Mwaka mpya wa fedha waanza na maumivu kwa wamiliki vyombo vya moto

July 6, 2022 1:49 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link


  • Ni baada ya kupanda kwa bei za petroli na dizeli kwa viwango tofauti.
  • Wakazi wa Kyerwa mkaoni Kagera kununua petroli kwa Sh3,458.
  • Serikali yatoa ruzuku ya Sh100 bilioni kupunguza makali.

Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto yakiwemo magari wameanza mwaka mpya wa fedha wa 2022/23 kwa maumivu baada ya bei za mafuta kupanda kwa viwango tofauti. 

Mwaka mpya wa 2022/23 ambao ni mahususi kwa utekelezaji wa bajeti kuu ya Serikali umeanza Julai mosi mwaka huu.

Katika bei mpya za rejareja zilizotangazwa Julai 5 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), bei ya petroli inayopitia bandari ya Dar es Salaam imepanda hadi kufikia Sh3,320 kwa lita kutoka Sh2,994 iliyokuwa ikitumika Juni.

Kwa bei hizo, itawafanya wamiliki wa vyombo vya moto kutoboa zaidi mifuko yao ambapo watanunua nishati hiyo kwa Sh226 zaidi ya mwezi uliopita.

Bei hiyo ya Julai ambayo imeanza kutumika leo imeongezeka kwa asilimia 7.5 licha ya Serikali kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni katika ili kuwapunguzia gharama za maisha Watanzania. 

Kiasi kikubwa cha ruzuku kimeelekezwa katika mafuta ya dizeli kwa lengo la kudhibiti mfumuko wa bei (inflation) kwa sababu dizeli hutumika zaidi katika shughuli za kiuchumi ikiwemo katika uzalishaji viwandani na katika usafirishaji wa mazao na bidhaa nyingine.

Dizeli kwa sasa inauzwa kwa Sh3,143 kwa lita moja kutoa Sh3,131 huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa Sh3,442 kutoka Sh3,299.

Wakazi wa Ruberwa wilayani Kyerwa mkoani Kagera ndiyo watanunua petroli kwa bei ya juu kuliko maeneo mengine Tanzania. Kwa mujibu wa Ewura petroli katika eneo hilo inauzwa Sh3,458.


Soma zaidi:


Maumivi hadi mikoani

Wakati bei zikipanda jijini Dar es Salaam, mikoa inayotumia mafuta yanayopitia katika Bandari ya Tanga zimeshuka ambapo petroli inauzwa kwa Sh3,214 kwa lita kutoka Sh2,985.

Hata hivyo, bei ya dizeli imeshuka hadi Sh3,150 kwa lita kutoka Sh3,162 ya mwezi uliopita.

Kwa mafuta yanayopitia bandari ya Mtwara, petroli sasa inauzwa Sh3,205 ambapo imeongezeka kutoa Sh2,979 kwa lita huku dizeli ikiuzwa kwa Sh3,172 kutoka Sh3,165.

Kupanda kwa bei ya mafuta huenda kukaongeza gharama za maisha kwa sababu nishati hutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, jambo likalowafanya watu watoboe zaidi mifuko yao.

Msemaji Mkuu wa Serikali Greyson Msigwa akizungumza na kituo cha redio cha C FM cha jijini Dodoma amesema ruzuku ya Sh100 bilioni iliyotolewa na Serikali zimeleta unafuu kwenye kwa wananchi.

“Zipo nchi lita moja ya mafuta imeshafika Sh8,000, lakini Rais Samia Suluhu akasema  wananchi wangu wa Tanzania watapata shida kwa sababu mafuta yakipanda bei kila kitu kitapanda bei,” amesema Msigwa huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kutafuta suluhu ya kupanda kwa bei ya mafuta.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW