Ukweli huu hapa viongozi kupanda mabasi mazishi ya Malkia Elizabeth II

September 20, 2022 11:01 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Uingereza ilifanya hivyo kuimarisha usalama na kupunguza msongamano wa magari.
  • Si ubaguzi wala ukoloni kama ilivyotafsiriwa.
  • Wachambuzi wa masuala ya intelejensia wasema Uingereza ilikuwa sahihi.

Dar es salaam. Hayati Malkia Elizabeth II amezikwa rasmi katika jumba la Westminster Abbey nchini Uingereza mara baada ya kufariki Septemba 8 mwaka huu huku mazishi yake yakihudhuriwa na maelfu ya watu kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Miongoni mwa waliohudhuria ni wakuu wa mataifa zaidi ya 500 akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye pamoja na wengine walipata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Malkia Elizabeth II kabla haujaenda kuzikwa.

Ushiriki wa viongozi hawa katika mazishi ya malkia umeibua mijadala na kuwa gumzo katika mitandao ya kijamii kutokana na utaratibu uliowekwa wa kuwasafirisha baadhi ya  wakuu wa nchi katika mabasi ya kifalme huku wengine wakitumia usafiri binafsi.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekwenda mbali zaidi na kutoa taarifa potofu kwa kuhusianisha kitendo hicho na ubaguzi na wengine kufananisha kitendo hicho na ukoloni.

Ipo hivi

Ni kwa mara ya kwanza ulimwengu unapata kushuhudia mazishi ya kiongozi mkubwa kabisa ulimwenguni hivyo kutokana na ukubwa wake ilitarajiwa mazishi hayo yangehudhuriwa na watu wengi kutoka mataifa ambayo yanahusiana kidiplomasia au kiuchumi na taifa la Uingereza.

Kwa kutambua hilo Serikali ya Uingereza, Septemba 11 mwaka huu  ilitoa mwongozo unaobainisha kuwa wakuu wote wa nchi watasafirishwa na mabasi kuelekea kwenye ibada ya mazishi ili kuepusha msongamano wa magari pamoja na sababu za usalama.

Taarifa hiyo iliyochapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Politico la nchini Marekani ilifafanua kwamba wageni wote wanaotarajia kuhudhuria mazishi hayo watumie ndege za abiria badala ya ndege binafsi. 

“Kutokana na idadi ya ndege zinazofanya kazi hivi sasa hatutaruhusu ndege binafsi, tunasikitika kwamba kutokana na ufinyu wa nafasi katika ibada ya mazishi hakuna washiriki wengine wa mgeni mkuu, wasaidizi au wafanyakazi watakaopokelewa,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Mazishi hayo ya kihistoria yamefuatiliwa na mabilioni ya watu kutoka pembe tofauti za ulimwengu ambapo takribani wakuu wa nchi 500 walihudhuria wakiwemo marais, mawaziri wakuu pamoja na familia za kifalme.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) tukio hilo lilihudhuriwa na watu zaidi ya 2,000.

Kwa muktadha huo kama kila kiongozi angeruhusiwa kuwa na usafiri wake binafsi ni wazi kungekuwa na msongamano ambao huenda ungekwamisha na kuchelewesha shughuli za mazishi au kuhatarisha usalama.

‘The Beast’ gari ya Rais wa Marekani Joe Biden yenye mifumo imara ya ulinzi ambayo aliitumia kwenye msafara wa ibada ya mazishi ya Malkia Elizabeth II. Picha| AFP.

Kwanini Joe Biden?

Miongoni mwa viongozi wa nchi waliotumia magari  binafsi ni pamoja na Rais wa Marekani Joe Biden ambaye alitumia gari maalumu yenye mfumo wa ulinzi iitwayo ‘the beast’ , jambo lililowaibua watu kuhoji kwa nini Rais wa Marekani pekee apewe upendeleo huo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza Litz Truss aliyekuwa akizungumza na wanahabari Septemba 13 mwaka huu alisema “kilichotolewa ni mwongozo na si sheria” hivyo unaweza kubadilika kulingana na maombi ya nchi husika.

Serikali ya Marekani iliiarifu Uingereza kuwa Biden hatotumia usafiri wa basi kutokana na sheria za ulinzi kwa viongozi wake ambazo taifa hilo kubwa zimejiwekea ikiwemo ya Rais wake kutumia usafiri binafsi anapokuwa katika ziara rasmi.


Soma zaidi:


Kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya intelejensia na ujasusi, Habibu Anga katika chapisho lake kwenye ukurasa wa Instagram, wajibu wa ulinzi kwa kiongozi wa nchi anapokuwa ugenini ni wa nchi husika na Uingereza walikuwa sahihi.

“Kama kila kiongozi angekuwa na msafara wake ina maana rasilimali za ulinzi zingegawanywa kwa watu zaidi ya 100 usalama wa viongozi ungekuwa hatarini zaidi,” inasomeka sehemu ya chapisho hilo.

Anga ameongeza kuwa matishio ya kiusalama kwa viongozi wa mataifa yanatofautiana kutokana na ukubwa wa taifa husika kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia. Ndiyo maana ilikuwa rahisi Uingereza kumruhusu Biden kuwa na gari binafsi.

Viongozi wengine ambao hawakutumia usafiri wa basi ni pamoja na wafalme wa Uholanzi, Hispania, Ubelgiji na Sweden. 

Marais wa Ujerumani, Israel, Waziri Mkuu wa Japan na Makamu wa Rais wa China  walitumia magari yaliyoandaliwa na Serikali ya Uingereza au ya balozi zao.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV