Majaliwa acharuka wanaodaiwa kutorosha mbolea ya ruzuku nje ya nchi

January 16, 2023 1:51 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Januari 16, 2023 wakati akisalimia na wananchi kwenye eneo la Mbalizi jijini Mbeya akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali. Amesema utoaji wa ruzuku hiyo ya mbolea unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na ni marufuku kuiuza nje. Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu. 


  • Asema mbolea hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya ndani tu.
  • Ataka hatua kali zichukuliwe kwa watakaobainika.
  • Mbolea hiyo inalenga kuongeza uzalishaji na kuwapunguzia wakulima makali ya bei. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuwa walinzi wa mbolea ya ruzuku iliyotolewa na Serikali ili kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuongeza uzalishaji wa mazao katika msimu wa 2022/23.

Majaliwa ametoa kauli hiyo baada ya kumekuwa madai kuwa wapo Watanzania wachache wanaotorosha mbolea kwenda nchi jirani kinyume na maelekezo ya Serikali. 

”Jambo hili lazima tulikemee na tulisimamie sote ili kuhakikisha mbolea iliyopo nchini ni kwa ajili ya Watanzania, kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake,” amesema Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Januari 16, 2023 wakati akisalimia na wananchi wa Mbalizi jijini Mbeya.

Katika Sherehe za Wakulima za Nane Nane mwaka 2022, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alitangaza mpango kutoa ruzuku kwa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea ili kuwapunguzia mzigo wakulima katika shughuli za uzalishaji mazao.

Hatua hiyo ilikuwa ni mkakati wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia kulikochangiwa na ugonjwa wa Uviko-19 na vita kati ya Urusi na Ukraine.


Zinazohusiana: 


Kupitia mpango huo mbolea zote za kupandia zinazofahamika kama NPK zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh122, 695, alisema zingeuzwa kwa Sh70 000 huku ruzuku ya Serikali ikiwa Sh52,695.

“UREA (ya kukuzia) itatoka Sh124,734 wakulima wataenda kuinunua kwa Sh70,000,” alisema Bashe katika kilele za sherehe hizo akiwa mkoani Mbeya. 

Majaliwa amesema utoaji wa ruzuku hiyo ya mbolea unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na ni marufuku kuiuza nje.

Ameongeza kuwa awali mbolea iliuzwa kwa zaidi ya shilingi 100,000 lakini Rais Dk Samia Suluhu Hassan aliridhia kutoa ruzuku Sh150 bilioni ili ikashushe bei ya mbolea na sasa inauzwa kwa shilingi 70,000. 

”Tusikubali fedha hiyo kutumika nje la malengo, tulinde mbolea yetu isiuzwe kwa wasiohusika.”

”Nimefurahi sana kwa hatua zilizochukuliwa mkoani Songwe, tani 2,199 zimekamatwa zikipelekwa nchi jirani hii haikubaliki, watanzania tuwe walinzi hii ni pesa yetu inatoroshwa na wachache, malengo yetu ni kuwahudumia ninyi kwa usimamizi wa Rais Dk Samia,” amesisitiza Waziri Mkuu. 

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...