Filamu ya King’s Affection: Majukumu yanavyobadilisha jinsia
- Filamu inamuhusu binti wa kifalme anayebadilika na kuishi kama mwanaume baada ya kaka yake kupoteza maisha.
SIKILIZA HAPA UCHAMBUZI WA FILAMU HII
Dar es Salaam. Filamu hii inaturudisha nyuma enzi hizo wakati nchi ya Joeson haijaitwa Korea. Katika kipindi hicho, Mwana mfalme mteule au “crown prince” Anatarajia mtoto ambaye atakuja kurithi kiti cha enzi kama mfalme wa Joeson.
“Crown princess” ama unaweza kumwita kipenzi cha nchi hiyo anafanikiwa kujifungua salama na kwa bumbuwazi, anajifungua watoto mapacha. Mmoja wa kike na mwingine wakiume.
Huenda upo kwenye moment za “waaoow” lakini katika kipindi hicho, kujifungua watoto mapacha haikuwa bahati au baraka kama inavyochukuliwa saizi.
Ilikuwa ni laana tena uliyotibiwa kwa njia za machungu. Ililazimu kati ya mapacha wawili, mmoja auwawe.
Kati ya mapacha hao, nani atakufa? Bila shaka ni wa kike, kwani kwa miaka hiyo mtoto wa kiume alikuwa anathaminiwa zaidi na ikizingatiwa kuwa ndiye atakaekuja kurithi kiti cha ufalme.
Kwa kuujua uhalisia, chozi linamtoka crown princess akimtazama binti yake kichanga, ambaye anatoa tabasamu pana baada ya kuliona jua bila ya kujua ana masaa machache tu kuishi.
Wahenga walisema uchungu wa mwana aujuwaye ni mzazi na kwa muktadha huu, ninamaanisha mama. Haikuwa raisi kwa mama kuona kichanga ambacho amekileta duniani kwa tabu kiuwawe kikatili kiasi kile.
Usiku wakati kila mtu amelala, anamtorosha mwanae ambapo anampeleka nje ya ikulu ya kifalme.
Na hapo ndio mwanzo wa maisha tofauti kati ya mapacha hawa. Watoto ambao dunia iliwaandikia kuishi maisha ya hadhi ya kifalme lakini walimwengu wakaamua kuwatenganisha.
Wakati mtoto wa kiume, Lee hwi akiishi kwenye hekalu, mtoto wa kike Dami anabaki akiishi maisha ya mtumwa.
Pale moyo unaposhindwa kujizuia, swali linabaki kama madaraka ni muhimu kuliko huba. Picha Showbiz Cheat Sheet.
Maisha mapya ya Dami
Baada ya miaka michache kupita Lee ambaye alikuwa anatarajia kuwa crown prince anapoteza maisha huku sababu ya kifo chake ikijawa sintofahamu.
Mama yake ambaye sasa ni malkia anafanya maamuzi magumu ya kuficha habari juu ya kifo cha mwanae huyo, na badala yake anaamua kumtafuta Dami ili achukue nafasi ya kaka yake.
Unaweza kuhisi malkia huyu amerukwa na akili, la hasha alifanya hivyo kulinda nafasi ya Lee ambayo ilikuwa ikimendewa na maadui wengi akiwemo mjomba wa mapacha hao.
Baada ya kuchukua nafasi ya kaka yake, Dami anaanza kuishi kama mtoto wa kiume, kuanzia mavazi, kutembea hadi kuongea. Na ili kuitunza siri yake anaishi maisha ya kujitenga bila kuwa na rafiki yeyote.
Ukurasa huu mpya wa maisha unakuwa ni mgumu kwa Dami, kwani vikwazo vyote anavivumilia, lakini changamoto inakuja pale ambapo inabidi azuie moyo wake kupenda kwani inaweza kuleta utata na kujulikana kwa siri yake.
Hata hivyo, “moyo mashine” bwana. Binti huyu ambaye ni crown prince sasa uvumilivu wake unagonga mwamba anapokutana na kijana Jung Ji Woon ambaye anafanikiwa kuteka hisia zake. Na hapo ndipo uhondo wa filamu hii unapoanza.
Unahisi ni nini kitaendelea katika maisha ya Dami? Je siri yake ambayo hata mfalme haifahamu itafanikiwa kutokuvunjika na vipi kuhusu hisia zake kwa Jung?
Fuatilia filamu ya King’s affection ili ufahamu mbichi na mbivu za kisa hiki cha kusisimua.
Latest
