Uzushi: Rais wa Zimbabwe hajazuiwa kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II

September 17, 2022 10:38 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ubalozi wa Uingereza nchini Zimbabwe umethibitisha Rais Emerson Mnangagwa atashiriki mazishi hayo.
  • Nchi ya Zimbabwe hawajatoa taarifa rasmi kuthibitisha uzushi huo.

Dar es Salaam. Rais wa Zimbabwe Emerson Mnangagwa atahudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II yanayotarajia kufanyika jumatatu ya wiki ijayo, tofauti na uzushi unaoenezwa mtandaoni kuwa amekataliwa kwa sababu ya vikwazo vya kusafiri alivyowekewa na Uingereza.

Malkia Elizabeth II aliyefariki Septemba 8 anatarajiwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele Septemba 19 mwaka huu huko Westminster Abbey, Scotland. 

Kifo cha Malkia Elizabeth II aliyetawala Uingereza kwa miaka 70 kimeibua taarifa nyingi za uzushi ikiwemo ya Rais Mnangagwa kuzuiliwa kushiriki mazishi yake. 

Moja ya taarifa hizo za uzushi ni ile iliyo kwenye mfumo wa picha ikionyesha ujumbe wenye muhuri wa kasri la Backingham kutoka kwa naibu afisa mawasiliano wa kasri hilo ikimuendea Waziri wa Mambo ya Nje nchini Zimbabwe Federick Shava aliyeandika barua kuomba Rais Mnangagwa kuwa sehemu ya wahudhuriaji wa mazishi ya Malkia Elizabeth II.

Ukweli ni upi?

Baada ya kusambaa kwa uzushi huo ambao baadhi ya vyombo vya habari vya mtandaoni ulitumia kuhabarisha, Ubalozi wa Uingereza nchini Zimbabwe uliotoa taarifa kukanusha madai hayo na kueleza kuwa Rais Mnangagwa hajazuiliwa kushiriki mazishi hayo.

Ubalozi wa Uingereza nchini Zimbabwe kupitia ukurasa wa Twiter umesema barua hiyo si ya kweli na Rais Mnangangwa atahudhuria mazishi ya Malkia siku ya jumatatu.


Pia timu ya Nukta Fakti imetumia zana za kidijitali ikiwemo ya Google Image na haijafanikiwa kupata taarifa ya Kasri la Backingham ya kumzuia Rais wa Zimbabwe kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II.

Kwa mujibu wa Uingereza, viongozi wa dunia zaidi ya 500 wakiwemo marais watahudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II katika eneo la Westminster Abbey lenye uwezo wa kuchukua watu 2,200.

Baadhi ya nchi ambazo wawakilishi wake hawataruhusiwa katika mazishi hayo ni pamoja na Urusi, Belarus na Myanmar kwa sababu mbalimbali ikiwemo vikwazo vya usafiri ambavyo viongozi wake wamewekewa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW