Wakulima walalamika kucheleweshewa mbolea ya ruzuku
- Wasema wameanza kupokea wakati mazao yameota tayari.
- Washauri Serikali kutimiza ahadi kwa wakati.
Mwanza. Licha ya wakulima mkoani Mwanza kuanza kupokea mbolea ya ruzuku, wamesema mbole hiyo imechelewa kufika, jambo ambalo limeathiri kwa sehemu shughuli zao za kilimo.
Katika Sherehe za Wakulima za Nane Nane mwaka 2022, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alitangaza mpango kutoa ruzuku kwa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea ili kuwapunguzia mzigo wakulima katika shughuli za uzalishaji mazao.
Hatua hiyo ilikuwa ni mkakati wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia kulikochangiwa na ugonjwa wa Uviko-19 na vita kati ya Urusi na Ukraine.
Baadhi ya wakulima wameiomba Serikali kuhakikisha inapotoa ruzuku ya mbolea kuiwasilisha kwa wakati kwa kuwa mazao mengi huanza kulimwa mapema.
Wakizungumza na Nukta Habari (www.Nukta.co.tz) leo Februari 9, 2023 wakulima hao wamesema tangu walivyojiandikisha Septemba mwaka jana ndiyo wameanza kupokea mbolea hiyo mwishoni mwa Januari 2023 ambapo tayari mazao mengi kama mahindi na maharage yameanza kukomaa.
Kawaida ya mbolea huwekwa mashambani mara mbili. Wakati unapanda mazao na pale unapopalilia kwa ajili ya kukuzia lakini waliyopata wakulima hao haitafaa kwa baadhi ya mazao kama mahindi labda kwa mpunga na pamba.
“Mfano tulijiandikisha toka mwezi Septemba mwaka jana tukiamini mpaka kufikia mwezi Oktoba tutakuwa tumepata mbolea lakini hadi msimu wa kilimo unaanza tulikuwa hatuna mbolea na tulianza kutumia za mboji au mwenye hela alienda kununua kwa wauzaji wa pembejeo,” amesema Petro Maganga, mkazi wa Sanjo wilayani Misungwi.
Amesema mbolea hiyo ya ruzuku inauzwa Sh70,000 kwa mfuko wa kilo 50 wakati kwa mawakala wanauza mbolea hiyo kwa Sh100,000.
Soma zaidi:
Mbolea ya ruzuku: Wakulima wadai haijawafikia, Serikali yawatoa hofu
Mkulima Mwingine Felister Boniphace amesema huenda wasipate mazao mengi mwaka huu kwa sababu wamechelewa kupata mboleo hiyo.
Amesema Serikali ingekuwa inatekeleza ahadi zake kwa wakati ingesaidia wakulima kuondokana na kilimo cha mazoea na kuhamia kilimo cha kisasa na chenye tija.
“Tunaiomba Serikali pale inapoahidi kuwapatia wakulima msaada basi wasichukue muda mrefu hasa sisi huku Kanda ya Ziwa mazao mengi yanawahi kulimwa kutokana na misimu ya mvua kubadilika, hivyo wanapotoa mbolea kwa wakati wanawasaidia wakulima kwenda na msimu,” amesema Felister.
Wamesema uzuri wa mbolea ije wakati wa kupanda ili mazao yanapoota na kupaliliwa waweke nyingine ya kukuzia.
“Kwa sasa labda tuinunue kwa ajili ya mwakani lakini si kwa wakati huu ambapo tayari mazao tumeshapanda na mengine yapo tayari kuvunwa, mfano mahindi na mharage tayari tumeshaanza kuvuna,” amesema Felister.
Pamoja na maombi hayo pia wakulima wamelalamikia kitendo cha baadhi ya mawakala wa mbolea kuwatumia kupata mbolea ya ruzuku inayotolewa na Serikali kwa gharama nafuu.
Wamesema wapo baadhi ya wakulima wametumiwa na mawakala wanaouza pembejeo za kilimo kununua mbolea hiyo kisha kuwauzia wao kwa gharama za kawaida.
Maganga amesema pamoja na masharti ya kununulia mbolea hiyo kuwekwa lakini baadhi ya wakulima wanayakiuka.
Amesema kitendo hicho kinawafanya mawakala wapate faida kwa kuwa wao huuza mfuko mmoja wa kilo 50 kwa Sh100, 000 hivyo kuwa na faidi ya Sh15,000 kwa kuwa kwa mkulima humnunulia mfuko mmoja kwa Sh85,000.
Afisa Kilimo mkoani Mwanza, Makenzi Keya akizungumzia kuchelewa kwa mbolea amesema ni taratibu tu za kiserikali ingawa kwa sasa mbolea ipo na ya mazao tofauti.
Tayari mbolea ya ruzuku imeshawisili mkoani humo na inasambazwa kwa wakulima.
“Baada ya kujiandikisha atasubiri ndani ya siku moja au mbili atapatiwa ujumbe ambao utamtaka kwenda kufuata mbolea yake ambapo akifika ataonyesha ujumbe huo na kulipia gharama ya kiasi cha mbolea anachotaka,” amesema Keya
Keya amesema taratibu za uchukuaji wa mbolea hiyo ni mkulima awe na kitambulisho cha Taifa, au mpiga kura, leseni ya udereva kisha ataenda kujiandikisha ofisi ya kata akianisha eneo la shamba lilipo na idadi ya ekari atakazolima kwa msimu huo.
Alipoulizwa suala la mawakala kutumia wakulima kujipatia mbolea ya Serikali amesema hilo ni ngumu kutokea kwa kuwa moja ya kigezo cha kupata mbolea ni kuanishia shamba lilipo kisha Bwana Shamba ataenda kulitembelea kabla ya kukabidhiwa mbolea hiyo.
Latest
