Mke adaiwa kumuua mume wake akishirikiana na watoto
- Aliyeuawa ni mkazi wa Kijiji cha Kiliwi wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Mange Washa (49).
- Inadaiwa aliuawawa na mke wake na watu wengine watano wa kukodi.
- Ugomvi wa familia wadaiwa kuwa chanzo.
Mwanza. Watu watano akiwemo mama na watoto wake wawili wanaodaiwa kuhusika katika mauaji ya baba yao ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kiliwi wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Mange Washa (49) wamepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka moja la mauaji.
Waliopandishwa kizimbani leo Disemba 14, 2022 katika Mahakama ya Wilaya ya Kwimba ni Hoka Mazuri (48) ambaye ni mke wa marehemu, watoto wake wawili ambao ni Masunga Mange na Paskali Mange.
Wengine ni wanaume wawili wanaodaiwa kulipwa Sh800,000 na wanafamilia hao kisha kutekeleza mauaji ya Washa ambao ni Shija Masalu (28) na Makoye Lusana (53) ambaye ni mshitakiwa namba moja katika kesi hiyo ya jinai namba 12/2022.
Tukio hilo la mauaji lilitokea Disemba mosi mwaka huu ambapo inadaiwa lilipangwa na familia ya Mwasha na kutekelezwa usiku wa manane nyumbani kwake.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mtafungwa amesema katika tukio hilo mke wa marehemu, watoto wake wawili na watu wengine walikodiwa kwa Sh800, 000 ili kutekeleza mauaji hayo.
Mtafungwa amesema siku ya tukio watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa marehemu Mwasha kwa kuvunja mlango kisha kuingia ndani na kumkata shingo hivyo kusababisha kifo chake.
“Baada ya kufanya uchunguzi chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa familia kati ya baba na watoto wake wa kiume ambaye alikuwa akimtuhumu kujihusisha na wizi,” amesema Mtafungwa.
Kwa mujibu wa Mtafungwa amesema baba mzazi wa kijana huyo baada ya kubaini mtoto wake alikuwa mwizi alimfukuza nyumbani kwake, kitendo ambacho hakikumfurahisha mama mzazi hivyo kuamua kuwashawishi watoto wake kumuua baba yao.
Mauaji ya Mwasha ni muendelea matukio ya kinyama ambayo yamekuwa yakiripotiwa kwa miezi miwili mkoani Mwanza ambapo tukio lilivuta hisia za watu ni Kifo cha utata cha Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza, Boniphace Kwangu.
Askofu Kwangu alikutwa amekufa Disemba Mosi majira ya saa 10:00 jioni na mwili wake ukielea juu ya maji katika Ziwa Victoria karibu na linapojengwa daraja la Kigongo-Busisi maarufu kama JPM.
Tukio lingine ni kifo cha Hamida Mussa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) tawi la Mwanza. Anadaiwa kunyongwa na binti wa kazi Novemba 28 mwaka huu katika Mtaa wa Buzuruga wilayani Ilemela.
Latest