Ifahamu iPhone 15 kwa undani
- Imetengenezwa kwa kuzingatia utunzaji mazingira
- Ndio iPhone ya kwanza kutumia ‘Type C’
Dar es Salaam. Wakati baadhi ya watumiaji wa simu za iPhone bado hawajamaliza kufaidi toleo la 14 la simu hizo lililotoka mwaka jana, tayari kampuni inayotengeneza simu hizo ya Apple imezindua iPhone 15 ikiwa na matoleo manne.
Matoleo hayo ni iPhone 15 plain, iPhone 15 plus, ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na matoleo mengine mawili ya iPhone 15 pro na promax kwa ajili ya matumizi maalumu kama kurekodi video na kupiga picha.
Simu za toleo jipya zimenakshiwa na makasha yaliyotengenezwa kwa madini ya titanium yanayotajwa kuiwezesha simu hizo kutumika angani na kuhimili kutu.
Toleo hili lina urefu wa inchi 6.29, upana wa inchi 3.02 na unene wa inchi 0.32. vipimo hivi vinalifanya toleo hili kuwa dogo ukilinganisha na la awali lenye urefu wa inchi 6.33, upana wa inchi 3.05 na unene wa inchi 0.31.
Soma zaidi
-
Sarufi AI teknolojia ya akili bandia inayorahisisha mawasiliano
-
Tanzania kutumia teknolojia kuwavuta vijana kwenye kilimo
Bei imechangamka
Kama kawaida, simu za iphone huuzwa kwa dau lililochangamka kidogo vijana huita pesa za madafu, ili kupata toleo jipya la iPhone 15 plain utalazimika kutoboa mfuko hadi Sh2 milioni, na kwa iPhone 15 plus utatoa, Sh2.2 milioni.
Kwa upande wa iPhone 15 Pro yenyewe utaipata kwa Sh2.5milioni na Sh3milioni kwa iPhone 15 Pro Max.
Kamera ndo mahali pake
Kwa wale wapenda ‘selfie’ na picha kali, iPhone 15 ndiyo yenyewe kwani inaweza kupiga picha na kurekodi filamu kwa ubora ang’avu (HD) kwa ubora wa 4K. Simu hii ina mfumo wa kamera unaoundwa na lenzi nne huku ikikuwezesha kukuza picha (zoom) mara tano zaidi ya iPhone 14.
Wabunifu wa picha na mitindo ya nguo wakitumia iPhone kwenye ‘photoshoot’ na watumiaji wanaweza kuhamisha picha hizo moja kwa moja hadi kwenye Macbook bila kupoteza ubora . Picha|Apple.com
Kelvin Alfred, afisa mauzo wa kampuni inayojihusha na uuzaji wa vishkwambi na simu janja ya Vetex, ameiambia Nukta Habari kuwa ubora wa kamera ya simu hiyo utakuwa neema kwa wapiga picha na watengeneza filamu kwani picha zake zitakuwa bora na kuongeza wateja.
“Ni kama iPhone 14 iliochangamka, kamera yake inauwezo kuliko hata Sony, kwa wanaoenda ‘photoshoot’ msishangae kukuta mpiga picha anatumia iPhone yake.” amebainisha Alfred.
Kwa wale wanaotengeneza filamu, unaweza kuepuka gharama za kamera kwa kununua tu iPhone 15 kwa kuwa kamera yake inaweza kurekodi picha 60 kwa video ya sekunde moja jambo linaloruhusu kutengeneza filamu yenye picha ang’avu.
Mfumo mpya wa chaja.
Kama ulikuwa haujui, toleo jipya la iPhone 15 linatumia chaja na viunganishi vya aina C (Type C) vilivyozoeleka kutumika katika simu za ‘Android’.
Hii itaipa simu hizi uwezo kuhamisha na kupokea data katika kasi ya gigabaiti 10 mpaka 25 kwa sekunde.
Hata hivyo, kama ulikuwa unadhani utaweza kutumia chaji za simu nyingine zinaofanana umeula wa chuya, pamoja na kutumia chaja type C, bado itatumia chaja maalumu zilizotengenezwa mahusus kwa ajili ya iPhone pekee.
Itakumbukwa kuwa Oktoba 2022 Bunge la Umoja wa Ulaya liliadhimia kutumia chaja na viunganishi aina C kwa vifaa vyote vya mkononi ili kuboresha urahisi wa watumiaji na kupunguza kwa kiasi kikubwa taka za kielektroniki.
USB ‘type C’ inaiwezesha iPhone kuchaji na kutuma data kwa kasi zaidi. Picha|apple.com
Zingatia haya unapotaka kununua iPhone 15
Kelvin amewarai watu wanaotarajia kununua simu hizo siku za usoni kuangaliwa kwanza namba za usajili za simu yaani ‘IMEI number’, na hakikisha kama simu haijawahi kuunganishwa na laini yoyote.
“Kama mtumiaji pia hakikisha simu yako ina Apple Warranty (dhamana) ya mwaka mmoja. Kwa kuingiza namba unazokuta kwenye kifuniko cha boksi lake.” anasema Lucho muuzaji wa iPhone kutoka kituo cha mabasi cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.