Simu za iPhone zinavyoweza kukupunguzia usumbufu mtandaoni

October 16, 2021 7:54 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kutumia teknolojia yake ya ‘Focus’ inayopatikana kwenye simu za iPhone 13.
  • Inasaidia kuipunguzia simu majukumu na usumbufu mwingine.
  • Teknolojia hiyo inasaidia kuongeza umakini wa kazi na shughuli zingine.

Dar es Salaam. Zipo nyakati unahitaji utulivu au unataka kujikita kutimiz amajukumu fulani na hautaki usumbufu wa kupigiwa simu au kupata arifa mbalimbali za mitandao ya kijamii na haujui ufanye nini. 

Suluhishi limepatikana, unaweza kuituliza simu yako kwa muda fulani bila kuizima na ukaendelea na shughuli zako.

Mfumo endeshi, (Operating System) wa iOS 15 uliambatana na mambo mapya mengi ikiwemo “share play” ya kusikiliza muziki mmoja au kutazama video pamoja kwenye simu za video za “faceTime”.

iOS 15 ni mfumo mpya unaotumika kwenye simu za iPhone ukiwa ni mfumobuliosasishwa baada ya iOS14.

Lingine ambalo ni jipya kwenye iOS15 ni mfumo wa “Focus” ambao umetengenezwa kuongeza umakini kwa mtu anapokuwa hahitaji bugdha ya simu.

Mfano pale unapokuwa kwenye kikao cha mtandaoni na mtu akakupigia, hiyo imekuondolea umakini na kikao chako na huenda ikaharibu uunganishwaji wa intaneti yako kwa sekunde au dakika kadhaa.

“Focus” inamwezesha mtu kutengeneza miundo (profiles) mbalimbali kwenye simu yake ambazo anaweza kuwa anachagua kulingana na sehemu alipo. 

Iwe kazini, wakati wa kulala, kuendesha gali na hata ibadani. Kupitia Focus, utaondoa arifa (notifications) zote usizozihitaji kwa muda fulani.


Unavyoweza kutumia Focus

Endapo umeshasasisha mfumo endeshi kuwa iOS15 katika simu ya iPhone, unaweza kuipata alama ya Focus kwenye sehemu ya udhibiti (control centre) ambayo inapatikana kwa kupangusa skrini yako kuelekea juu (swipe up). Utaona alama ya mwezi iliyoandikwa focus.  

Lakini kabla ya yote, unahitaji kuwa umetengeneza miundo yako binafsi katika matengenezo (settings).

Kuna miundo ya mazoezi, kujisomea, kuendesha gari, kucheza magemu, na kufanya kazi na muundo wowote unaotaka kutengeneza. Kwa kila muundo utaruhusu apps ambazo unaweza kupokea arifa zake huku zingine zote zikipigwa “stop” ya kukusumbua.

Unaweza kuchagua muundo unaouhitaji kwa wakati fulani na arifa za kukuondolea umakini zikapotezewa. Picha| The Verge.

Kutumia Focus unapohitaji

Kwa kuwa tayari umeshatengeneza miundo, pale unapokuwa sehemu fulani, tuseme unafanya mazoezi, utapangusa kuelekea juu na kisha utabonyeza neno focus ambapo utachagua muundo wa mazoezi.

Kwenye muudo huo, kama uliruhusu app ya muziki pekee kukutumia arifa ndio app pakee utakayopata arifa yake. Hakuna arifa ya simu itakayoingia wala ya ujumbe mfupi isopokuwa utawachagua wakati unatengeneza muundo huo.

Pia unaweza kuweka kikomo cha muundo huo kufanya kazi. Inaweza kuwa dakika na hata saa.

Baada ya muundo huo kuzimwa, arifa zako utazikuta ikiwemo simu ulizozikosa yaani “missed calls” na jumbe fupi pamoja na apps nyingine kama Instagram, WhatsApp na zinginezo.

Kupitia Focus pia, unaweza kuchagua watu kurudishiwa arifa ya kuwa upo kwenye muundo fulani. Mfano kama mtu akikutumia ujumbe na upo kwenye muundo wa kuendesha gari, atarudishiwa ujumbe mfupi wa kuwa unaendesha gari. Ujumbe wa kurudishiwa watu unaweza kuutengeneza mwenyewe au ukatumia uliopo.

Vivyo hivyo ukiwa unafanya mazoezi, umelala, upo kazini na kadhalika.

Focus inaweza kukuondolea arifa ambazo hauzihitaji kwa wakati fulani. Picha| The Verge.

Pia, unaweza kuchagua muundo fulani kujiwasha kiautomatiki kulingana na muda. Mfano kama huwa unakuwa kazini kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 11 jioni, unaweza kuiruhusu Focus ijiwashe kwenye muundo wa kazini kila inapofika saa mbili  na kujizima kila inapofika saa 11 kwa siku tano za kazi.

Kwa muundo wa kuendesha gari, unaweza kuiruhusu Focus ijiwashe kiautomatiki pale tu unapounganisha simu yako na “bluetooth” ya gari yako.

Huenda kama wewe ni mtumiaji wa simu za iPhone ukawa hauna sababu tena ya kusumbuliwa na arifa za simu pale unapokuwa unahitaji kuweka umakini wako kwenye jambo fulani. 

Mfumo huu pia unaweza kukusaidia kuepukana na ajali za barabarani endapo utautumia ukiwa unaendesha gari kwani mambo yote ya kukusumbua kiasi cha kukuondolea umakini ukiwa barabarani yanakuwa yamepigwa “stop”.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW