Kutapika damu, goita vinavyowatesa wananchi Ukerewe

January 22, 2022 6:02 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Madaktari wabaini magonjwa hayo yanawasumbua watu wengi wilayani humo.
  • Sababu kubwa ni kutumia maji machafu.
  • Utafiti zaidi kufanyika kutafuta suluhu ya kudumu.

Mwanza. Wakazi wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wameiomba Serikali kufanya utafiti wa sababu za kuongezeka kwa ugonjwa wa goita unaowatesa zaidi wanawake na kutapika damu ambayo yamekuwa tishio kwa wakazi wilayani humo.

Ombi hilo limetolewa baada Taasisi ya kidini ya  Al Jazeerakwa kushirikiana na shirika la Peleks la nchini Saudi Arabia ambalo lilipiga kambi wilayani hapo kutoa matibabu ya upasuaji  wa magonjwa na huduma zingine za ushauri bure na kubaini kuwepo kwa wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na magonjwa hayo.

Akizungumza baada ya kufanyiwa upasuaji, Angelina Ndema amesema amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa goita  kwa muda wa miaka 12 na hakuweza kupata matibabu kutokana na gharama kuwa juu.

“Nilianza kuugua ugonjwa huu miaka 12 iliyopita, nilikuwa napata maumivu makali kwenye uti wa mgongo, napumua kwa shida, kichwa kuuma na wakati mwingine kulala kwa shida, lakini toka juzi nilipofanyiwa upasuaji nimepata nafuu,” amesema Angelina.

Amesema mwaka 2005 alifika Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza kufanyiwa upasuaji lakini alishindwa kutokana na gharama kuwa kubwa.

Ameiomba Serikali kufanya uchunguzi kubaini sababu za kuwepo kwa ugonjwa huo na kutoa suluhisho la kudumu.


Zinazohusiana:


Uchunguzi wa awali

Daktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji, Makame Omary amesema katika kipindi cha siku saba zilizopita watu 50 katika wilaya hiyo wamefanyiwa upasuaji wa magonjwa ya goita, uvimbe kwenye kizazi na mfuko wa uzazi huku wengine 200 wakitibiwa magonjwa ya ndani.

“Ugonjwa wa tezi la shingo (goita) inaonekana kushika kasi kwa wilaya ya Ukerewe na sababu kubwa ya ugonjwa huo ni upungufu wa madini joto mwilini,” amesema Dk Omary.

Ametaja ugonjwa wa goita kuwashika zaidi wanawake na kubainisha madhara yanayowakumba ni pamoja na kuziba kwa njia ya hewa na chakula na wakati mwingine husababisha ugonjwa wa saratani. 

Gharama za kufanyiwa upasuaji wa ugonjwa huo si chini ya Sh1.5milioni  hadi  Sh2 milioni.

Mratibu wa zoezi hilo, Ismail Makumbo ameeleza lengo la kuwaleta madaktari hao kuwa ni kuwasaidia wakazi wa wilaya ya Ukerewe ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za kufanyiwa upasuaji.

Amesema katika kambi hiyo walikusudia kuwafikia wananchi 1,000 kuwapatia matibabu na kwamba hadi zoezi linafungwa tayari watu 200 walikuwa wamefikiwa.

“Idadi hiyo ni kubwa kutokana na Wilaya ya Ukerewe kuzungukwa na maji hivyo wengi walishindwa kufika, mpango uliopo ndani ya miezi mwili ijayo timu hii ya madaktari watarejea kwa ajili ya kutoa huduma hiyo lakini pia kufanya utafiti wa kuwepo kwa magonjwa hayo,” amesema Makumbo.

Amesema madaktari bingwa waliopiga kambi katika kisiwa hicho watano wametoka Saudi Arabia na wawili ni kutoka Zanzibar.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, Dk Flora Chacha amekiri kuwepo kwa magonjwa hayo na kwamba kwa siku hospitali hiyo inapokea wagonjwa watatu hadi wanne.

Amesema wagonjwa wenye tatizo la goita na mifuko ya uzazi hupewa rufaa kwenda hospitali ya Bugando kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

 “Kwa siku tunapokea wagonjwa watatu hadi wanne wanaotapika damu na kuvimba matumbo, na hii inasababishwa na wengi kutumia maji yenye vimelea vya vichocho na wengine kuogelea kwenye maji hayo,” amesema Dk Chacha.

Ameeleza njia wanazozifanya katika kuwasaidia wananchi wa  kisiwa hicho kuwa ni pamoja na kutoa dawa kila baada ya miezi mitatu kwa wanafunzi wote shuleni, kampeni ambayo inafanywa na wataalam wa afya kutoka Bugando.

Habari hii imeandikwa na Mariam John

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW