Mfumo wa kidijitali utakavyorahisisha usajili, malipo wanafunzi elimu ya juu

January 10, 2022 7:39 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mfumo wa kidijitali wa malipo ya fedha za mikopo ambao utawawezesha kupokea fedha ndani ya saa 24.
  • Utaondoa usumbufu wa kutunza kumbukumbu kwenye makaratasi.
  • Usajili wa wanafuzi wanufaika unaanza leo Januari 10, 2022.

Dar es Salaam. Huenda mchakato wa kusajili na kuwalipa fedha wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ukarahisishwa baada ya Serikali kuanzisha mfumo wa usajili mtandaoni utakaowawezesha kupata fedha ndani ya muda mfupi.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inatarajia kuanza kuwasajili wanafunzi 70,396 wanufaika wa mikopo wa mwaka wa kwanza katika mfumo wa kidigitali wa malipo ya fedha za mikopo ambao utawawezesha kupokea fedha ndani ya saa 24.

Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo HESLB, Dk Veronica Nyahende aliyekuwa akizungumza jana Januari 10, 2022 jijini Dar es Salaam amesema kuwa usajili huo utajumuisha kuchukuliwa kwa alama za vidole, taarifa za kibenki, picha pamoja na taarifa za usajili wa wanafunzi vyuoni.

Usajili huo utafanyika katika taasisi za elimu ya juu nchini kuanzia leo Januari 10 hadi Februari 3 mwaka huu.

“Mfumo huu unaitwa ‘Digital Disbursement Solution’ maarufu kama DiDiS na tuliuanzisha mwaka 2018 ili kurahisisha fedha kuwafikia wanafunzi kutoka siku 10 hadi saa 24 hivi sasa,” amesema Dk Nyahende.

Aidha, amewakumbusha wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza ambao ni wanufaika wa mikopo na wengine ambao wamepata mikopo kwa mara ya kwanza mwaka 2021/22 kujitokeza ili kusajiliwa. 

“Malipo yote ya robo ya tatu kwa mwaka huu wa masomo yatafanyika kupitia mfumo huu, kwa hiyo ni muhimu kwa wanafunzi kujisajili ili wapokee malipo yao,” ameongeza Dk Nyahende.


Soma zaidi:


Maafisa wa HESLB watakuwa vyuoni kuanzia leo ili kushirikiana na maafisa wa vyuo katika kazi ya usajili na taarifa za ziada kuhusu maeneo na muda wa usajili yatatolewa katika ofisi za maafisa mikopo wa vyuo husika.

Viongozi wa serikali za wanafunzi na maafisa mikopo katika vyuo wametakiwa kuwahamasiha wanafunzi wanufaika kujitokeza ili kujiandaa kupokea fedha za malipo ya mikopo bila usumbufu.

“Usajili huu ukifanikiwa, maafisa mikopo wataondokana na usumbufu wa kutunza kumbukumbu kwa karatasi na wanafunzi watakuwa wanapokea fedha haraka na hivyo kutumia muda mwingi kusoma,” amesisitiza Dk Nyahende.

Katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imetenga Sh570 bilioni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na zinazowanufaisha jumla ya wanafunzi 168,000.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW