Uviko-19 wachangia ongezeko la wagonjwa wa TB duniani
India inaendelea kubeba mzigo mkubwa zaidi wa wagonjwa wa kifua kikuu duniani yasema WHO. Picha | ILO/Vijay Kutty.
- Watu milioni 10.6 waliugua ugonjwa kifua kikuu (TB) mwaka 2021.
- Ni ongezeko la asilimia 4.5 ndani ya mwaka mmoja.
- Uviko-19 wachangia watu wengi kuugua TB.
Dar es Salaam.Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) inakadiria kuwa watu milioni 10.6 waliugua ugonjwa kifua kikuu (TB) mwaka 2021, huku janga la Uviko-19 baada ya kutatizika kwa matibabu ya ugonjwa huo.
Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 4.5 kutoka mwaka 2020, na watu milioni 1.6 walikufa kutokana na TB ambapo kati yao watu 187,000 wakiwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Taarifa ya shirika hilo kutoka Geneva Uswisi imesema ripoti hiyo ya mwaka 2022 ya Kifua Kikuu imeonesha kuwa hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi kuwa na ongezeko wa wagonjwa wa kifua kikuu.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus ametaja janga la Uviko-19 kuwa kichocheo cha watu wengi kukosa dawa za kujitibu kifua kikuu.
“Kama kuna kitu tumejifunza kutokana na janga la Uviko-19 ni kwamba kwa mshikamano, kufanya maamuzi, uvumbuzi na utumiaji sawa wa zana, tunaweza kushinda vitisho vikali vya kiafya.
“Hebu tutumie masomo hayo kwenye eneo la kifua kikuu. Ni wakati wa kumkomesha muuaji huyu wa muda mrefu. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kukomesha TB,” amesema Dk Tedros.
Ugonjwa wa kifua kikuu ni muuaji wa pili wa magonjwa ya kuambukiza duniani, baada ya Uviko-19.
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria ambao mara nyingi huathiri mapafu, lakini unaweza kuzuilika na kutibika.
Huduma za afya kwa ujumla ziliathiriwa sana wakati wa janga la Uviko-19, lakini athari zake kwa wagonjwa wa TB imekuwa mbaya. Hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na migogoro inayoendelea huko Ulaya, Afrika pamoja na Mashariki ya Kati.
Kuendelea kwa changamoto za kutoa na kupata huduma muhimu za TB kumesababisha watu wengi waliokuwa na ugonjwa huo kutogunduliwa na kutibiwa.
Idadi ya watu waliogunduliwa hivi karibuni ilipungua kutoka milioni 7.1 mwaka 2019 hadi milioni 5.8 mwaka 2020, kulingana na ripoti ya Global TB.
Ingawa kulikuwa na ahueni ya kiasi hadi milioni 6.4 mwaka 2021, hata hivyo utambuzi huo bado ulikuwa chini ya viwango vya kabla ya janga.
Soma zaidi:
Kupungua huku kunaonesha kuwa idadi ya watu wenye TB ambayo haijagunduliwa au ambayo haijatibiwa imeongezeka, WHO imesema, na kusababisha kuongezeka kwa vifo na maambukizi zaidi na hatimaye watu wengi zaidi wanaougua ugonjwa huo.
Kumekuwa na habari njema, ulimwenguni kote, watu milioni 26.3 walitibiwa TB kati ya 2018 na 2021, ingawa ni pungufu ya lengo la milioni 40 lililowekwa miaka minne iliyopita.
Matibabu ya kuzuia TB kwa watu wanaoishi na VVU pia ilivuka lengo la kimataifa la milioni sita, na kufikia zaidi ya milioni 10 katika kipindi hicho.
Ripoti hiyo inasisitiza haja ya nchi kutekeleza hatua za haraka kurejesha upatikanaji wa huduma muhimu za TB.
Pia inataka uwekezaji uongezeke, na hatua zichukuliwe, kushughulikia kwa upana wake viambukizi vinavyosababisha milipuko ya TB na athari zake za kijamii na kiuchumi pamoja na hitaji la uchunguzi mpya, dawa na chanjo.
WHO itaitisha mkutano wa ngazi ya juu mapema mwaka 2023 ili kuimarisha maendeleo ya chanjo, kwa kuzingatia walichojifunza kutoka kwa janga hili.