Rais Samia awaapisha Sirro, Wambura akitaka maboresho polisi

July 20, 2022 2:39 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Taarifa ya uteuzi wa IGP mpya Wambura yatolewa usiku wa manane.
  • Sirro sasa kuwa balozi nchini Zimbabwe. 
  • Wambura sasa kuwa IGP wa 11 Tanzania.

Dar es Salaam. Baada ya kuhudumu kwa miaka mitano akiwa bosi wa juu kabisa wa jeshi la Polisi Tanzania, safari ya Simon Sirro katika nafasi hiyo imefikia tamati huku Rais Samia Suluhu Hassan akipanga kufanya maboresho zaidi katika taasisi za haki jamii ikiwemo polisi. 

Hitimisho la safari ya Sirro katika nafasi hiyo limekuja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumpandisha cheo Camilius Wambura kuwa Inspekta Jenerali na kumteua kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wa 11. 

Katika uteuzi uliotangazwa usiku wa manane na Ikulu, Sirro sasa atakuwa balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe na tayari ameapa leo (Julai 20, 2022) kuitumikia nafasi hiyo katika taifa hilo la kusini mwa Afrika. 

Sirro aliteuliwa na hayati Rais John Magufuli Mei 28, 2017 kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania baada ya kupandishwa cheo kutoka Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.


Rais Samia Suluhu Hassan akimvalisha beji ya cheo kipya Inspekta Jenerali, Camillius Wambura jijini Dodoma leo. Picha|Ikulu. 


Sirro alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Ernest Mangu ambaye alipangiwa majukumu mengine.

Kiongozi huyo ni miongoni mwa vigogo wa polisi walio mbioni kustaafu kazi kutoka katika jeshi hilo baada ya mwaka jana kueleza kuwa anakaribia kuhitimisha utumishi wake.

“Sisi ambao tunakaribia kustaafu tunajua hawa ndio wangeendesha jeshi…naamini wale mliobaki mnajifunza sasa,” alisema Sirro, alipokuwa akitoa  hotuba ya kuaga miili ya askari waliouawa kwa kupigwa risasi na mtu aliyefahamika kwa jina la Hamza jijini Dar es Salaam Agosti 2021.

Katika uongozi wake wa miaka mitano, Sirro alikabiliana na changamoto kadhaa za kiusalama ikiwemo mauaji ya askari na raia na watu wasiojulikana katika maeneo ya Kibiti na Rufiji, matishio ya ugaidi mkoani Mtwara na kutekwa kwa Bilionea Mo Dewji.

Katika kipindi hicho Sirro amekuwa akikosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu na vyama vya siasa kwa kuminya haki za binadamu ikiwemo kuzuia mikutano ya kisiasa licha ya kuwa ni haki ya kikatiba. Serikali imekana tuhuma za kuminya haki za binadamu. 

Katika mabadiliko yaliyohusisha uteuzi wa Wambura, Rais Samia ameonekana akilenga kufanya mabadiliko makubwa ndani ya jeshi la polisi kwa  kuwateua na kuwahamisha baadhi ya vigogo wa jeshi hilo. 

Rais Samia amemteua Kamishna wa Polisi (CP) Liberati Sabas kuwa Kamishna wa Fedha na Logistiki kutoka kuwa Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa jeshi hilo. 


Soma zaidi:


Viongozi wengine walio badilishwa ndani ya jeshi hilo ni Kamishna wa Polisi (CP) Hamad Khamis Hamad aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa polisi Zanzibar na  Awadh Juma Haji ambaye anachukua nafasi ya Sabas. 

Katika hotuba yake leo, Rais Samia amesema amepanga kufanya maboresho kwenye taasisi za haki jamii ikiwemo polisi ili kuimarisha utendaji kazi. 

“Suala la haki za watu na haki za nchi linapaswa kupewa kipaumbele kikubwa na kwa maana hiyo nimeamua tufanye maboresho kwenye taasisi za haki jamii,” amesema Rais Samia.

Taasisi za haki jamii zinazotarajiwa kufanyiwa maboresho ni pamoja na jeshi la polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru),Jeshi la Magereza na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za kulevya.

Maboresho hayo, kwa mujibu wa Rais, yatagusa nyanja mbalimbali ikiwemo miundo ya taasisi, mifumo ya ajira, mafunzo maadili na nidhamu, mifumo ya utendaji kazi, upandishaji vyeo vya taaluma na vyeo vya madaraka pamoja  na mahusiano ya taasisi na raia.

“Tumesema tunafungua nchi, tumeifungua na wageni wanaingia wengi lakini malalamiko tunayoyapata kwa  wageni ni mengi kwa hiyo tunakwenda kuangalia haya mambo yapoje,” ameongeza Rais Samia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW