WHO: Janga la Uviko-19 limeimarisha mapambano dhidi ya malaria
- Ni baada ya nchi mbalimbali kuchukua hatua za kupunguza athari za Uviko-19
- Ripoti yaonesha kasi ya ongezeko la wagonjwa imepungua
Dar es salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema janga la Uviko-19 lilisaidia kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kutokana na kuongezeka kwa juhudi za kukabiliana na athari za janga hilo.
Kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya mwaka 2022 ya ugonjwa wa malaria imeonesha kuwa kulikuwa na vifo vya malaria vinavyokadiriwa kufikia 619,000 duniani kote mwaka 2021 ikilinganishwa na vifo 625,000 katika mwaka wa kwanza wa janga la Uviko-19.
Mkurugenzi wa WHO, Daktari Tedros Ghebreyesus amesema kupungua kwa idadi ya vifo vitokanavyo na malaria kumesababishwa na kuongeza juhudi za kupunguza athari mbaya zaidi za usumbufu unaohusiana na Uviko-19 kwa huduma za malaria.
“Kufuatia ongezeko kubwa la wagonjwa wa malaria na vifo katika mwaka wa kwanza wa janga la Uviko-19, nchi zilizoathiriwa na ugonjwa wa malaria ziliongeza juhudi zao na kuweza kupunguza athari mbaya zaidi za usumbufu unaohusiana na Uviko-19 kwa huduma za malaria,” amesema Dk Tedros.
Soma zaidi
Ripoti hiyo inaeleza kuwa ingawa wagonjwa wa malaria wameendelea kuongezeka kati ya mwaka 2020 na 2021, lakini ni kwa kiwango cha polepole kuliko kipindi cha mwaka 2019 hadi 2020.
Idadi ya wagonjwa wa malaria duniani kote ilifikia watu milioni 247 mwaka 2021, ikilinganishwa na watu milioni 245 mwaka 2020 na watu milioni 232 mwaka 2019.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mwaka 2021 jumla ya vyandarua milioni 128 vilisambazwa katika maeneo yenye malaria kama njia kuu ya kupambana na ugonjwa huo kati ya vyandarua milioni 175 vilivyotakiwa kusambazwa.
Pamoja na mwaka 2021 kuvunja rekodi ya kusambaza vyandarua vingi zaidi kuliko wakati wowote yapo baadhi ya mataifa ambayo hayakusambaza kabisa vyandarua kama Botswana, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Chad, Haiti, India, Pakistan na Sierra Leone.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Viashiria vya Malaria nchini Tanzania wa mwaka 2017 unaonesha kuwa asilimia 78 ya kaya zote nchini Tanzania zinamiliki angalau chandarua kimoja chenye dawa.
Latest