China yazindua chanjo ya hewa kujikinga dhidi ya Uviko -19
- Huenda ikavutia baadhi ya watu ambao wana hofu na sindano
- Mtu ataweza kuivuta kwa mfumo wa hewa ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo.
Dar es Salaam. China imezindua chanjo mpya ya virusi vya Corona (Uviko-19) ambayo mtu ataweza kuvuta kwa mfumo wa hewa ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), China inakuwa nchi ya kwanza duniani kuja na aina hiyo ya chanjo ambayo imetengenezwa na kampuni ya chanjo ya CanSino Biologics Inc.
Mtendaji Mkuu wa CanSino, Xuefeng Yu amesema kampuni ya CanSino imetengeneza chanjo hiyo ya kuvuta ili kuchochea kingamwili kwenye tishu za pua na njia ya hewa ili kujilinda dhidi ya virusi vya Corona.
“Tumetumia muda mwingi (Miaka) kutengeneza chanjo ya aina hii na tulianza kwenye magonjwa yote yanayoaambukizwa kwa mfumo wa hewa kama kifua kikuu,” amesema Yu, akinukuliwa na BBC.
Ameongeza kuwa waliamini kwamba endapo mfumo wa hewa ambayo ndio njia kuu ya virusi kupita ikiwa na kinga imara basi itapunguza uwezekano wa vizuri vya Corona kuenea.
Zinazohusiana:
- Chanjo ya Uviko-19 Afrika Mashariki bado ngoma ngumu
- Dar es Salaam yaongoza maambukizi ya Uviko-19 Julai
Huenda njia aina hii ya chanjo ikawavutia baadhi ya watu ambao wamekuwa ni waoga wa kuchomwa sindano ambayo ndio utaratibu unaoendelea kutumika sasa nchi nyingi duniani.
Aidha, baada ya uzinduzi wa chanjo hiyo mpya hisa za kampuni hiyo zimeshuhudiwa kupanda kwa asilimia 14.5 katika soko la hisa jijini Hong Kong.