Chungu, tamu bajeti kuu ya Serikali 2022-23 kuanza leo

July 1, 2022 5:59 am · admin
Share
Tweet
Copy Link

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma, Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23. Picha | Wizara ya Fedha na Mipango.


  • Tozo ya mawigi na ving’amuzi kung’ata.
  • Serikali kubana matumizi, kutengeneza ajira na kuwezesha kilimo.
  • Kupanua wigo wa elimu bila ada na kupandisha kima cha mshahara vyapongezwa.

Dar es Salaam. Utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 unaanza leo Julai mosi huku ikiwa imetoa ahueni na maumivu katika baadhi ya maeneo wakati ambao bei ya bidhaa mbalimbali zikiwa zimepanda bei.

Bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/2023 ya Sh41.48 trilioni ilipitishwa na wabunge Juni 24,2022 baada ya wabunge 356 kati ya 379 kupiga kura za ndio.

Kati ya fedha hizo, Sh26.48 trilioni sawa na asilimia 63.8 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bajeti hiyo bungeni Juni 14 alisema inalenga kutoa nafuu ya maisha kwa wananchi pamoja na kufufua uchumi baada ya kuathiriwa na Uviko-19 na madhara ya vita ya Urusi na Ukraine. 

Dk Nchemba alisema Uviko-19 na vita inayoendelea Ulaya Mashariki imeathiri mwenendo wa uchumi na sasa Serikali inaangazia namna ya kuwapatia Watanzania ahueni. 

“Nchi ya Urusi ni ya pili katika uzalishaji wa gesi asilia na bidhaa za mafuta ya petroli duniani. Kadhalika, nchi ya Ukraine ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta ya alizeti kwa wingi duniani. 

“Kufuatia madhara haya ya vita, ni dhahiri kuwa uchumi na gharama za maisha duniani hazitabaki zilivyokuwa awali,” Dk Nchemba alisema.

Bajeti hiyo inatilia mkazo sera za mapato, sera za matumizi, kujali ufanisi (Value for Money), mapambano ya vitendo vya rushwa na kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ili kutengeneza ajira kwa vijana. 


Chungu ya bajeti hiyo

Licha ya Serikali kubainisha kuwa bajeti hiyo itawaletea unafuu Watanzania, yapo baadhi ya mambo huenda yatawaletea maumivu katika maisha yao ya kila siku ikiwemo ongezeko la kodi na ushuru katika baadhi ya maeneo. 

Kuanzia leo, wafanyabiashara au watumiaji wanaoagiza nywele bandia (mawigi) kutoka nje ya nchi wanaanza kutozwa ushuru wa asilimia 35 kwenye bidhaa hiyo. 

Ushuru huo ambao umeongezeka kutoka asilimia 25 ya awali, umelalamikiwa na baadhi ya watu kuwa utaongeza gharama za maisha na huenda ukaua baadhi ya biashara huku wengine wakisema utavipa nguvu viwanda vya ndani.

Pia watumiaji wa ving’amuzi kuanzia leo wanaanza kutozwa tozo wakati wakitumia vifaa hivyo vinavyowawezesha kupata mawasiliano kwa njia ya televisheni.

Hata hivyo, Serikali imepunguza tozo ya ving’amuzi nchini kufikia Sh500 hadi Sh2000 kwa kadri ya matumizi ya mteja baada ya majadiliano na Kamati ya Bunge ya Bajeti.

Kabla ya majadiliano hayo tozo iliyopendekezwa ilikuwa Sh1,000 hadi Sh3,000.

Baadhi ya watumiaji wanasema bado itakuwa na maumivu kwao kwa sababu wanatozwa tozo kwenye miamala wanayoifanya kwenye simu zao.


Soma zaidi:


Ni ahueni

Licha ya baadhi ya maeneo ya bajeti hiyo kulalamikiwa na Watanzania, imetoa ahueni ikiwemo kuondolewa kwa ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita, kujenga vyuo 36 vya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) kila wilaya ili kuwapatia vijana wanaomaliza shule za msingi na sekondari kupata fursa ya kusoma.

Pia Serikali imefuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa Tanzania pamoja na imeridhia asilimia 50 ya ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi kwenda kutumika kama ruzuku kwenye pembejeo za zao hilo la biashara. 

Serikali imepunguza tozo ya miamala kutoka kiwango kisichozidi Sh7,000 hadi kiwango kisichozidi Sh4,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa kwenye simu za mkononi.

“Punguzo hili ni sawa na asilimia 43 ya kiwango cha sasa,” alisema Dk Nchemba.

Kwa mujibu wa Dk Nchemba, katika bajeti hiyo, Serikali inakusudia kuendelea kukamilisha miradi ya vielelezo na ile ya kimkakati inayotarajiwa kuwa na matokeo mapana na ya haraka katika uchumi wa Tanzania ukiwemo mradi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi mkubwa wa bwawa la umeme la Nyerere katika mto Rufiji.  

“Miradi hii inatarajiwa kuchochea uzalishaji ajira, kukuza kipato na kuchangia zaidi kupunguza hali ya umaskini nchini. Katika kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na huduma, miradi itajielekeza katika kukuza sekta ya kilimo kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ya umwagiliaji,” alisema Waziri Nchemba wakati akiwasilisha mpango wa bajeti kwa mwaka 2022/23. 

Pia Serikali itaongeza ajira kwa vijana ambapo Serikali imeongeza bajeti ya Kilimo kutoka Sh294 billioni hadi Sh954 bilioni na itaendelea kuongezeka kila mwaka ili kuwavutia wengi kuingia katika sekta hiyo.

Umejipangaje kutekeleza bajeti ya mwaka huu wa fedha ambao umeanza leo?

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...