Tisa mbaroni mauaji ya mwanafunzi SAUT, dereva
- Walitekeleza uharifu huo kwa matukio mawili tofauti.
- Waliouawa ni dereva taxi na mwanafunzi wa Saut.
- Serikali yawakamata watu tisa kwa uchunguzi.
Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu tisa kwa mauaji ya watu wawili akiwemo dereva wa taxi kuuawa kwa kunyongwa na kamba shingoni na kuchomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili.
Mauaji hayo yametokea katika matukio mawili tofauti.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ramadhan Ng’azi katika taarifa yake iliyotolewa leo Februari 1, 2022 amesema tukio la dereva huyo kuuawa lilitokea Januari 26 mwaka huu katika kijiji cha Kasungamile wakati watuhumiwa walipomkodi dereva huyo kuwapeleka nyumbani kwao Wilaya ya Sengerema.
Amewataja watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni Robert Daud (42), Sylivester Renatus (30), Ryabakamba Sekelwa(30) ambaye ni mganga wa kienyeji na Elizabeth Jackson(23) ambapo wote watuhimiwa wote wanne ni wakazi wa Katunguru mkoani Mwanza.
Inadaiwa marehemu ambaye ni mwanaume aliuawa ndani ya gari aina ya IST rangi nyeusi yenye namba za usajili T143 DHV kwa kukabwa na kamba, kuchomwa na visu shingoni na kutobolewa macho.
Kamanda Ng’azi amesema marehemu alikodiwa na Sylivester Renatus akiwa na mkewe Elizabeth Jackson kutoka Buzuruga Mwanza kwenda kijiji cha Kasungumile Wilaya Sengerema na inadaiwa baada ya kufanya mauaji hayo walikwenda kwa mganga wa kienyeji ili wasafishwe aitwaye Sekelwa.
“Kiini cha tukio la mauaji hayo ni kuwania mal i(kupora gari) ingawa tayari gari imepatikana ikiwa imefungwa namba bandia mbele na nyuma ambayo ni T620 CGN na eneo la tukio kulipatikana visu viwili, panga moja, nyundo moja na simu mbili aina ya Tecno moja kubwa na nyingine ndogo na kamba moja,” amesema Ng’azi.
Soma zaidi:
-
Miili ya wanawake watatu waliouawa yazikwa Mwanza
-
Watano mbaroni mauaji ya ndugu wa familia moja Mwanza
Upelelezi wa tukio hilo unaendelea utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Katika tukio la pili polisi wanawashikilia watu watano wakazi wa mtaa wa Ng’washi kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana kwa kosa la kumuua mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mtakatifu Augustine (Saut), Nicholus Teleshory mwenye miaka 24.
Mwanafunzi huyo aliuawa kwa kupigwa mawe na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake akituhumiwa kuiba televisheni na baadaye kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekouture.
Tukio hilo lilitokea Januari 29 mwaka huu na kuwataja watuhumiwa kuwa ni Thobias Lucus (20), Alex Madoshi (20), Yusuph Mwandesha (25), Samwel Masalu (25) na Nyanda Madirisha (19) ambapo wote ni waendesha bajaji kata ya Buhongwa.
Kamanda Ng’azi amesema kitendo walichofanya watuhumiwa hao ni kujichukulia sheria mkononi na kwamba upelelezi unafanyika ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Latest
