uchumi wazidi kuimarika Tanzania-BoT
-
Wizara tano zilizoidhinishiwa fedha nyingi 2022-23
Madereva wa vyombo vya moto
Ramadhan Said, dereva wa daladala linalofanya safari zake kati ya Makumbusho na Bunju anasema anatamani kuona bajeti hiyo ikija na mipango ya kupunguza bei ya mafuta ili waweze kupata faida na kuendesha maisha yao kwani kwa sasa hivi wanaonufaika zaidi ni wamiliki wa vyombo na siyo wao.
“Gharama za mafuta ndiyo zinachangia maisha kuwa magumu kama sasa hivi tunafanya tu kazi lakini hakuna faida, pamoja na mama kutupunguzia gharama kidogo lakini mafuta bado yako juu na faida hakuna…..shughuli zetu hizi hazina mshahara tunafanya tu kwa sababu kwa kukimbilia hatuna,” anasema Said.
Bei ya mafuta ya petroli na dizeli ilipungua kidogo mwezi Juni baada ya Serikali kutoa ruzuku ya Sh70 bilioni ili kuwapunguzia maumivu wamiliki wa vyombo vya moto.
Hata hivyo, madereva wanadai bado ziko juu ziendelee kushuka.
Dereva bodaboda katika eneo la Mwananyamala sokoni, Mohamed Mzee anatamani kuona bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23, tozo za mafuta zinapunguzwa ili bei za mafuta nazo zipungue.
“Kama mafuta yatapungua bei na sisi tutafaidika…kinachotuumiza ni tozo za mafuta inaonekana imekuwa ni changamoto,” anasema Mzee.
Wauzaji wa bidhaa za vyakula
Baadhi ya wananchi katika Jiji la Dar es Salaam wamesema kwa sasa bei za bidhaa hasa vyakula ziko juu na zinaendelea kupanda, jambo linalowaongezea gharama za maisha.
Ikiwa bajeti itakuja na majibu ya suala hilo, basi itawasaidia wananchi wa hali ya chini ambao wamekuwa wakijushughulisha na biashara ndogo ndogo.
Asha Rashid Kadewele, muuza vitafunio katika kituo cha daladala cha Makumbusho anasema hivi sasa biashara imekuwa ngumu kutokana na malighafi wanazotumia kupanda bei hali inayosababisha na wao kuuza bidhaa kwa bei ya juu ili kuendana na hali ya maisha na ombi lake kwa Serikali ni kupunguza bei ya bidhaa.
“Wakishatushushia bei ya bidhaa naona mambo yetu yatakuwa afadhali hali itakuwa kidogo siyo mbaya sana…. tunaomba gharama zishuke zaidi kwa sababu na sisi ndiyo tunapata kujikwamua,” anasema Kadewele.
Kupanda kwa bei ya bidhaa hasa nafaka ikiwemo ngano kumesababishwa na vita kati ya Urusi na Ukraine, jambo lililochangia kutatizika kwa mfumo wa usafirishaji wa bidhaa hiyo kutoka Ukraine, nchi inayosambaza kwa wingi ngano duniani.
Muuza duka la nafaka na mahitaji mengine ya nyumbani, Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Saimon Lazaro anasema kupanda kwa bei ya mafuta kumesababisha hata bei za bidhaa za kawaida zipande, hivyo kusababisha yeye kukosa wateja, hivyo ni ombi lake kuwa bajeti ya mwaka ujao igusie maeneo hayo.
“Kilio chetu ni vitu kupanda bei hatujui Serikali imefikia wapi, mafuta yako juu mzigo wangu umekwama Mbeya siku nne hapa sina biashara,” anasema Lazaro.
Jamila Kipingu, mfanyabiashara jijini hapa anasema biashara yake kwa sasa haiendi vizuri kama kipindi cha nyuma kwa sababu wateja wamemkimbia mara baada ya kupandisha bei ya bidhaa.
“Changamoto zipo kwa mfano ngano imepanda bei, mafuta yamepanda bei….Serikali ipunguze makali ya upandaji wa bei ili na sisi biashara zetu ziwe kwa wepesi,” anasema Kipingu.
Tangazo:

“Vijana wakumbukwe”
Linah Asecheck, mkazi wa Mbagala jijini hapa anaiomba Serikali katika bajeti hiyo iboreshe maslahi ya vijana kwa kutoa fursa mbalimbali za ajira ili wawezesha kupata kipato kuendesha maisha yao.
“Mimi ningeiomba Serikali yetu ya Tanzania itutetee sisi vijana, itupe fursa mbalimbali ambazo tunaweza kufanya kwa urahisi na tukakidhi mahitaji yetu. Hiyo itasaidia kupunguza watoto wa mtaani na matendo maovu,” anasema Asecheck.
Naye John Nkomo kutoka mkoani Mbeya anasema vijana ni nguvukazi muhimu ya Taifa, hivyo bajeti isiwaache nyuma bali ije na mikakati ya kutanua wigo wa ajira hasa katika sekta za kilimo na viwanda ili wasaidie katika kukuza uchumi wa nchi.
Iwe bajeti ya kuboresha huduma za jamii
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mwanza wanasema huduma za kijamii ikiwemo shule, vituo vya afya na maji zimulikwe kwenye bajeti hiyo kwa sababu bado maeneo mengi hayapati huduma hizo kwa uhakika.
“Furaha yetu ni kuona huduma za kijamii zinakuwepo katika maeneo yetu. Hatuwezi kufanya kazi kama hatuna maji wala afya bora, Serikali iliangalie hilo kwenye bajeti,” anasema Mwita Nyamhonga wa Ukerewe.
Habari hii imeandikwa na Lucy Samson na Esau Ng’umbi
Latest
