Simu za mezani bado zipo zipo sana

August 30, 2022 12:15 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Matumizi yake yaongezeka kwa ndani ya mwaka mmoja uliopita.
  • Hadi Juni 2022, kulikuwa na watumiaji 71,650. 

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaoamini kuwa simu za mezani hazitumiki kwa sasa, fahamu kuwa bado zipo zipo sana. 

Matumizi ya simu hizo yanazidi kuongezeka Tanzania licha ya kuwa ongezeko lake ni dogo ikilinganishwa na simu za mkononi ambazo ndiyo maarufu kwa sasa.

Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za mawasiliano ya robo ya pili ya mwaka 2022 iliyotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia mwaka unaoishia Juni 2022 watumiaji wa simu za mezani walikuwa 71,650 kutoka 71,405 waliorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Hilo ni sawa na ongezeko la watumiaji 245 au asilimia 0.34 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Idadi hiyo ya watumiaji wa simu za mezani ni sawa na asilimia 0.13 ya watumiaji wote milioni 56.2 wa simu Tanzania waliorekodiwa hadi Juni mwaka huu.

Simu za mezani ni pamoja na zile zisizohamishika kwa maana kuwa zimeunganishwa na mfumo wa waya kufanikisha mawasiliano ya watu, ofisi au kampuni.

Pia ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika miezi ya hivi karibuni idadi ya wanaotumia simu za mezani imekuwa ikiongezeka mfululizo hasa katika robo ya pili ya mwaka 2022.

Mathalan Aprili mwaka huu kulikuwa na watumiaji wa simu za mezani 71,479, mwezi uliofuata wakaongezeka hadi 71,492 kabla hawajaongezeka zaidi hadi kufikia 71,650 mwezi Juni.

Kwa sehemu kubwa, huduma za simu za mezani zinatolewa na kampuni ya TTCL ambayo inamilikiwa na Serikali. 

Simu za mezani zimekuwa zikitumika zaidi kwa mawasiliano ya kiofisi kutokana na ufanisi wake katika kuwasiliana.

Upepo umebadilika

Kwa sasa, simu za mkononi ndiyo zimeshikilia soko, jambo linalodhihirisha mageuzi makubwa katika sekta ya mawasiliano nchini. 

Mwaka 1995 ilikuwa ni anasa kumiliki simu ya mkononi. Kati ya watumiaji 100 wa simu, ni takriban watatu tu walikuwa wakitumia simu za mkononi kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Wakati huo, watumiaji wa simu za mkononi walikuwa 2,198 kati ya watumiaji 90,298 waliokuwepo nchini ambapo huduma za simu za mezani ilikuwa ni habari ya mjini.

Hali hiyo ilitokana na simu za mkononi kuwa ghali na teknolojia kutofika katika maeneo mengi Tanzania.


Zinazohusiana:  


Simu za mkononi zimechangia kwa kiasi kubwa kuleta maendeleo nchini kwa kuongeza kasi ya mawasiliano huku mapinduzi makubwa yakitokea baada ya kuanza kutoa huduma za kifedha.

Kwa mujibu wa TCRA, hadi kufikia Juni 2022, Tanzania ilikuwa na watumiaji wa simu za mkononi milioni 56.2 na idadi hiyo imekuwa ikipanda kila mwaka. 

Kwa sasa, kampuni ya Vodacom Tanzania ndiyo inaongoza kuwa na watumiaji wengi ambapo hadi Juni walikuwa milioni 17.2 sawa na asilimia 31 ya watumiaji wote.

Vodacom inachauna vikali na Airtel ambayo ilikuwa na watumiaji milioni 15.9 ikifuatiwa na Tigo iliyokuwa na watumiaji milioni 14.9.

Kampuni hizo zote tatu zinamiliki soko la mawasiliano ya simu kwa asilimia 85 huku asilimia zilizobaki zikimilikiwa na kampuni nyingine ikiwemo TTCL na Halotel.

 

Huu ndiyo mwisho wa simu za mezani?

Simu za mezani zitaendeleza kuwepo kwa muda mrefu ujao hasa kwa shughuli za kiofisi ambazo hazihitaji simu za kuhamishika.

Mtaalam wa Tehama, John Mwakipesile anasema huduma za simu zitaendelea kuwepo kwa sababu kinachoabdilika ni teknolojia ya uendeshaji lakini dhana ya simu hizo inabaki kama ilivyo.

“Simu hizo zimekuwepo kwa muda mrefu na haziwezi kutoweka kwa sababu  zinatoa uhakika wa mawasiliano hasa ofisini,” anasema Mwakipesile.

Simu hizo pia zinaondoa changamoto ya kutembea na kifaa hicho badala yake inakua sehemu moja na hivyo kuondoa changamoto ya kuharibika. 

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...