Matumizi ya ndani ya Dola ya Marekani yanavyoweza kuathiri uchumi wa Tanzania
- Matumizi yakizidi hudhoofisha nguvu ya ununuzi kwa shilingi na kuchochea mfumuko wa bei katika uchumi wa nchi.
Dar es Salaam. Licha ya jitihada za Serikali kuimarisha Shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu za kigeni, ikiwemo Dola ya Marekani, baadhi ya wafanyabiashara na watoa huduma wameendelea kutumia fedha hizo za kigeni katika miamala ya ndani suala linaloathiri uchumi wa Tanzania.
Mwenendo huo uliibua mjadala mpana bungeni Dodoma wakati wa maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu wa Tanzania Dk Mwigulu Nchemba aliyetakiwa kufafanua maeneo ambayo fedha hizo zinapaswa kutumika ili kunusuru uchumi wa nchi.
“Tumetoa maeneo ambayo yanaweza yakatumia sarafu ya nje kwa mfano katika maeneo ambayo yanafanyika mauzo ya nje ya bidhaa, huduma na vitu vinavyo husiana na hivyo na baadhi ya taasisi ambazo zinafanya manunuzi makubwa ya bidhaa, tumebainisha na taasisi hizo zimekwisha julishwa,” amesema Dk Mwigulu Juni 25, 2026 alipokuwa akijibu swali la Suma Fyandomo, Mbunge wa viti maalum CCM.
Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197 [R.E. 2023] Shilingi ya Tanzania ndiyo sarafu pekee inayotambulika kisheria kwa matumizi ya miamala ya ndani.
Aidha, Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za Mwaka 2025 zinaruhusu matumizi ya fedha za kigeni katika mazingira maalumu pekee, ikiwemo michango ya uanachama inayolipwa na Serikali kwa taasisi za kikanda zilizopo nchini, miamala inayohusisha balozi na mashirika ya kimataifa yaliyopo Tanzania, mikopo ya fedha za kigeni inayotolewa na benki za biashara na taasisi za fedha, pamoja na malipo ya bidhaa katika maduka yasiyotoza ushuru (duty-free shops).
Kwanini Dola ya Marekani inaendelea kutumika?
Mtaalamu wa uchumi na fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo ameiambia Nukta Habari kuwa matumizi ya dola katika baadhi ya miamala ya ndani yanachochewa na jitihada za wafanyabiashara kutafuta sarafu iliyo tulivu zaidi ili kujikinga dhidi ya hasara zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya thamani ya fedha pamoja na mfumuko wa bei.
Profesa Kinyondo ameeleza kuwa wafanyabiashara wengi hususan wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, hununua bidhaa hizo kwa dola hivyo kuuza bidhaa zao kwa sarafu nyingine huwaweka katika hatari ya hasara endapo kutakuwa na mabadiliko makubwa ya viwango vya ubadilishaji wa fedha.
“Wapo wanaotaka kulipwa moja kwa moja kwa Dola za Marekani, na wapo ambao huweka bei kwa dola lakini wanapokea malipo kwa Shilingi ya Tanzania kulingana na thamani ya siku husika.
Hivyo, bidhaa inaweza kuwa ileile, lakini mtu anayelipa leo na anayelipa siku nyingine anaweza kukutana na bei tofauti kutokana na mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji wa fedha,” amefafanua Profesa Kinyondo.
Inaathiri vipi uchumi ?
Akifafanua zaidi kuhusu athari za matumizi ya sarafu za kigeni katika uchumi wa ndani, Profesa Kinyondo amesema hali hiyo ina mchango mkubwa katika mwenendo wa thamani ya fedha na mfumuko wa bei nchini.
Ongezeko la matumizi ya dola katika miamala ya ndani linaweza kuongeza uhitaji wa sarafu hiyo katika soko, jambo ambalo huweza kupandisha thamani yake zaidi.
Hali kama hiyo inapotokea hudhoofisha nguvu ya ununuzi ya wananchi kwa shilingi na kuchochea mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma, hatimaye kuathiri mwenendo wa mfumuko wa bei katika uchumi wa nchi.
“Bidhaa ikihitajika kwa wingi duniani thamani yake inapanda, kwahiyo kama kila mahali tutatumia dola kununua bidhaa mana yake uhitaji wa dola utakuwa mkubwa na thamani yake itapanda na ikipanda kinyume chake shilingi itaporomoka na kadiri inavyoporomoka yanakuja mambo mengi ikiwemo mfumuko wa bei,” amesema Profesa Kinyondo.
‘Serikali ichukue hatua’
Ili kutatua changamoto hiyo Profesa Kinyondo amesema ni vyema Serikali ikaongeza udhibiti ikiwemo kuchukua hatua za wazi za kisheria kuhakikisha sheria zinazolinda matumizi ya Shilingi ya Tanzania zinatekelezwa kikamilifu.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuimarisha uhamasishaji wa matumizi ya sarafu ya taifa katika sekta zote, ikiwemo kuhakikisha taasisi zake za umma zinaacha kutumia fedha za kigeni katika miamala ya ndani.
“Serikali inasema tusitumie dola, lakini hatujawahi kusikia kuna mtu kakamatwa…Hata kuna taasisi nyingi za Serikali ambazo na zenyewe zinatumia dola kalita miamala yake..hasa zilizopo kwenye maliasili, vyuo vya Serikali…huwezi ukakataza matumizi ya dola wakati wewe mwenyewe unatumia,” amesema Profesa Kinyondo.