Yanayoambatana na mfumo mpya endeshi wa simu za iPhone

September 21, 2021 8:23 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mfumo endeshi wa simu na saa wa iOS15
  • Mfumo huo umeboresha kurahisisha mawasiliano ya simu.
  • Unawezesha kufanya kazi zaidi ya moja kwenye simu kwa wakati mmoja.

Dar es Salaam. Ni kawaida kwa Apple kuwa na mfumo endeshi mpya kila mwaka. Kwa mwaka jana, kulikuwa na iOS14 ambayo iliipatia skrini ya simu za iPhone muonekano mpya.

Kampuni hiyo ya teknolojia ya Marekani jana Septemba 20, 2021 imetambulisha mfumo mpya endeshi wa iOS15 ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wa simu za iPhone duniani.

Kabla ya kwenda mbali, huenda unajiuliza iOS ni nini. Kwa lugha nyepesi, iOS ni mfumo endeshi unaotumika kwenye bidhaa za Apple ikiwemo simu, iPads na saa.

Kwa mfumo endeshi ambao tayari umeingia sokoni, haya ndiyo yanayoambatana nao.

Mfumo wa “share play”

Kama wewe ni mdau wa simu za iPhone na iPad, bila shaka unafahamu programu ya FaceTime. Kwa wageni, programu hiyo inafanya kazi kama ilivyo “WhatsApp video call” lakini ni mahsusi kwa bidhaa za Apple tu.

iOS15 itawezesha watumiaji wa FaceTime kusikiliza muziki, kutazama video pamoja na kuonyesha kinachoendelea katika skrini ya simu wakati wa mazungumzo. 

Kwa kifupi, ni kama simu za video za Zoom zinavyofanya kazi.

Pia kupitia FaceTime, mtu anaweza kuendelea na mazungumzo wakati akiangalia video zingine. Mtu hatokuwa na haja ya kuacha kila kitu alichokuwa anakifanya ili aongee na mtu.

Kingine ni muonekano wa picha za potrait (Picha zinazoweka umakii au “focus” kwa mtu na kufifisha mandari ya nyuma yake) lakini kwenye video, muundo unaompa mtu umakini kuliko mazingira ya nyuma yake na pia muundo wa “voice isolation” unaoondoa kelele za watu wengine ulio nao karibu na kuibakiza sauti yako tu.

Ni kama kusema, ukiwa kwenye daladala na konda anaongea huku wewe upo kwenye  mazungumzo, sauti ya konda itaminywa ili yako isikike zaidi.

Mfumo huu utaongeza ukaribu kati ya mtu na mtu kwani watu walio mbali, wanaweza kuangalia filamu pamoja na hata kama kuna mafunzo ya mapishi kwa njia ya video, watu wanaweza kujifunza pamoja huku video hiyo ikiendelea.

Mtu anaweza kuangalia filamu, kusikiliza muziki na hata kucheza gemu wakati akiongea na simu ya video. Picha| 9to5Mac.

“Kupiga mbizi” kwenye utendaji kazi wako

Katika kufanya kazi, kuna mambo mengi yanayoweza kukutoa kwenye reli. Mlio wa meseji mpya ukiingia, mlio wa simu ikikukumbusha tukio fulani na kadhalika.

Ili kuhakikisha kuwa unakamilisha majukumu yako ipasavyo, iOS15 imekuja na mbinu mpya ya “Focus”.

Focus inakupa wasaa wa kuchagua vipaumbele vyako vya siku. Kama utaanza na majukumu ya kazi, na kisha kutaka muda wa kujisomea na kisha kupumzika, yote hayo Focus itakusaidia kukukumbusha ili uyatimize.

Ukiweka mfumo huo, utapata taarifa “notifications” husika tu. Tusema kama upo kazini, utapata taarifa zinazohusiana na kazi yako tu.

Pia, Focus itakusaidia kujibu meseji za rafiki zako watakaokuwa wanajaribu kuwasiliana na wewe wakati umepiga mbizi kwenye majukumu yako. 

Muonekano mpya wa ramani

Kwa kawaida, ramani huonyesha hadi paa la nyumba na sehemu kidogo ya upande wa nyumba ukiwa kwenye mtandao mzuri. Lakini iOS15 inakupa muonekano mpya wa “Maps” unakuruhusu kuona ramani katika muundo wa pembe tatu (3D).

Japo 3D ni kwa majengo maarufu tu, lakini bado itasaidia katika kumuelekeza mtu kutumia ramani kufika mahala fulani kuliko ilivyokuwa awali.

Mbali na ramani, kivinjari (browser) cha Safari pia kina muonekano mpya. Kwa wageni, Safari ni kivinjari kinachotumika kwenye simu, iPad na kompyuta za Apple.

Zamani sehemu ya kuandikia (tab bar) kwenye tovuti ilikuwa kwa juu lakini sasa imeshushwa chini kwa ajili ya urahisi wa kufikika pale unapotumia simu yako hata kwa mkono mmoja.

Pia, ukipangusa kwenda juu, utaona tovuti zote (tabs) unazovinjari. Pia unaweza kuvinjari mtandaoni kwa kutumia sauti yako.

Maboresho yamefanyika kwenye ramani, kivinjari na programu za meseji na simu. Picha| Apple.

Mengineyo ni mfumo wa “Live Text” ambao unafanya kazi sawia na Google Lens ambayo inakuwezesha kutumia kamera kunakili maandishi yaliyopo kwenye matangazo, mabango na vipeperushi. 

Live Text inaelewa lugha saba ikiwemo Kiingereza, Kichina, Kifaransa, Kiitaliano, Kireno, Kijerumani na Kihispania.

Kingine ni ulinzi wa taarifa zako. iOS15 inazuia programu (apps) mbalimbali kukusanya taarifa zako kiholela na pia sauti yako unayotumia kuzungumza na roboti sauti. Siri hazitotoka nje ya simu yako.

Nani kaachwa? 

iOS14 mwaka jana ilitemana na simu za iPhone 6 kwenda chini. Kwa mfumo endeshi mpya wa iOS!5, mwendo umebaki ule ule kwani itafanya kazi kwenye simu zote za Apple kuanzia iPhone 6S kwenda juu hadi iPhone 13 Pro Max.

Vipi, simu yako ipo au nawe ndiyo umeachwa?

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW