Filamu: Wafahamu madereva wa kudumu wa maisha yako
Arusha. Umewahi kuamka asubuhi ukajikuta na furaha na baada ya muda ikawa imetoweka? Vivyo hivyo kadri siku zinavyoenda, hisia zako zikawa hazieleweki. Mara hasira, mara upendo na muda mwingine kuhisi ya kuwa hauna haja ya kujali yaani, liwalo na liwe?
Leo katika ulimwengu wa filamu, ni kana kwamba hisia zako zina dereva zaidi ya mmoja. Madereva hao wanahusika na kuendesha siku yako ni pamoja na furaha, hasira, hofu, huzuni na kinyaa.
Kama bado haujafahamu naongelea filamu gani, wacha niweke ukomo kwenye mchezo wako wa bahati nasibu. Ninazungumzia filamu ya “Inside Out” sehemu ya pili ambayo inamuongelea binti Riley katika hatua za ukuaji wake.
Sehemu ya kwanza ya filamu hii ilituacha na mafunzo ya kuwa ni muhimu kuzingatia hisia zote kwani ndizo zinazotufanya tuwe tulivyo.
Furaha ina nafasi yake katika kutuonyesha umuhimu wa watu na matukio yanayotuzunguka. Hofu ina nafasi yake katika kutulinda na hatari na hata kujali hisia za wengine. Pia huzuni inatufanya tujue hisia zetu ni nzito kiasi gani.
Hodi hodi wenyeji, ni zamu ya wageni
Riley anaingia kwenye umri wa balehe yaani anatimiza miaka 13 na ndipo mwili wake unahitaji madereva wapya.
Kwenye kichwa cha Riley, wageni wanapiga hodi kuchukua nafasi zao kwenye hisia zake nao ni, wasiwasi, wivu, aibu, uchovu na kumbukizi za zamani. Ujio wao, ni kengele ya mashaka kwa madereva wa zamani kwani kila mtu anahitaji nafasi ya kushika uskani katika maisha ya Riley.
Hata hivyo, dereva mkuu ambaye ni furaha bado hajajua kuwa nafasi yake inanyemelewa na siku inapowadia, kiti chake cha enzi kinapata mkaaji mpya.
Hisia gani zitamtawala Riley ikiwa furaha siyo hisia kuu? Mapinduzi hayo yameziteka hisia zote za zamani na Riley ni msichana mpya kiasi cha kuwa rafiki zake wanajiuliza kama ndio mtu waliyempenda na kumthamini awali.
Fuatilia kisa hiki cha “Inside Out” na kama wewe ni mjomba au shangazi, ni vyema ukahakikisha unaangalia na wapwa zako ama watoto wako kwani wana mengi ya kujifunza kutokana na maudhui haya. Filamu hii inapatikana katika majukwaa ya mtandaoni.
Unapenda filamu? Usikose kutufuatilia kila ijumaa kwa ajili ya mapendekezo ya filamu za kutazama kwenye wikiendi yako.