Rais Samia: Majaji tokeni nje mkajifunze

August 29, 2022 10:26 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema wakitoka watapata maarifa mapya na kubadilishana uzoefu.
  • Asema hajawahi kukataa maombi ya majaji kwenda kujifunza.
  • Kuendelea kuteua majaji wanawake wengi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka majaji wa Mahakama Kuu na Rufani kuendelea kushiriki mafunzo na warsha mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuboresha utendaji wa mahakama Tanzania.

Rais Samia aliyekuwa akiwaapisha Majaji na Kamishna wa Magereza leo Agosti 29, 2022 Ikulu Chamwino jijini Dodoma amesema ataendelea kutoa ruhusa kwa majaji kwenda kwenye mafunzo ili mhimili wa mahakama ufanye kazi vema.

“Sijawahi kukataa maombi ya majaji na nitaendelea kufanya hivyo, lengo langu mkajifunze mhimili wa mahakama usimame na muachane na yale yaliyokuwa historia huko nyuma. Mahakama nyuma hazikuwa zikisemwa vizuri,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema kupitia mikutano ya ndani au nje ya Afrika inawapa majaji  fursa ya kubadilishana mawazo na watu wengine  jambo litakalosaidia kujifunza mbinu mpya na kuepuka makosa yaliyokuwa yanafanyika awali.

Jumla ya majaji 21 wameapishwa hii leo, tisa ni wa Mahakama ya Rufani huku Majaji 13 wakiwa ni wa Mahakama Kuu. Majaji hao 21 ni kati ya 22 walioteuliwa na Rais Samia hivi karibuni.

Pamoja na kuwataka majaji hao kufanya kazi kwa uadilifu, unyenyekevu na weledi, Rais Samia amesema ataendelea kushirikiana na mhimili wa mahakama ikiwa ni pamoja na kuongeza watendaji pale hali ya kifedha itakaporuhusu.

“Nilitakiwa kuteua majaji 47, lakini kwa nafasi ya hali ya uchumi nikasema niteue kwanza majaji 22 kwa sababu majaji mnajijua mambo yenu sio madogo, ukiitwa tu Jaji yanayofuata hapo, sasa kwenye wage bill na yale matumizi ya serikali mzigo ungenielemea,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema katika kuimarisha utendaji kazi wa mahakama atateua majaji wanawake zaidi ili kufikia uwiano wa 50 kwa 50 kwani majaji wanawake wameonekana kutimiza wajibu wao kwa weledi zaidi na kuchangia idadi ya malalamiko kwa mahakama kupungua.


Soma zaidi:


“Majaji wanawake wanakuwa waadilifu zaidi, dhambi ambazo utazishika kwa majaji wanaume huzikuti kwa majaji wanawake, lakini anahukumu kwa moyo pamoja na kufuata sheria, mila, desturi na mambo mengine ya Tanzania wako vizuri,” amesema Rais.

Majaji hao 22 walioteuliwa wanamfanya Rais Samia kufikisha jumla ya majaji 52 aliowateua tangu aliposhika madaraka mwezi Machi mwaka 2022 ambapo kati yao majaji tisa ni wa Mahakama ya Rufani na 43 ni wa Mahakama Kuu.

Kuongezeka kwa idadi ya majaji kutasaidia kuongeza ufanisi wa mahakama kutoa haki kwa wananchi kwa sababu kesi zitashughulikiwa kwa wakati.

Kwa Mujibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, jaji mmoja alikuwa na wastani wa mashauri 340 na hivi sasa jaji mmoja atakuwa na wastani wa mashauri 265 kwa mwaka.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW