Zaidi Sh24.3 bilioni zitakavyopunguza umaskini Mwanza
- Zitatumika miaka mitano ijayo.
- Zitajenga miundombonu ya kutoa huduma za kijamii.
- Kuzalisha ajira za muda kwa vijana.
Mwanza. Huenda watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri ukapungua mkoani Mwanza kwa miaka mitano ijayo, baada ya mkoa huo kupata fedha zitakazoelekezwa katika uboreshaji wa miundombinu ya kijamii.
Mkoa wa Mwanza unatarajia kupokea zaidi ya Sh24.3 bilioni zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi ya kupunguza umasikini mkoani humo.
Fedha hizo zinatarajiwa kupokelewa katika kipindi cha miaka mitano ijayo ambazo zitasaidia kutekeleza miradi 40 ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya na utoaji wa ajira za muda.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza kwenye kikao kazi cha kujengeana uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa miradi ya kupunguza umasikini awamu ya nne (TPRP IV) katika mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), amesema matarajio yake katika awamu hii ni kusaidia jamii kupata huduma za afya.
“Ni mataajio yangu kuwa katika mradi huu wa awamu ya nne utawezesha jamii kupata mafanikio ikiwemo ongezeko la huduma za afya, elimu hasa katika kuwawezesha watoto chini ya miaka mitano kuhudhuria kliniki na wanafunzi kuhudhuria shuleni,” amesema Mhandisi Robert.
Mkuu huyo wa mkoa amewataka viongozi na wataalam wote kuzingatia sheria kanuni, taratibu na miongozo wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na usimamizi thabiti wa fedha itakayotumika iendane na ubora wa miradi hiyo.
Soma zaidi:
Utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kuwaondolea umaskini wakazi wa mkoa huo na hivyo afya na maisha yao wakati wakitekeleza shughuli za maendeleo.
Awali, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi- Mipango na Uratibu Mkoa wa Mwanza, Joachim Otaru amesema zoezi la uibuaji wa miradi ya kupunguza umasikini awamu ya nne (TPRPIV) ambayo jumla ya miradi 104 imeibuliwa na kupitishwa na wizara kwa ajili ya utekelezaji.
Amesema kati ya miradi hiyo, 31 ni ya afya, 49 elimu na 24 ni miradi ya kutoa ajira za muda na kwamba miradi hiyo itagharimu zaidi ya Sh7.8 bilioni.
“Hadi sasa Mkoa umepokea jumla ya bilioni 3.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 40 ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, 23 ni miradi ya afya na 16 ni ajira za muda,” amesema Otaru
Akizungumzia mafanikio yaliyofikia katika utekelezaji wa miradi hiyo katika awamu tatu ni pamoja na ongezeko la mahudhurio ya wanafunzi shuleni na kwa watoto wenye umri wa kuhudhuria huduma ya kiliniki kwa asilimia 95.
Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Mwanza, Monica Mahundi amesema mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa mitano inayotekeleza miradi ya kupunguza umasikini awamu ya nne.
“Mkoa wa Mwanza tumepokea zaidi ya Sh 3.2 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi 40 ikiwa na maana ya miradi mitano kwa kila halmashauri zilizopo mkoani hapa, miradi hiyo inaanza utekelezaji wake muda si mrefu kuanzia sasa,” amesema Mahundi.
Latest