Youtube yaipiga chini Netflix, yavuna Sh154 trilioni mwaka 2025
- Mapato yaliyokusanywa na Youtube ni zaidi ya asilimia 32.8 ya mapato yaliyokusanywa na Netflix.
Dar es Salaam. Mtandao wa Youtube umetangaza kupata mapato ya zaidi Dola za Marekani bilioni 60 (zaidi ya Sh154 trilioni) katika mwaka wa fedha 2025, yakichangiwa zaidi na matangazo ya biashara na huduma za usajili.
Hii ni kwa mara ya kwanza kwa Alphabet, kampuni mama ya mtandao huo wenye watumiaji zaidi ya bilioni 2.7 duniani kote kuweka wazi mapato ya jumla ya YouTube kwa mwaka mzima, hatua inayodhihirisha ukubwa na mchango wa jukwaa hilo katika uchumi wa kidijitali wa kimataifa.
Kiasi hicho cha mapato kinaifanya YouTube kuwa kinara wa majukwaa ya kuonyesha maudhui ‘streaming’ na kuacha mbali Netflix iliyoripoti mapato ya Dola za Marekani bilioni 45.18 (zaidi ya Sh116.82 trilioni) kwa mwaka 2025.

Mapato yaliyokusanywa na Youtube ni zaidi ya asilimia 32.8 zaidi ya mapato ya Netfix ambayo hivi karibuni imeanza kupandisha ada kwa wateja wake huku ikikabiliwa na presha ya soko.
Kwa kulinganisha na makampuni mengine shindani katika soko, YouTube imezidi mapato karibu kampuni zote kubwa za burudani isipokuwa Disney, ambayo ilirekodi Dola bilioni 95.7 katika kipindi kama hicho.
Sundar Pichai, Mkurugenzi Mtendaji wa Alphabet na Google amesema huduma za kampuni hiyo kwa sasa zina zaidi ya sajili milioni 325 za kulipiwa, ikiwemo YouTube Premium, YouTube TV na Google One, jambo linaloonyesha mabadiliko katika matumizi ya maudhui ya kidijitali yanayolipiwa.
Matangazo chanzo kikubwa cha mapato
Kwa mujibu wa Pichai, matangazo ya biashara yameendelea kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa YouTube, ambapo robo ya nne ya mwaka 2025 yalifikia Dola za Marekani bilioni 11.38, kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa katika robo moja ya mwaka.
Hata hivyo, mapato hayo yalikuwa chini ya matarajio ya Wall Street ya Dola za Marekani bilioni 11.84, kutokana na kupungua kwa matangazo ya kisiasa ikilinganishwa na robo kama hiyo mwaka 2024.

Katika ngazi ya kampuni, Alphabet iliripoti mapato ya Dola za Marekani bilioni 113.8 kwa robo ya nne ya mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 18, huku faida halisi ikiongezeka kwa asilimia 30 hadi Dola za Marekani bilioni 34.5.
Huenda kukua kwa mapato ya Youtube kukawa ni kicheko kwa watengeneza maudhui ikiwemo wasanii na wacheza filamu duniani kote ikiwemo Tanzania kutunisha mifuko yao zaidi kutokana na mapato ya matangazo kupitia jukwaa hilo ambalo watu hujitengenezea mamilioni.
Latest