Dar es Salaam kinara matumizi huduma za simu Tanzania

July 20, 2023 11:05 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Asilimia 18 ya watumiaji wa huduma za simu nchini wapo Dar es Salaam
  • Mikoa ya Kaskazini Pemba na Unguja yashika mkia.

Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kuwa kinara kwa watumiaji wengi wa huduma ya simu za mkononi Tanzania ambapo kwa sasa mkoa huo una takribani watumiaji milioni 11.8.

Matumizi ya simu nchini hupimwa kwa idadi ya watu waliojisajili kutumia mitandao ya simu za mkononi na mezani inayotoa huduma ya mawasiliano ya  Vodacom, Tigo, Airtel, TTCL, Halotel na Smile kwa kuangalia laini zilizotumika angalau mara moja kwa kipindi cha miezi mitatu.

Kwa mujibu wa  takwimu za robo ya pili ya mwaka 2023 (Aprili-Juni 2023) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaongoza kwa kuwa na watumiaji wa simu za mkononi milioni 11.8

Takwimu za TCRA zinaonesha kuwa mpaka mwezi Disemba 2022, Dar es Salaam ilikuwa na watumiaji milioni 10.6 ambao wameongezeka hadi milioni 11.8.

Idadi hiyo ya watumiaji wa huduma za simu jijini Dar es Salaam ni sawa na asilimia 18.7 ya watumiaji wote waliopo nchini Tanzania.Hii ni inamaanisha  kuwa katika watu 100 wanaotumia huduma za simu watu 18 wapo jijini Dar es Salaam.

Idadi hiyo ya watumiaji wa huduma za simu imeongezeka kutoka milioni 10.9 ilyokuwepo mwezi Machi 2023 hadi milioni 11.7 mwezi Juni.Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 18.4 ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni 2023.

Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi za mwaka 2022 jiji la Dar es Salaam lina jumla ya wakazi milioni 5.4.

Kwa mujibu wa takwimu hizo ni sawa na kusema kila mkazi wa jiji la Dar es Salaam anamiliki laini mbili za simu za mkononi 

Mbali na Dar es Salaam, mikoa mingine tisa yenye watumiaji wengi wa huduma simu za mkononi ni Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Morogoro,Tabora, Kilimanjaro,Tanga na Geita.

Katika mikoa hiyo 10 ina jumla ya watumiaji milioni 36.4 ambao ni sawa na asilimia 56.8 ya watumiaji wote nchi nzima.

Majiji sita yameingia katika orodha ya maeneo yenye watumiaji wengi zaidi, ambayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma, Arusha, Tanga pamoja na Mwanza.

Unguja na Pemba watumiaji Kiduchu

Wakati mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa watumiaji wa simu mkoa Kaskazini unguja, Kusini unguja na Pemba imeshika mkia kwa kuwa na watumiaji wachache wa vifaa hivyo vya mawasiliano.

Kwa mujibu wa takwimu za TCRA mkoa wa Kaskazini unguja una watumiaji wa simu za mkononi 58,591 iliyoongezeka kutoka 56,907 iliyokuwepo mwezi Machi mwaka huu.

Mkoa wa Kusini unguja ulikuwa na watumiaji wa simu za mkononi 88,169 ikifuatiwa na Kaskazini pemba yenye watumiaji 99,065.

Huenda uchache huo ukachangiwa na idadi ndogo ya wau iliyopo kulinganisha na wingi wa watu uliopo katika majiji mengine nchini.

Kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika Agosti 2022 mkoa wa Kaskazini unguja una wakazi 257,290  idadi ndogo kidogo baada ya kusini unguja yenye wakazi 195,873.


Zinazohusiana


Watumiaji waongezeka 

Kwa mujibu wa Ripoti ya takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya robo ya pili ya mwaka 2023 (Aprili hadi Juni 2023) imebainisha kuwa watumiaji wameongezeka kutoka milioni 61.9 walioripotiwa Machi 2023 hadi kufikia milioni 64.1 mwaka ulioishia Juni 2023.

Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 3.6 ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya mawasiliano na uchumi wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa ongezeko la watumiaji wa simu linatoa fursa kwa watu kuwasiliana kwa njia ya sauti na kuperuzi mtandaoni .

“Kiuchumi inampa fursa Mtanzania wa kawaida kushiriki katika manunuzi ya mtandaoni. Biashara zikiimarika  maana yake ni mapato kwa Serikali na ndiyo maana utaona Serikali inataka kurasimisha hizi biashara za mtandaoni, inaongeza wigo wa mapato kwa mamlaka husika,” anasema Bernard Mumwi, mchambuzi wa kujitegemea wa masuala ya uchumi. 

Pia inaongeza uwanda wa  kutuma na kupokea pesa popote kwa urahisi, jambo linalosaidia kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa wananchi wote ili kuwaondolea vikwazo kuendesha shughuli zao.

“Mzunguko mkubwa wa pesa una boresha hata thamani ya shilingi ya Tanzania,” anaeleza Mumwi na kubainisha kuwa simu zimesaidia watu kufanya biashara za kimataifa.

Ongezeko la matumizi ya simu linachochea shughuli za utalii anaeleza mtalaam huyo “ukipanda mlima Kilimanjaro leo, ukaenda mubashara au ukaenda Ngorongoro ukatuma picha Facebook ama Instagram, rafiki zako Marekani watavutiwa kuja kutalii. Na unajua utalii ni mlango wa Foreign Direct Investment (fedha za kigeni) Tanzania.” 

Enable Notifications OK No thanks