YouTube yaja kivingine, kufanya kolabo na ‘Podcasters’

March 7, 2022 11:43 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Watengeneza maudhui ya sauti watapata zaidi ya Sh700 milioni.
  • Wadau wasema ni hatua nzuri ya kuongeza mifumo ya mapato.
  • Wasikilizaji wafurahi kuwaona watangazaji wao.

Dar es Salaam.Kampuni ya kupakia video mtandao ya YouTube inazidi kuongeza ushindani katika sekta ya teknolojia na mawasiliano baada ya kuamua kuwafikia watengeneza maudhui ya sauti za mtandaoni (Podcasters) ili kufanya nao kazi kwa nia ya kuongeza kipato.

Imetangaza mpango huo wa kuwalipa wanaotengeneza maudhui ya sauti (podcasters) ili kutengeneza vipindi vya video kwa ajili ya kuvipakia kwenye jukwaa lake. Malipo hayo yatafanyika kutokana na matangazo yatakayowekwa kwenye vipindi. 

Hii ni baada ya vipindi hivyo kupata umaarufu katika majukwaa mbalimbali ikiwemo Spotify, Apple Podcasts na Deezer.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Bloomberg, YouTube itawafikia watengeneza maudhui pamoja na mitandao ya kutengeneza maudhui hiyo yaani Podcast Networks.

YouTube imesema itatoa msaada wa hadi Dola za Marekani 300,000 sawa na takriban Sh703 milioni kwa ajili ya kuhuisha watengeneza maudhui ya sauti kutengeneza viindi vya video sambamba na maudhui yao.

Kwa watu binafsi, YouTube itatoa Dola za Marekani 50,000 ambayo ni zaidi ya Sh117 milioni huku mitandao ya maudhui ya podcast ikipata Dola za Marekani 200,000 (Sh468 milioni) hadi Dola za Marekani 300,000 (Sh703 milioni).

Wadau waliofikiwa na Bloomberg wamesema fedha hizo zitawasaidia kutengeneza video za vipindi vya zamani na hata kutengeneza vipindi vipya.

Bloomberg imeandika kuwa, gharama za ujenzi wa studio, manunuzi ya vifaa na kuajiri wataalamu wa kamera huenda zikarudisha nyuma juhudi za YouTube.


Zinazohusiana:


Wadau wa Podcast wanena

Licha ya kuwa mfumo huo utawafikia wachache ambao tayari wana majina wadau wa podcast wamesema jitihada hizo zitawapatia matumaini na zinabadilisha mtazamo wa muundo wa maudhui ya podcasts.

Mwanzilishi mwenza wa podcast ya Sports Cast kutoka Tanzania, Clifford Sangai ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa hatua ya YouTube ni nzuri lakini huenda watengeneza maudhui watahitaji kufikiria urefu wa maudhui wanayoyaweka mtandaoni humo.

Kwa kawaida, zipo podcast ambazo hutumia hadi dakika 45 na zaidi, jambo ambalo Watanzania wengi wanaweza kushindwa kuzifuatilia kutokana na gharama za bando.

“Cha kushauri hapo ni labda wakate vipande vya msingi ndiyo wapakie YouTube na siyo kipindi kizima,” amesema Sangai.

Sangai amesema kwa Watanzania wengi, kutumia bando zao kuangalia kitu cha dakika 40 na zaidi ya hapo ni mtihani.

Mdau huyo amesema mfumo huo utawasaidia watengeneza maudhui kupata vyanzo vya mapato kutoka matangazo ya ndani ya kipindi hadi matangazo ya YouTube.

Naye Daniella Duncan, mkazi wa Morogoro amesema mfumo huo utasaidia kuchangamana zaidi na podcast zake kwani huwa anatamani aone hisia za mtangazaji lakini kwa kuwa zipo kwenye sauti, anashindwa.

“Unakuta kipindi kimechangamka kweli na unatamani kweli uone mtangazaji anachofanya lakini hauwezi. Hii ikifanikiwa itafaa sana,” amesema Duncan.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW