Watumiaji wa huduma za simu wafikia milioni 64.1 Tanzania
- Wameongezeka kwa asilimia 3.6 katika robo ya pili ya mwaka 2022/23.
- Asilimia 30 ya wanatumia mtandao wa Vodacom.
Dar es Salaam. Huenda changamoto ya mawasiliano kwa njia ya simu za mikononi ikasahaulika Tanzania siku zijazo baada ya kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa huduma za simu ambao wamefikia milioni 64.1.
Matumizi ya simu hupimwa kwa idadi ya watu waliojisajili kutumia mitandao ya simu za mkononi na mezani inayotoa huduma hiyo (Vodacom, Tigo, Airtel, TTCL, Halotel na Smile) kwa laini iliyotumika angalau mara moja katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa Ripoti ya takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya robo ya pili ya mwaka 2023 (Aprili hadi Juni 2023) imebainisha kuwa watumiaji wameongezeka kutoka milioni 61.9 walioripotiwa Machi 2023 hadi kufikia milioni 64.1 mwaka ulioishia Juni 2023.
Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 3.6 ndani ya kipindi cha miezi mitatu.Â
Idadi ya watumiaji wa simu imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja unaoishia Juni 2023, watumiaji wa vifaa hivyo vya mawasiliano wameongezeka kutoka milioni 56.2 walioripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2022.
Soma zaidi
-
Vodacom, Tigo: Jino kwa jino watumiaji wa simu Tanzania
-
Mikoa 10 vinara matumizi ya simu za mkononi Tanzania
Mchuano mkali mitandao ya simu
Wakati watumiaji wa simu wakiongezeka, kampuni ya Vodacom ndio inaongoza kuwa na watumiaji wengi zaidi. Hadi kufikia Juni 2023, kampuni hiyo ilikuwa na watumiaji milioni 19.1 sawa na asilimia 30 ya watumiaji wote.
Mtandao wa Airtel unafuatia kwa kuwa na watumiaji milioni 17.5 huku Tigo ukishika nafasi ya tatu kwa kuwa na watumiaji milioni 17.4, ingawa kampuni zote mbili zinashikilia asilimia 27 ya soko la mawasiliano ya simu nchini.
Halotel imeshika nafasi ya nne ikiwa na watumiaji milioni 8.4, TTCL (milioni 1.5) na Smile inashika nafasi ya mwisho ikiwa na watumiaji 13,840 pekee.
Kutokana na kutokuwa na mtandao unaomiliki soko kwa zaidi ya asilimia 35, TCRA katika ripoti hiyo imebainisha kuwa kuna ushindani wenye afya kati ya watoa huduma ya mawasiliano.
Simu zimekuwa nyenzo ya kuwawezesha watu kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi na hivyo kujiletea maendeleo.Â
Latest