Unavyoweza kufahamu kama simu yako ina teknolojia ya eSIM
- Ni pamoja na kuangalia kupitia mipangilio ya simu.
- Unaweza kujua kupitia namba maalumu zinazokuwezasha kutambua kama simu yako ina teknolojia ya eSIM.
Dar es Salaam. Simu nyingi za kisasa zinaunga mkono eSIM, na baadhi ya chapa kubwa kama Apple na Samsung zimeshakuwa vinara wa teknolojia hii. Kwa makampuni makubwa ya simu kama Apple matoleo ya iPhone 15, iPhone 14, iPhone 13, iPhone 12, iPhone 11, iPhone SE (2020 na 2022) yote yanasapoti teknolojia hii.
Kwa upande wa kampuni ya Samsung pia matoleo kama Galaxy S23, Galaxy S22, Galaxy S21, Galaxy Z Flip 4, Galaxy Z Fold 4, Galaxy Note 20 Ultra yote yana uwezo wa kusapoti teknolojia ya eSim.
Hata hivyo, katika simu nyingi, unaweza kuangalia kama eSIM inapatikana kupitia mipangilio ya simu,kwa watumiaji wa iPhone unaweza kuangalia kupitia mipangilio ya simu kuwa kwenda kwenye ‘Settings’ kisha ‘Cellular’ au ‘Mobile Data’ kama una chaguo la ‘Add eSIM’ au ‘Add Cellular Plan’, basi simu yako inasapoti eSIM.
Kwa upande wa watumiaji wa Android, Samsung, Google Pixel, na nyingine unaweza kuangalia kama simu yako inasapoti teknolojia ya eSim kwa kwenda kwenye ‘Settings’ kisha ‘Connections’au ‘Network & Internet’, bofya ‘SIM Card Manager’, kama kuna chaguola’Add Mobile Plan’ au eSim basi simu yako inasapoti teknolojia hii.
Kwa baadhi ya simu, unaweza kuingiza code ifuatayo kwenye sehemu ya kupiga simu (Dialer) ili kuangalia kama eSIM inapatikana.
Unachotakiwa kufanya ni kufungua sehemu ya kupiga simu kisha kubofya *#06#, ikiwa kuna namba inayoitwa EID (Embedded Identity Document) inavyoonekana kwenye skrini, basi simu yako inaunga mkono eSIM.
Makampuni ya simu yanavyotazama mustakabali wa eSIM
Kampuni ya Apple imekwenda mbali zaidi na kuachana kabisa na slot ya SIM ya kawaida kwenye baadhi ya matoleo ya iPhone, ikisisitiza matumizi ya eSIM pekee, hasa katika masoko ya Marekani.
Kwa upande wa Samsung, kampuni hiyo inaendelea kuboresha teknolojia ya eSIM na kuhakikisha kuwa simu zake nyingi mpya zinatoa chaguo la eSIM kwa wateja wake.
Teknolojia ya eSIM inaleta mageuzi makubwa katika sekta ya mawasiliano. Kwa Tanzania, huduma hii inazidi kupata umaarufu huku mitandao kama Vodacom, Tigo, na Airtel wakihamasisha matumizi yake.
Ingawa bado kuna changamoto, faida zake zinaashiria kuwa eSIM huenda ikawa mustakabali wa mawasiliano ya simu, hasa kwa wale wanaotaka kubadilika na kuendana na kasi ya teknolojia mpya.