Bei ya mafuta yaendelea kung’ata watumiaji, wamiliki vyombo vya moto Tanzania
- Lita moja ya petroli yaongezeka kwa Sh68 na dizeli kwa Sh189.
- Kupanda kwa gharama za mafuta na uagizwaji kwatajwa kama sababu.
Dar es Salaam. Ni kama bei ya mafuta inawaambia watumiaji wa vyombo vya moto Tanzania ‘bado hamjasema’ kwa kwenda kinyume na matarajio ya wengi wakidhani labda safari hii itakuwa ahueni lakini bei mpya zinaonesha sivyo.
Hii inaashiria wamiliki na watumiaji wa vyombo vya moto wataendelea kutoboa mifuko yao ili kupata huduma hiyo muhimu kwa ukuaji wa uchumi ambayo imekuwa ikipanda mfululizo tangu Julai 2023.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) katika taarifa yake ya bei mpya za mafuta zinazoanza kutumika leo Octoba 4, 2023 imeeleza kuwa lita moja ya petroli jijini Dar es Salaam inauzwa Sh3,281 huku ya dizeli ikiuzwa Sh3,448.
Hii ina maana kuwa bei ya petroli jijini Dar es Salaam kwa lita imeongezeka kwa Sh68 kutoka Sh3,213 ya Septemba huku ya dizeli ikiongezeka kwa Sh189.
Bofya hapa kuona bei za mafuta mwezi Octoba nchi nzima.
Ewura imesema kupanda kwa bei ya mafuta mwezi Octoba kumechagizwa na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia hadi kufikia asilimia 4.21 huku gharama za uagizwaji mafuta zikiongezeka kwa silimia 17 kwa petroli na asilimia 62 kwa dizeli.
“Pia, uamuzi wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani (OPEC+) kupunguza uzalishaji na vikwazo vya kiuchumi ambavyo nchi ya Urusi imewekewa na mataifa ya magharibi,” imeainisha taarifa ya Ewura.
OPEC ina wanachama 13 ikiwemo Saudi Arabia na washirika wake 10 wakiongozwa na Urusi ambapo Julai 2023 waliazimia kupunguza uzalishaji wa mafuta ili kuongeza thamani ya bidhaa hiyo muhimu duniani.
Maumivu ya kupanda kwa mafuta hayajaishia Dar es Salaam pekee, mikoa mingine yenye bandari kama Mtwara na Tanga nako moto ni ule ule.
Soma zaidi : Dk. Mpango atoa maagizo mazito kwa ATCL akipokea ndege mpya
Mafuta yanayopitia bandari ya Mtwara bei ya petroli imepanda kwa Sh68 na kufikia Sh3,353 kwa lita huku dizeli ikiuzwa Sh3,520 kutoka Sh3,332 ya mwezi uliopita.
Aidha, wanaotumia mafuta yanayopitia bandari ya Tanga wao watanunua petroli kwa Sh3,327 kutoka Sh3,259 na lita ya dizeli inauzwa Sh3,494.
Kyerwa bei juu zaidi
Licha ya kupanda kwa bei ya mafuta kwa viwango tofauti, wakazi wa Ruberwa, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera wao ndio wananunua mafuta kwa bei ya juu zaidi kuliko maeneo mengine nchini.
Katika eneo hilo petroli inauzwa kwa Sh3,519 na dizeli Sh3,686.
Hii ina maana kuwa wakazi wa eneo hilo wananunua lita moja ya petroli na dizeli kwa Sh238 juu zaidi ya wakazi wa Dar es Salaam.
Kutokana na kupanda kwa bei za mafuta mwaka 2022 kuliko changiwa na vita kati ya Ukraine na Urusi, Mei mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilitangaza kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni katika bidhaa hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi kila mwezi ili kuwapunguzia Watanzania ukali wa maisha.
Hata hivyo, iliondolewa Januari 2023 baada ya bei za mafuta kuanza kupungua.
Latest