Jeshi la Polisi lapiga marufuku maandamano ya Chadema Dar
Dar es Salaam. . Jeshi la Polisi limekitaka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kusitisha mara moja mipango ya kufanya maandamano yaliyokusudiwa kufanyika Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Jeshi la Polisi inakuja ikiwa imepita siku moja tangu Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe kutangaza kuwa wataandamana ili kuishinikiza Serikali kuwajibika kutokana na matukio ya utekaji na mauaji yaliyoripotiwa.
Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Septemba 13, 2024 amesema maandamano ya Chadema yanakusudia kuwatoa kwenye reli ya uchunguzi wa tukio la kifo cha aliyekuwa kada wa chama hicho Ally Kibao.
Kwa mujibu wa Chadema Kibao aliuwawa baada ya kutekwa na watu wawili wenye silaha ndani ya basi la Tashrif eneo la Tegeta akiwa safarini kutokea Dar es Salaam kwenda Tanga.
Hata hivyo, Misime amesema tayari kuna hatua imeshapigwa na vyombo vya uchunguz kwenye tukio hilo kama vilivyoagizwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hivyo Jeshi la Polisi limetoa onyo na katazo kwa wafuasi wa Chadema kushiriki katika maandamano hayo.
“Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kwa viongozi wa chama hicho kuacha kuendelea kuhamasisha wananchi kujihusisha katika uhalifu huo na yeyote atakae ingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi, “ amesema Misime.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka watu wote walioalikwa kushiriki maandamano hayo kutoka mkoa wowote kutofanya hivyo kwa kuwa maandamano hayo ni haramu na hayatofanyika.
Hii ni mara ya pili kwa Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya Chadema mara baada ya yale yaliyopangwa kufanyika Agosti 12, 2024 jijini Mbeya kuzuiliwa ambapo baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwemo Mbowe walikamatwa.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi jumla ya wafuasi 520 wa Chadema waliopanga kushiriki kwenye maandamano hayo kuadhimisha siku ya vijana duniani.