Mbolea ya ruzuku: Wakulima wadai haijawafikia, Serikali yawatoa hofu

October 20, 2022 10:32 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kupita zaidi ya miezi miwili tangu waandikishwe lakini bado hajapata mbolea.
  • Wakulima wa Misungwi mkoani Mwanza wahofia kukosa mazao endapo mbolea haitawafikia. 
  • Serikali yasema inafanyia kazi suala hilo na watapata kwa wakati.

Mwanza.  Ni zaidi ya miezi miwili sasa tangu wakulima katika Kata ya Usagara wilayani Misungwi kujiandikisha kwa ajili ya kupata ruzuku ya mbolea hawajapata licha ya kuelezwa kuwa zingefika kwa wakati.

Wasiwasi wao ni kuwa msimu wa kilimo umeanza na hawaoni matumaini kama watapata mbolea za kupandia iwapo mvua zitaanza kwa wakati.

Katika Sherehe za Wakulima za Nane Nane 2022, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alitangaza mpango kutoa ruzuku kwa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea ili kuwapunguzia mzigo wakulima katika shughuli za uzalishaji mazao.

Hatua hiyo ilikuwa ni mkakati wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia kulikochangiwa na ugonjwa wa Uviko-19 na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Kupitia mpango huo mbolea zote za kupandia zinazofahamika kama NPK zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh122, 695 zitauzwa kwa Sh70 000 huku ruzuku ya Serikali ikiwa Sh52,695.

“UREA (ya kukuzia) itatoka Sh124,734 wakulima wataenda kuinunua kwa Sh70,000,” alisema Bashe katika kilele za sherehe hizo akiwa mkoani Mbeya. 

Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo aliagiza mpango huo uanze Agosti 15 ili kuwawezesha wakulima kujianda vema na msimu wa kilimo wa mwaka huu.

Hata hivyo, baadhi ya wakulima mkoani Mwanza wamesema mpaka sasa hawajapata mbolea hiyo na wameanza kukata tamaa kwa sababu msimu wa kuanza kupanda mazao umekaribia.

Petro Pendo ni mkazi wa Mtaa wa Usagara, jijini hapa amesema imani ya kupata mbolea hiyo ya ruzuku kutoka serikalini imeanza kupotea hasa kutokana na ahadi walizopewa mara tu walipojiandikisha.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (aliyevaa kofia katikati) amefanya ziara ya pamoja na Rais wa Shirika la AGRA Agnes Kalibata katika mradi wa mashamba ya pamoja (Block Farm) ya Chinangali Mkoani Dodoma pamoja na Kituo cha Mafunzo ya Wakulima na Kuhimilisha Vijana BIHAWANA Oktoba 13, 2022. Picha | Wizara ya Kilimo.

Pendo anasema wakulima wote wanaotumia kilimo cha umwagiliaji na hata wale wanaotegemea mvua ya masika wote watalazimika kutoboa mifuko yao zaidi kununua mbolea kwa mawakala wa mbolea kwa kuwa ya ruzuku haitabiriki.

“Kifupi wakulima watalazimika kutumia pesa zaidi kwa kuwa tuliahidiwa kuwa tujiandikishe kwa ajili ya kupata mbolea yenye gharama nafuu, ni miezi mitatu sasa toka tujiandikishe lakini hakuna taarifa yoyote tuliyopata ya kwenda kufuata mbolea kama tulivyoelezwa baada ya kukamilisha taratibu za kujiandikisha,” amesema Pendo.

Pendo ambaye anamiliki shamba la ekari mbili la mahindi na tatu la mpunga amesema walielezwa mbolea hiyo wangeipata kwa thamani ya Sh70,000 kwa mfuko wa kilogramu 50 badala ya Sh150,000 kwa bei za mawakala wa pembejeo.

“Kinachotusononesha ni kuwa mbolea haijafika kwa wakati, hali itakayosababisha sasa wakulima kutumia mbolea nyingine aidha ya samadi au mboji ambayo pia nayo inatakiwa ivundikwe kwa muda mrefu walau miaka miwili ndiyo iweze kufanya kazi kwenye mazao,” amesema Pendo.

Akitolea mfano katika msimu uliopita, Pendo anasema katika ekari zake mbili za mahindi aliweza kuvuna gunia sita tu kwakuwa alikuwa amelima kilimo cha mazoea na kwamba angetumia mbolea angeweza kuvuna kati ya gunia 13 hadi 15.

Mkulima mwingine wa Usagara, Neema Magalaya mesema hadi wakati huu Serikali ingekuwa imeshasambaza mbolea kwa wakulima kwa ajili ya kupandia kwakuwa msimu wa kilimo tayari umekaribia kuanza.

“Kutokana na changamoto hiyo, wakulima tutalazimika kutumia mbolea ya ng’ombe au ya kuku tu kwa kuwa wakulima walio wengi hawawezi kumudu kununua mbolea iliyopo madukani ni ghali,” amesema Magalaya.

Anasema kilo moja ya mbolea kwa sasa inauzwa Sh4,000 na shamba la ekari moja linatakiwa angalau kilo 25 kwa ajili ya kupandia na kilo 25 kwa ajili ya kukuzia au mavuno.

“Unapotumia mbolea unakua na uhakika wa kupata mazao mengi hata kama umelima shamba dogo mavuno yanakuwa ya uhakika, lakini sasa bado hatujaelewa kama tutaendelea kulima kilimo cha kizamani au Serikali itatuletea mbolea,” amesema Neema na kueleza kushangazwa kwakuwa baadhi ya mikoa mbolea zimeshaanza kutolewa huku kwa Wilaya ya Misungwi hazijawafikia.


Zinazohusiana: 


Serikali yaingilia kati

Mwenyekiti wa Mtaa wa Identemya jijini hapa, Buzuka Kijika bila kutaja idadi ya wakulima waliojiandikisha kupata ruzuku ya mbolea amesema baadhi ya watu wamepokea ujumbe kuwa wameingizwa kwenye mfumo wa kupokea mbolea ingawa hawajajua ni wapi wanapotakiwa kwenda kuipokelea.

Kijaka ameiomba Serikali kuwahisha mbolea ili wakulima waweze kulima kwa wakati. 

“Ni vema Serikali ikawahisha mbolea ili wakulima wazipate kwa wakati kwakuwa hivi sasa msimu umekaribia kuanza ili wasikose mbolea ya kupandia,” amesema Kijika.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali imeanza kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ambapo wale watakaosajiliwa watapata namba ya siri itakayosaidia kwenda kununua mbolea kwa mawakala kwa bei elekezi.

“Namba hiyo ya siri ndiyo silaha yako, ukiitoa kwa mtu anaweza kununua mbolea kupitia namba yako ya siri na kukusababisha usipate ruzuku,” amesema Bashe wakati akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).

Bashe amekiri kuwepo kwa changamoto ya mawakala wa kusambaza mbolea ya ruzuku kwenye maeneo yao na kwamba Serikali inalifanyia kazi suala hilo kuhakikisha inaongeza idadi ya mawakala kwenye maeneo ambayo yana upungufu ili wakulima waweze kununua mbolea jirani na maeneo yao.

Amesema Serikali itachukua hatua kwa wote watakaokuwa wanaiba mbolea ya ruzuku kwa kutumia namba za siri za wakulima.


Tangazo:


Atoa maagizo

Waziri Bashe amewaagiza viongozi wa ushirika kupeleka maombi Wizara ya Kilimo ili wapate fursa za kuuza hizo mbolea kwenye maeneo yao kwa kuwa ndiyo wanakuwa karibu na wakulima.

Katika hatua nyingine amewataka wakulima kutumia mvua zitakazoanza kunyesha kupanda mazao ili kukabiliana na hali ya hewa iliyopo kwa sasa.

“Hivi sasa mikoa ya Kanda ya Ziwa mvua zimeanza japo sio nyingi ni vyema wakazitumia zilizopo kwa kupandia ili kusaidia kuwa na mazao mengi ya chakula nchini,” amesema Bashe.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW