Dirisha la rufaa maombi ya mikopo HESLB kufunguliwa Novemba 8, 2023

November 3, 2023 6:30 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kukamilika kwa awamu tatu ambapo wanufaika 73,078 wamepangiwa mikopo.
  • Wanafunzi wa stashahada kupangiwa mikopo yao Novemba 9, 2023.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imebainisha kuwa iko mbioni kufungua dirisha la maombi ya rufaa kwa wanafunzi ambao hawakupangiwa mikopo katika awamu zote tatu au ambao hawakuridhishwa na kiwango walichopangiwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na HESLB, Novemba 2, 2023 dirisha hilo litakuwa wazi kuanzia Novemba 8, 2023.

Serikali ilitenga Sh731 bilioni kwa ajili ya  wanafunzi 220,376 kwa mwaka wa masomo 2023/2024. Kati yao wanafunzi 75,000 wanatarajiwa kuwa ni wanufaika wa mwaka wa kwanza baada ya kukamilishwa kwa uchambuzi wa maombi ya rufaa yatakayowasilishwa. 


Soma zaidi : Mapato yasiyokusanywa Serikali za mitaa yaongezeka kwa asilimia 61.7


Mpaka Novemba 2, 2023 Idadi ya wanafunzi wapya waliopangiwa mikopo ilifikia  73,078 baada ya kutangazwa kwa awamu ya tatu ya wanufaika 2,518 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya Sh 6.9 bilioni.

Awali wanafunzi 56,132 wa shahada ya kwanza walipangiwa mikopo yenye thamani ya Sh 159.7 bilioni katika awamu ya Kwanza iliyotangazwa Ijumaa, Oktoba 20, 2023 ikifuatiwa na awamu ya pili iliyokuwa na wanafunzi 14,428 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya Sh 44.2 bilioni iliyotangazwa Ijumaa, Oktoba 27, 2023.

Kati ya wanafunzi 73,078 waliopangiwa mikopo katika awamu tatu, wanafunzi wa kiume ni 42,386 (asilimia 57) na wa kike ni 30,692 (asilimia 42.6).

 

Aidha, waombaji wote wa mkopo wametakiwa kutembelea akaunti mtandao walizotumia kuomba mkopo zinazojulikana kama ‘SIPA’ ili kupata taarifa muhimu kuhusu mkopo wake.

Mikopo kwa Stashahada

Aidha, wanafunzi wa ngazi ya stashahada walioomba mikopo ya elimu mwaka 2023/24 wametakiwa kuendelea kuwa wavumilivu kwa  kuwa uchambuzi wa maombi yao unakamilishwa na orodha ya waliopangiwa mikopo kwa mwaka 2023/2024 itatangazwa Alhamisi, Novemba 9, 2023.


Soma zaidi : ‘Betting’, vinywaji baridi kuchangia bima ya afya kwa wote Tanzania


Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW