Mbowe atoa msimamo mpya kuhusu katiba mpya, maridhiano

March 18, 2022 10:04 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema katiba mpya, tume huru ni ajenda za kudumu za Chadema.
  • Akubali kufanya mazungumzo kutafuta muafaka wa kitaifa.
  • Akataa kushiriki kongamano la TCD mwishoni mwa Machi.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema katiba mpya itaendelea kuwa ajenda kuu ya chama hicho huku akibainisha kuwa hatashiriki kongamano la Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD) likalofanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Mbowe aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 18, 2022 kuhusu maadhimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi wiki hii amesema katiba na tume huru ya uchaguzi vitaendelea kuwa ajenda ya kudumu ya chama hicho.

“Tatizo la nchi yetu ni katiba, la pili tatizo la uvurugaji wa uchaguzi katika nchi hii liko kwenye Tume ya Uchaguzi. Sisi kama chama tukaamua hizi ndiyo ajenda zetu kuu na kwa sababu tulikuwa na imani hizi ni ajenda za wananchi,” amesema Mbowe ambaye hivi karibuni aliachiwa huru baada ya kufutiwa mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili na wenzake watatu.

Amesema hata baada ya yeye kutoka gerezani, msimamo huo haujabadilika huku akisisitiza kuwa, “Chadema na Katiba hutatutenganishwa.”

Aidha, amesema katika kuzifikia ajenda hizo mbili, kwa sasa watatumia njia ya mazungumzo zaidi na makundi mbalimbali ikiwemo vyama vya siasa na Serikali ili kufikia muafaka wa kitaifa utakaosidia kupatikana kwa katiba bora. 

Mbowe aliachiwa huru Machi 4 mwaka huu na siku hiyo hiyo alikutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Dar es Salaam ambapo amesema walikubaliana kuweka msingi wa maridhiano na haki kama njia ya kufikia muafaka wa changamoto mbalimbali zilizopo ikiwemo maumivu anayodai yalitokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021.


Soma zaidi:


Chadema yajiweka pembeni kongamano la TCD

Licha ya Chadema kuwa mwanachama mwanzilishi wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimesema hakitashiriki katika kongamano la kituo hicho likalofanyika Machi 30 na 31 mwaka huu jijini Dodoma.

Kongamano hilo la haki, amani na maridhiano ambalo mgeni rasmi atakuwa Rais Samia linalenga kuwaleta pmaoja wadau mbalimbali kwenye jamii wakiwemo wanasiasa kujadili mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kuendeleza demokrasia nchini.

“Sasa kongamano la TCD tumeshauriana (Kamati Kuu), haya maridhiano yanayozungumzwa kuhusu TCD sisi hatukushiriki kuyaandaa, viongozi wetu walipokwenda kutafuta taarifa za kina na tukapitia yaliyopangwa, tumeangalia vizuri tukasema hapana!,” amesema Mbowe, makao makuu ya Chadema.

Lcha ya kuwa kongamano hilo kuwa na umuhimu mkubwa, amesema hawaoni nia njema katika kuleta maridhiano ya kweli kwa sababu wao kama chama hawakushiriki katika maandalizi yake.

“Sisi hatushiriki katika vikao vya TCD kwa sababu hatuioni nia njema ya kutibu kiu ya Watanzania kuhusu katiba,” amesisitiza Mbowe na kubainisha kuwa,  

“Siyo Mbowe, wala kiongozi yeyote wa Chadema atashirii vikao hivyo, japo nimekubali kuwa tutashiriki katika mazungumzo na kila yoyote anayehusika lakini kwa sasa hivi hatushiriki.”

Kwa mujibu wa Mbowe, msingi wa maridhiano yoyote ni kutafuta chanzo cha tatizo, kujenga mazingira ya kusameheana na kuaminiana ili kupata muafaka wa pamoja. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW