Fahamu: Corona haidhibitiwi kwa chanjo ya nimonia

November 19, 2020 2:01 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Virusi vya magonjwa hayo hushambulia mfumo wa mpumuaji.
  • WHO yasema virusi vya COVID-19 ni vipya na vinahitaji chanjo yake. 
  • Watu watakiwa kuendelea kutumia chanjo zinazopendekezwa kwa ugonjwa husika.

Dar es Salaam. Wapo baadhi ya watu wanaoamini kuwa ikiwa mtu atapata chanjo ya ugonjwa nimonia basi anajiweka katika nafasi nzuri ya kutoambukizwa ugonjwa wa Corona. Dhana hiyo siyo sahihi.

Nimonia (Pneumonia) ni ugonjwa wa mfumo wa upumuaji unaoambatana na kupungua ufanisi wa mbadilishano wa hewa kati ya binadamu na mazingira yake ya nje.

Ugonjwa huo wa homa ya mapafu huenezwa kwa njia ya hewa ama kugusana  na mgonjwa ambapo huwapata zaidi watoto na wazee kutokana na kutokuwa na mfumo imara wa kinga ya mwili. 

Licha ya kuwa virusi aina ya COVID-19 hushambulia mfumo wa upumuaji kama ilivyo kwa virusi vya nimonia, haviwezi kudhibitiwa na chanjo ya ugonjwa huo. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema virusi vya COVID-19 ni vipya na vinahitaji chanjo yake isiyohusishwa na chanjo za magonjwa mengine ili kuhakikisha ufanisi wake. 

“Watafiti wanaendelea kutengeneza chanjo dhidi ya COVID-19 na WHO inazitambua na kufanikisha juhudi hizo,” imesema WHO.


Zinazohusiana:


Shirika hilo ambalo ni mwangalizi mkuu wa masuala ya afya duniani, limesema licha ya kuwa chanjo ya nimonia siyo sahihi dhidi ya COVID-19, bado linapendekeza watu kupata chanjo ya magonjwa mengine ya mfumo wa upumuaji zinazopendekezwa na wataalam wa afya ili kulinda afya zao.

Njia sahihi ya kujikinga na Corona ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa, kutumia tishu wakati kukohoa au kupiga chafya na kuepuka mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima.

Enable Notifications OK No thanks