Mwanafunzi afariki kwa kuangukiwa na jiwe akitekeleza adhabu ya kutoongea Kiingereza

March 17, 2023 2:23 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mwanafunzi wa Shule ya sekondari Mwinuko mkoani Mwanza.
  • Walipewa adhabu na wenzake 31 ya kusomba kifusi baada ya kufanya kosa la kuongea Kiswahili shuleni. 
  • Walimu wawili washikiliwa na polisi kusababisha kifo chake. 

Mwanza. Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia walimu wawili wa Shule ya Sekondari Mwinuko kwa kosa la kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja wa kidato cha kwanza na mwingine kujeruhiwa waliokuwa wakitekeleza adhabu ya kusomba kifusi cha mchanga baada ya kuzungumza lugha ya Kiswahili shuleni.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mtafungwa akizungumza na waandishi wa habari leo Marchi 17, 2023 amesema tukio hilo limetokea leo saa 1:50 asubuhi ambapo wanafunzi hao wakiwa na wenzao 30 walipatiwa adhabu hiyo jana baada ya kuzungumza lugha ya Kiswahili shuleni kinyume na taratibu za shule hiyo.

Amemtaja aliyefariki dunia kuwa ni Gloria Faustine (14), mwanafunzi wa kidato cha kwanza huku  Emmanuel Lyatuu ambaye amajeruhiwa akiwa amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekouture akiendelea kupatiwa matibabu.

Kamanda Mtafungwa amesema adhabu hiyo walipatiwa na mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalu Baluya ambapo walianza kutekeleza adhabu hiyo jana Machi 16 lakini hawakuimaliza hivyo leo wakawa wanaendelea nayo.

“Wakiwa wanaendelea kutekeleza adhabu hiyo, gafla jiwe kubwa lililokuwa linashikiliwa na udongo huo lilidondoka na kuwaangukia wanafunzi hao ambapo mmoja alifariki papo hapo na mwingine kujeruhiwa kwenye mguu wake wa kulia,” amesema Mtafungwa.

Amesema wanafunzi wengine waliokuwa kwenye adhabu hiyo walikimbia hivyo hawakuweza kupata madhara yoyote. 

Amesema kitendo hicho kilizua taflani kwa wazazi wanaoishi eneo hilo ambapo walianza kuwashambulia walimu hao kwa kuwarushia mawe na kung’oa mbogamboga na viazi vilivyolimwa shuleni hapo.

Mwonekano wa jiwe lililoanguka na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja wa kidato cha kwanza na mwingine kujeruhiwa waliokuwa wakitekeleza adhabu ya kuchimba kifusi na kufukia mitaro kama adhabu ya kutojua kuzungumza Kiingereza katika Shule ya Sekondari Mwinuko. Picha | Mariam John.

Hata hivyo, vurugu  zilizuiwa na polisi na kufanikiwa kurejesha hali ya utulivu kwenye eneo hilo.

Kamanda Mtafungwa amesema wanawashikiliwa walimu hao kwa mahojiano zaidi kujua namna adhabu ilivyotekelezwa na usimamizi uliokuwepo wakati wanafunzi hao wakitekeleza lakini pia kujiridhisha udongo ulivyokuwa kwenye eneo hilo.

 “ Tunawashikilia walimu hao kwa ajili ya uchunguzi zaidi kujua namna adhabu zilivyokuwa zimetolewa na namna walivyoweza kuzisimamia,” amesema Mtafungwa.

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Kamila Labani ametoa rai kwa walimu hususani katika kipindi hiki cha mvua kufahamu kuwa ardhi inakuwa oevu na watoto wanapenda kucheza kwenye mawe hayo wasiyaamini sana.

“Jiografia ya Mkoa wa Mwanza ni mawe, hivyo wazazi wasiyaamini sana hasa kipindi hiki cha mvua wawe waangalifu ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea,” amesema.


Zinazohusiana


Wazazi wacharuka

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya wazazi wanaoishi karibu na neo la Mwinuka Sekondari wamesema shule hiyo inaongoza kwa kutoa adhabu kali kwa wanafunzi hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo yao.

Agnes Majola amesema kitendo kilichofanywa na walimu hao hakivumiliki na kuiomba Serikali kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa walimu wengine wenye tabia hizo.

“Huyo mwalimu aliyetoa adhabu hiyo ni mama na amezaa, itakuwaje iwapo mtoto wake afanyishwe adhadbu kama hizo, tena mtoto wa kike si bora angepewa adhabu nyingine kama ya kufagia au kudeki chooni,” amesema Diana Peter, mkazi wa Mwanza. 

Mzazi wa marehemu azungumza

Akiwa na masikitiko makubwa, baba mzazi wa mtoto huyo, Felician Faustine amesema binti yake amemuaga asubuhi kuwa anaenda shule na kumwambia amchukule hela sehemu wanayowekaga kwa ajili matumizi shuleni.

Amesema majira ya saa 3 alipokea simu kutoka kwa mtu akimweleza kuwa mtoto wake amepata ajali lakini hali yake sio nzuri sana.

“Baada ya kupata taarifa hizo nilienda moja kwa moja shuleni na kuonyeshwa sehemu walipokuwa wanatoa kifusi lakini mwili sikuukuta na mpaka sasa sijafika hospitalini kujiridhisha kama mtoto amefariki,” amesema Faustine baba wa binti aliyefariki kwa adhabu ya kusomba kifusi shuleni.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
25 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
25 May, 2026
No active movers today
Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

Nukta TV

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Nukta TV

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

Nukta TV