Chadema yashinikiza mabadiliko ya kimifumo kuelekea uchaguzi mkuu 2025
- Yasema kama hakutakuwa na mabadiliko uchaguzi hautafanyika.
Dar es salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa msimamo wake kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2025 kikishinikiza mabadiliko ya kimifumo kabla ya kufanyika uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Disemba 10, 2024 ameyataja masuala yanayohitaji kufanyiwa mabadiliko ikiwemo madai ya kuminywa kwa uhuru wa vyama vya upinzani kushiriki uchaguzi.
“Sisi kama Chadema tunasema tutaendelea kuangalia kwa ukaribu ni nini kinabadilika yapo mambo mengi tutakaa na wadau wengine kuweka ajenda za nchi za mabadiliko ikifika mwaka 2025 wakati wa uchaguzi na hakuna ‘reform; zozote zimefanyika tutafanya maamuzi sahihi lakini ‘no reform no election’” amesema Mbowe.
Mbali na kuweka msimamo huo Mbowe amebainisha maazimio ya kamati kuu ya chama hicho ambayo ni pamoja na kulaani vitendo vya unyanyasaji ikiwemo mauaji,na vipigo uliofanywa na jeshi la polisi kwa wagombea, mawakala, viongozi na wanachama wa chama,
Kwa mujibu wa Mbowe vitendo hivyo vilivyofanyika kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka huu vinafanana na yale yaliyofanyika katika chaguzi zilizopita jambo ambalo linakandamiza demokrasia ya vyama vingi nchini.
“Matatizo yalioonekana katika uchaguzi huu hayana tofauti yoyote na matatizo yaliyojitokeza mwaka 2019 na mwaka 2020 watu ni wale wale mambo ni yale yakle, sisi kama chama kikuu lazima tuweke nguvu zetu za pamoja.” amebainisha Mbowe.
Hata hivyo, malalamiko hayo yanatofautiana na kauli ya Serikali iliyothibitisha uchaguzi huo kuwa huru na haki huku ukitoa mtazamo chanya kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Mwaka 2025.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu amesema tatizo kubwa linalozuia uchaguzi wa huru na wa haki nchini ni ubovu wa mifumo ya uchaguzi.
“Sisi hatijashindwa uchaguzi na CCM tumeshindwa uchaguzi na jeshi la polisi , idara ya usala wa taifa na mfumo mzima wa tawala za za mikoa, wakuu wa wilaya, mkurugenzi na watumishi wake wote, tmeshindwa na uchaguzi na walimu waliosimamia uchaguzi na sio CCM…
…Tatizo letu la msingi ni mfumo wa uchaguzi huu unaopanga polisi, usalama wa Taifa, watumishi wa umma badala ya kusimamia uchaguzi na kutenda haki wanakuwa wao ndio wapambanaji wa uchaguzi huo na wanaamua nani anashinda,”ameeleza Lissu.
Katika hatua nyingine Mbowe amewataka wanachama wa Chadema na Watanzania wote wanaotaka haki kuungana na kuonyesha ujasiri wa kupigania mabadiliko bila kukata tamaa.
“Tutakutana na vikwazo vingi, kamwe tusikubali vifanye tukate tamaa kwa sababu kukata tamaa ni dhambi kubwa sana duniani,” amesema huku akiapa kuwa chama chake kitasimama imara kupigania mustakabali bora wa Taifa.