Wakulima wa ngano wanavyopishana na mabilioni Tanzania
- Uzalishaji wao ni mdogo ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo.
- Tanzania inaagiza takriban tani 863,000 za ngano nje ya nchi huku uzalishaji wa ndani ukiwa chini ya tani 100,000.
- Wizara ya Kilimo yasema inakusudia kushirikiana na sekta binafsi kuongeza uzalishaji wa zao hilo Tanzania.
Dar es Salaam. Wakulima wanaolima ngano Tanzania wanapishana na fursa ya mabilioni baada ya Serikali kueleza kuwa kiwango wanachozalisha nchini kimeshindwa kukidhi mahitaji ya ndani ya soko na kusababisha sehemu kubwa ya shehena ya chakula hicho iagizwe kutoka nje ya nchi.
Serikali imeeleza leo kuwa zaidi ya nusu ya chakula chote kilichoagizwa nje ya nchi kwa miaka sita iliyopita kilikuwa ni ngano ili kukidhi mahitaji ya ndani ya uzalishaji hasa viwandani.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amesema leo (Februari 27, 2020) katika Mkutano wa mwaka wa kilimo biashara 2020 jijini Dar es Salaam kuwa kati ya mwaka 2014 na 2019 chakula kilichoagizwa nje ya nchi kilikuwa na thamani ya takriban Sh7.74 trilioni.
“Lakini ukigawanya hizo takwimu ni chakula gani tunaingiza kwa wingi katika kipindi cha miaka sita? Ngano ni asilimia 53.3,” amesema Bashungwa katika mkutano huo uliwakutanisha wadau kuzungumzia mikakati ya kukifanya kilimo cha Tanzania kuwa cha kibiashara.
Amesema kwa wastani katika kipindi hicho cha miaka sita iliyopita, Tanzania imekuwa ikiagiza wastani wa chakula chenye thamani ya Sh1.3 trilioni kila mwaka.
Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaeleza kuwa kila mwaka Tanzania inaagiza takriban tani 863,000 za ngano nje ya nchi huku uzalishaji wa ndani ukiwa chini ya tani 100,000.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, mwaka juzi Tanzania ilizalisha ngano tani 57,000 ikilinganishwa na tani 50,000 za mwaka 2017.
Kutokana na uhaba wa ngano inayozalishwa Tanzania, wawekezaji mbalimbali wakiwemo wa viwanda vya bia wanalazimika kuagiza ngano nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotegemea malighafi ya zao hilo.
Bashungwa amesema ni wakati mwafaka kwa wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa ya kulima ngano kwa wingi ili kufaidika na soko la ndani na kupunguza uagizaji wa zao hilo nje ya nchi.
Mikoa yenye ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo cha ngano ni pamoja na Manyara, Mbeya, Arusha na Rukwa.
Zinazohusiana:
- Mkulazi kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha sukari Morogoro
- Wakulima wa miwa Morogoro kunufaika na fursa za mikopo, soko
- Rais Magufuli aagiza mashamba ya ngano Manyara yaanze kulimwa
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema sababu kubwa ya wakulima kushindwa kuzalishaji kiasi kikubwa cha ngano kukidhi mahitaji ni gharama kubwa za uzalishaji ambazo wakulima wadogo wanashindwa kuzimudu.
Hata hivyo, amesema mkakati wa wizara yake ni kushirikiana na sekta binafsi kuwezesha wakulima wadogo kulima zao hilo kwa nyenzo za kisasa na upatikanaji wa mitaji kutoka benki ya kilimo (TADB).
Amesema kwa kuanzia wataendesha mradi mkubwa kuwawezesha wakulima kulima ngano katika mashamba ya Kapunga yenye ukubwa wa ekari 3,000 hadi 4,000 yaliyopo wilayani Mbarali katika mkoa wa Mbeya.
“Suala la ngano lioneni kama ni fursa, huu mfumo wa “block funding” wa kuwaweka wakulima wadogo sehemu moja kupunguza gharama za uzalishaji wa ngano na kuifanya ngano ya Tanzania iwe na ushindani,” amesema Bashe katika mkutano huo.