Saa 24 za kummaliza rafiki aliyegeuka kuwa adui

September 24, 2021 10:51 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni filamu ya Kate, inayomhusu binti mwenye kiu ya kisasi.
  • Aliyetegemea ni msaada ndiye anayegeuka adui mkubwa.
  • Ana saa 24 tu kummaliza adui yake.

Dar es salaam. Kuna fumbo ambalo wanadamu tumeumbiwa. Ni lile la kutokujua lini pumzi uliyopewa na muumba wako itarudi ilikotoka. 

Hilo linatupatia wanadamu uhakika wa “sasa hivi tu” kwenye maisha na kutuacha tukiwa bila ufahamu wa kama sekunde mbili zijazo tutakuwa hai. 

Hata hivyo, ikitokea mtu amekuambia kuwa una saa 24 tu za kuishi, utafanyaje?

Bila shaka utatamani, utimize kila kitu ambacho ulitamani ukifanye, kama hujawahi tembelea sehemu basi, utatumia hayo masaa walau kuuridhisha moyo wako. 

Binafsi ningelikwea pipa na kwenda Korea huko kukutana na waigizaji ninaowapenda na kwa kuwa ni bachela, ningelinunua hata shela nivae kuona jinsi mabibi harusi hujihisi.

Lakini leo, hainihusu mimi. Inamhusu mwanamama Kate ambaye akiwa kwenye kilele cha kutaka kutimiza ndoto zake za kibabe, daktari ana uvunja moyo wake kwa kumwambia ana saa 24 kama siyo 15 tu za kuishi.

Filamu ya Kate inamhusu mwanadada ambaye hajawahi kufaidi mapenzi ya baba na mama, kwani waliomleta duniani walifariki akiwa bado ni mtoto.

Wahenga walisema Mungu si Athumani na kweli walimaanisha. Baada ya wazazi wake kuaga dunia, Kate alipata msamaria wa kumlea. Ni Varrick ambaye alifanikiwa kumsahaulisha Kate uyatima alioachwa nao.

Mapenzi ya baba kwa bintiye yaliyomfanya Kate ahisi dunia nzima imeumbwa kwa aili yake. Alimuona Varrick kama malaika aliyeshushwa mbinguni kumsahaulisha shida zote.

Sidhani kama nilikwambia kuwa wazazi wa kibayolojia wa Kate hawakufa kifo cha kawaida kama nilisahau basi ndiyo nakuambia hivyo, waliuwawa. 

Sijui ni bahati nzuri au mbaya kwani Varrick anamuandaa Kate kulipiza kisasi kwa wote walioshiriki kumwaga damu ya baba na mama yake.

Kate (pichani) anapitia mafunzo ya jasho na damu na kuwa mlengaji shabaha matata. Picha| Forbes Alert.

Mafunzo ya damu na jasho anayopitishwa Kate si kitu kwa kiu aliyonayo juu ya kisasi chake. Mwanadada huyo anavumilia yote ilimradi tu atimize haja ya moyo wake.

Niseme nini Herimina mimi? Labda nikupe methali ya Kitanda hakizai haramu kwani mafunzo hayo yanamfanya Kate kuwa mpiganaji aliyeiva haswa kwani kutumia bunduki kwake ni kama kushika mwiko tu.

Kate anakuwa mlengaji wa hatari wa shabaha na kwa kiwango hicho, wacha tumwite sniper.

 “Kikulacho ki nguoni mwako” 

Siku zote Kate ameishi kwa kinyongo sana akitamani kumpata mbaya aliyeteketeza maisha ya wazazi wake.

Huku msaada anaoupata kutoka kwa Varrick, unamfanya kuamini kuwa ana mtu muhimu wa kumsaidia katika safari hiyo.

Varrick amekua akimpa maelekezo Kate ya kwenda kuwaangamiza maadui anaodai kuwa ndiyo walihusika katika kifo cha wazazi wake, na Kate amekuwa akiitumia nafasi hiyo vyema kwani alihakikisha anamaliza kila kiumbe anachoambiwa ni adui.

Cha ajabu maadui hao wamekuwa hawaishi kila uchao. Leo huyu, kesho yule utasema wazazi wa Kate waliuliwa na dunia nzima.

Wahenga hawakukosea waliposema kikulacho ki nguoni mwako, kwani adui mkubwa wa Kate ni huyo anayemwamini na kumpa maelekezo ya kwenda kuteketeza watu wengine. 

Muda wote huo,  amekuwa akiishi chini ya pua yake na Kate, amekuwa kibaraka wake.

                       

Bila shaka umeshtuka, na kwa wale waliowahi kusalitiwa na watu wanaowaamini basi maumivu yake wanayajua.

Kiufupi ni kwamba Varrick alikuwa akimtumia Kate kwenye masula yake, na watu ambao amekuwa akimchochea Kate akawaue ni wahasimu wake kwenye mambo yake binafsi.

Vuta picha ungekuwa wewe ungefanyaje, na ukizingatia kuwa umeshamwaga damu za kutosha za watu wasio na hatia. 

Kinachoumiza zaidi ni kwamba Varrick hakuishia tu kumtumia Kate, bali alienda mbali na kumuwekea sumu, inayomfanya binti huyo kuoza taratibu huku bado anapumua.

Habari zinazo badilisha maisha ya kate

Wakati Kate akiwa na kibarua kizito cha kumteketeza adui yake, daktari anamwambia hana saa nyingi za kuendelea kuliona jua.

Ukizingatia kuwa ametumia maisha yake yote akiua, akinyonga, akiumia na kuteswa na kisasi, hata ungekuwa wewe ungeona umeyachezea maisha yako.

Moyo wake unapasuka kwa hasira, lakini taarifa za daktari hazimfanyi aache kumalizia mkia wa n’gombe aliyekuwa ameanza kumla.

Niseme tu kwamba kuna mengi sijakusimulia kuhusu filamu hii kwa sababu sitaki kuwa rufufu wako, lakini nihakikishe kuwa utakosa mengi usipoitazama filamu ya Kate, kwani imejaa mkasa wa kusisimua unaosindikizwa na visa mbalimbali vitakavyokufanya ufurahie ulimwengu wa filamu.

Unaweza kuitazama filamu hii kwenye app ya Netflix kama umelipia kifurushi chako na kukuibia siri, au kuazima kwa jirani yako.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW