Watumiaji wa huduma za simu Tanzania waongezeka kwa asilimia 4.6
- Asilimia 18 ya watumiaji wa huduma za simu nchini wapo Dar es Salaam.
- Mikoa ya Kaskazini Pemba na Unguja yashika mkia.
- Ni fursa ya Watanzania kujiimarisha kiuchumi.
Dar es Salaam. Huenda kasi ya maendeleo nchini Tanzania ikaongezeka, mara baada ya sekta ya mawasiliano kuendelea kushuhudia ukuaji chanya katika maeneo mbalimbali ikiwemo matumizi ya huduma za simu.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Mwenendo wa Sekta ya Mawasiliano Julai – Septemba, 2023 iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Bakari Jabir leo Oktoba 25, 2023, mpaka mwezi Septemba watumiaji wa huduma za simu nchini Tanzania ni 67.1 milioni.
Idadi hiyo imeongezeka kutoka watumiaji milioni 64 waliorekodiwa mwezi Juni mwaka huu ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 4.6
Matumizi ya simu nchini hupimwa kwa idadi ya watu waliojisajili kutumia mitandao ya simu za mkononi na mezani inayotoa huduma ya mawasiliano ya Vodacom, Tigo, Airtel, TTCL, Halotel na Smile kwa kuangalia laini zilizotumika angalau mara moja kwa kipindi cha miezi mitatu.
Soma zaidi : DP World kuendesha bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 30
Mikoa vinara kwa matumizi ya huduma za simu
Taarifa ya TCRA imebainisha kuwa mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kuwa kinara kwa kuwa na watumiaji wengi zaidi wa huduma za simu wakifikia milioni 12.3 kutoka milioni 11 iliyokuwepo mwezi Juni mwaka huu.
Idadi hiyo ya watumiaji wa huduma za simu jijini Dar es Salaam ni sawa na asilimia 18 ya watumiaji wote waliopo nchini Tanzania.
Hii ni kumaanisha kuwa katika watu 100 wanaotumia huduma za simu watu 18 wapo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi za mwaka 2022 jiji la Dar es Salaam lina jumla ya wakazi milioni 5.4.
Soma zaidi : Haya ndiyo magari 10 yanayopendwa zaidi na Watanzania
Kwa mujibu wa takwimu hizo ni sawa na kusema karibu kila mkazi wa jiji la Dar es Salaam anamiliki laini mbili za simu za mkononi
Mbali na Dar es Salaam, mikoa mingine tisa yenye watumiaji wengi wa huduma simu za mkononi ni Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Morogoro,Tabora, Kilimanjaro,Tanga na Geita.
Mikoa hiyo 10 ina jumla ya watumiaji milioni 38.9 ambao ni sawa na asilimia 58 ya watumiaji wote nchi nzima.
Majiji sita yameingia katika orodha ya maeneo yenye watumiaji wengi zaidi, ambayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma, Arusha, Tanga pamoja na Mwanza.
Unguja watumiaji Kiduchu
Wakati mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa watumiaji wa simu mkoa Kaskazini unguja, na Kusini unguja na imeshika mkia kwa kuwa na watumiaji wachache wa vifaa hivyo vya mawasiliano.
Kwa mujibu wa takwimu za TCRA mkoa wa Kaskazini unguja una watumiaji 92,336 iliyoongezeka kutoka wakati Kusini Unguja ina watumiaji 61,360 pekee.
Huenda uchache huo ukachangiwa na idadi ndogo ya wau iliyopo kulinganisha na wingi wa watu uliopo katika majiji mengine nchini.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika Agosti 2022 mkoa wa Kaskazini unguja una wakazi 257,290 idadi ndogo kidogo baada ya kusini unguja yenye wakazi 195,873.
Ongezeko ni fursa
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya mawasiliano na uchumi wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa ongezeko la watumiaji wa simu linatoa fursa kwa watu kuwasiliana kwa njia ya sauti na kuperuzi mtandaoni .
“Kiuchumi inampa fursa Mtanzania wa kawaida kushiriki katika manunuzi ya mtandaoni. Biashara zikiimarika maana yake ni mapato kwa Serikali na ndiyo maana utaona Serikali inataka kurasimisha hizi biashara za mtandaoni, inaongeza wigo wa mapato kwa mamlaka husika,” anasema Bernard Mumwi, mchambuzi wa kujitegemea wa masuala ya uchumi.
Pia inaongeza uwanda wa kutuma na kupokea pesa popote kwa urahisi, jambo linalosaidia kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa wananchi wote ili kuwaondolea vikwazo kuendesha shughuli zao.
“Mzunguko mkubwa wa pesa una boresha hata thamani ya shilingi ya Tanzania,” anaeleza Mumwi na kubainisha kuwa simu zimesaidia watu kufanya biashara za kimataifa.
Ongezeko la matumizi ya simu linachochea shughuli za utalii anaeleza mtalaam huyo “ukipanda mlima Kilimanjaro leo, ukaenda mubashara au ukaenda Ngorongoro ukatuma picha Facebook ama Instagram, rafiki zako Marekani watavutiwa kuja kutalii. Na unajua utalii ni mlango wa Foreign Direct Investment (fedha za kigeni) Tanzania.”