Viongozi wa Chadema waongoza maelfu ya wafuasi kuandamana Dar es Salaam
- Ni maandamano ya amani kushinikiza kuondolewa kwa miswada ya sheria za uchaguzi.
- Ni pamoja na ule wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Dar es Salaam. Viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe wameongoza maelfu ya wafuasi wa chama hicho kuandamana wakipinga miswada mitatu ya uchaguzi pamoja na ugumu wa maisha.
Maandamano hayo yaliyoanza asubuhi ya leo Januari 24, 2024 yaliitishwa Januari 13 na mwenyekiti wa chama hicho akisema lengo ni kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba 10 mwaka jana ambayo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa yote ya mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi.
Aidha, Mbowe alibainisha kuwa lengo jingine la maandamano hayo ni kuishinikiza Serikali kusikiliza maoni ya wananchi na kutaka itengeneze mpango wa dharura wa kukabiliana kwa kupanda gharama za maisha kwa Watanzania na mfumuko wa bei.
Alfajiri ya leo, Januari 24, 2024, wananchi walianza kujitokeza katika vituo viwili vya maandamano katika eneo la Buguruni na katika kituo cha mabasi cha Magufuli wakiwa mabango yenye ujumbe unaoelekezwa kwa viongozi wa Serikali tayari kuanza safari ya itakayoishia ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) hapa nchini.
Soma zaidi: Zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi hawajaripoti kidato cha kwanza Magu
Miongoni mwa jumbe zilizoandikwa kwenye mabango yaliyobebwa na waandamanaji unasomeka: “Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu usimamiwe na tume huru na sio Tamisemi,” huku mwingine akiandika “Rais Samia umesaliti 4r’s. Jisahihishe”.
Maandamano hayo yalifika ofisi za UN zilizopo barabara ya Sam Nujoma Saa 9:15 alasiri huku wafuasi wakiwa nje wakiimba nyimbo mbalimbali zikiwemo kushuka kwa gharama za maisha.
Baada ya kuwasili ofisi za UN, Mbowe na baadhi ya viongozi waliingia ndani ya ofisi hizo ambapo kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wamewasilisha malalamiko yao kwenda kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mtaifa Antonio Guteres kupitia kwa Mwakilishi Mkazi wa Un nchini Zlatan Milišić.
“Maandamano yetu yalikuwa yanafikia tamati kwenye ofisi za UN ambapo sisi kama chama kikuu cha upinzani kwa niaba ya Chadema na Watanzania wengine wote ambao wanaona kuna mambo hayapo sawa, tumeleta mashtaka yetu kwenda kwa Katibu Mkuu wa UN, New York…
Muwakilishi wa UN amepokea barua yetu kwa niaba ya Katibu ya Mkuu wa UN, barua hiyo ikishapokelewa rasmi tutaisambaza kwa vyombo vyite vya habari,” amesema Mbowe.

Baadhi ya wandamanaji hao waliokuwa wamevalia sare mbalimbali za chama hicho, walikuwa wakiimba: “Polisi wote mishahara juu, polisi mishahara juu…walimu wote mishahara juu”.
Jakobo Bailemba (70), Mkazi wa Tabata Kimanga jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa, kuongezeka kwa gharama za maisha ni miongoni mwa sababu zilizomchochea kuingia kwenye maaandamano licha ya uzee wake.
“Hakuna kitu tulichonacho Tanzania kama matatizo yaliyosababishwa na Rais Samia, tuna shida haina mfano…sukari imepanda saivi kilo ni Sh5,000 wazee tunadanganywa ukienda hospitali ni bure, lakini nenda pale unakuta wazee wanakufa pale…nisiandamane mwanangu? kuandamana ni haki yangu,” amesema mzee huyo aliyekuwa ameshika fimbo ya kutembelea.
Kwa upande wake mwanaharakati mashuhuri Dk. Ananilea Nkya amesema kuwa licha ya kuwa maandamano hayo yameitishwa na chadema, wameona ni vyema kujitokeza ili kushinikiza kupatikana kwa katiba mpya na sheria bora za uchaguzi zitakazoleta viongozi wawajibikaji.
“Tukiwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo kila anayegombea awe mwanamke au mwanaume ni bora tutakuwa na viongozi bora wanaowajibika kwa wananchi,” amesema Dk. Ananilea Nkya.
Tofauti na miaka ya nyuma, jeshi la polisi limeimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ambako waandamanaji hao wanapita, jambo lililopongezwa na kupokelewa vyema na Watanzania wengi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alikutana na wafuasi na wanachama wa Chadema na kuwapa salamu za kubariki maandamano hayo akidai ni za Rais Samia Suluhu Hassan huku akiwasihi kuandamana bila kusababisha uvunjifu wa amani.
Habari hii imeongezwa nukuu za waandamanaji na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe
(Imeandikwa na Esau Ng’umbi na Nuzulack Dausen)
Latest