Rais Samia aligeukia Jeshi la Magereza, atoa maagizo mazito

August 29, 2022 1:37 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Amtaka kusimamia kazi ya msingi ya Magereza, kutunza, kulinda na kurekebisha wafungwa.
  • Kusimamia matumizi ya fedha na utawala bora.

Dar es salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza, Mzee Ramadhani Nyamka kuifanyia mabadiliko taasisi hiyo ikiwemo kuondoa ubadhirifu wa fedha ili ijiendeshe kwa weledi na kutimiza majukumu yake kwa ufasaha.​​​​​​​

Samia aliyekuwa akiwaapisha majaji 21 pamoja na Kamishna Jenerali  wa Magereza hii leo Agosti 29, 2022 ikulu Chamwino jijini Dodoma amesema taasisi hiyo ilikengeuka na kuacha kufanya jukumu lake la msingi ambalo ni kulinda haki  na maisha ya wanaofungwa pamoja na kurekebisha tabia zao.

“Mliacha njia ya ile kazi ya msingi ya kurekebisha tabia za hao watu lakini pia kulinda haki zao wakiwa kule, wale ni wanadamu kama wengine, wanatakiwa kupata hewa safi, mavazi, chakula kizuri, nenda kalinde haki zao,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema Jeshi la Magereza halina utawala bora na hivyo amemtaka Kamishna Nyamka kusimamia hilo kwa kuwapeleka mafunzoni baadhi ya maofisa wa jeshi hilo ili kufanya maboresho.

“Peleka watu mafunzo waende tena wakajifunze kwa sababu najua kuna wengine toka wametoka mafunzo ya uaskari Magereza mpaka leo hawajaenda mafunzo yoyote kwa hiyo la kwanza ni mafunzo ndani ya taasisi yako,” amesema Samia.

Amemtaka Kamishna huyo kuwa na utawala bora unaozingatia haki za jeshi hilo ili kuhimiza usawa.

Kufanya kazi ya msingi ya kurekebisha tabia 

Kamishna Mkuu wa Magereza Nyamka ametakiwa kusimamia kazi ya msingi ya taasisi hiyo ambayo ni kurekebisha tabia ya wanaofungwa kulingana na uhalisia wa wahusika kwani siyo wote wanaohukumiwa wanakuwa wamefanya makosa.

“Si kila anayekuja  kule ni mhalifu wa hivyo na wenyewe mnajua ndio maana mmetenga aina ya magereza, kwa hiyo nataka mkafanye urekebishaji wa tabia kuendana na hadhi zao,” amesema Rais Samia.

Samia ameongeza kuwa kutokana na magereza kutofanya jukumu lake la msingi imesababisha baadhi ya wafungwa wanaosamehewa kufanya makosa ya makusudi ili warejee gerezani kwani wanakuwa hawajafundishwa nini cha kufanya wakiwa huru.


Soma zaidi:


Kusimamia matumizi ya fedha

Kutokana na Jeshi la Magereza Kujikita katika shughuli za biashara kutokana na ufinyu wa bajeti Rais Samia amesema hivi sasa Jeshi hilo limeongezewa fedha katika bajeti ya 2022/23 hivyo amemtaka Kamishna Jenerali kusimamia matumizi ya fedha.

“Moja ya makosa ya ndani ya taasisi yako ni kutokufuata sheria kwenye matumizi ya fedha. Nenda kasimamie matumizi ya fedha na uhakikishe fedha hizi zinakwenda katika magereza yote  kwenda kutoa huduma kwa hawa watu,” amesema Rais.

Kamishna Jenerali Nyamka aliyeapishwa leo anachukua nafasi ya Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Kabla ya nafasi hiyo Nyamka alikuwa Kaimu Kamishna wa Magereza Huduma za Urekebu ambapo taarifa ya uteuzi wake ilitolewa Agosti 26, 2022 huku uteuzi huo ukianza Agosti 24, 2022.

Mapema mwezi Julai Rais Samia alisema anataka kufanyia marekebisho muundo wa haki jinai kutokana na kuwepo kwa malalamiko kadhaa yaliyosababishwa na utendaji kazi usio wa kurishisha katika taasisi za haki jinai ikiwemo Jeshi la Magereza.

Hatua hiyo ya kumteua Nyamka inaweza kuwa ni mwendelezo wa mabadiliko hayo katika taasisi za vyombo vya dola.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW